Saturday, January 24, 2015

UKAWA WAMEAMUA HAYA JUU YA MCHAKATO WA KATIBA

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjtkKWaScfzwSSOZaRTk5SC-AJ96zbCAoWqerXhRj0KNIHrXbkGEZ6QG-ji3FeVVi0-LqSKak_HgHMnnqTHsTRwX1c1Rbt0TK4z_GWnsrrEgwZ9o6pmYWMQk35azirPVU2RffnNFxKzK8Cl/s1600/ukawa5.jpg
Dar es Salaam. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimeeleza kuwa kuna matatizo mengi kwenye mchakato wa Kura ya Maoni na kutangaza rasmi kutoshiriki, vikidai vitahamasisha wananchi kuwaunga mkono.
Tamko hilo limekuja siku chache baada ya mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza kuwa uwezekano wa Kura ya Maoni kupigwa Aprili 30 ni mdogo na kwamba juhudi za kutaka azma hiyo itimie zinaweza kusababisha sheria kupindishwa.
Kauli yake iliungwa mkono na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye alisema uwezekano wa kupiga Kura ya Maoni siku hiyo ni mdogo na kwamba Serikali inahitaji kuwa makini ili kuhakikisha inapigwa Aprili 30.
Jana, vyama hivyo viliongeza uzito kwenye hoja hiyo ya kutaka mchakato huo usimamishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu vilipotoa tamko la pamoja la kususia mchakato huo, vikieleza kuwa muda uliosalia kukamilisha mchakato wa Kura ya Maoni ni mfupi, ikilinganishwa na maandalizi hafifu yanayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ambayo imetangaza uandikishaji katika Daftari la Wapigakura utaanza Februari 16.
Wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, Freeman Mbowe wa Chadema, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzina na Emmanuel Makaidi wa NLD, walitangaza msimamo huo jana baada ya kumalizika kwa kikao chao kwenye ofisi za makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam.
Profesa Lipumba ambaye alitoa tamko la Ukawa kujiondoa kwenye Bunge Maalumu la Katiba Aprili mwaka jana, alisema wamefikia uamuzi wa kutoshiriki katika Kura ya Maoni kwa sababu mchakato mzima haukuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Vyama vya siasa, ikiwemo CCM vilikubaliana mwaka jana kwamba Kura za Maoni ifanyike mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu, tulisaini wote na Rais Jakaya Kikwete alikubali,” alisema Lipumba.
Alisema jambo la kushangaza, Rais Kikwete aliwageuka na kutangaza kwamba Aprili 30, mwaka huu kuwa siku ya kupiga kura ya maoni.
“Tukashangaa Rais anatupiga chenga kwenye jambo kubwa kama hili ambalo tulishakubaliana naye kuwa lifanyike baada ya uchaguzi,” alisema.
Alisema pamoja na kutangaza siku ya kupiga kura, bado uandikishaji katika Daftari la Wapigakura haujaanza kwa sababu wanasubiri vifaa.
“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration (BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7,500, Tume inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika?” alihoji Lipumba.
Hata hivyo, juzi uongozi wa Nec ulisema Kura ya Maoni itafanyika kama ilivyopangwa licha ya vifaa hivyo kuchelewa kufika.

Ulisema muda uliobaki utatosha kwa asasi za kiraia kutoa elimu na vyama vya siasa kufanya kampeni.
Lipumba alisema historia ya mchakato huo imekuwa haishirikisha maoni ya watu na matatizo yanayojitokeza katika maandalizi ya Kura ya Maoni, wameamua kujitoa na hawatashiriki kutengeneza Katiba ambayo ni batili.
Naye Mbowe aliwaomba Watanzania wote kujitoa kwenye mchakato wa kura za maoni kwa sababu unalazimishwa na unafanyika bila ya kuwa na uhakika.
“Tumeamua kwamba hatuwezi kukengeuka na kushiriki kupigia kura kwenye mchakato ambao ni haramu. Tumeona tuwaachie CCM wenyewe wamalizie mchakato wao haramu,” alisema Mbowe.
Akifafanua zaidi Mbowe alisema Sheria ya Kura ya Maoni inataka Jaji wa Tanzania na Jaji wa Zanzibar kutengeneza kanuni ambazo wasioridhika kwenye kura ya maoni wanaweza kushtaki.
“Lakini hadi leo majaji hao hawajakaa kutengeneza kanuni hizo jambo ambalo tunaona mchakato huu hauna masilahi ya wananchi bali ya watu,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema mchakato mzima wa Katiba sasa `umeporwa’ na Ikulu kwa sababu hata kutangaza siku ya kupiga Kura ya Maoni kulitakiwa kufanywe na mwenyekiti wa Nec, lakini cha kushangaza Rais ndiye aliyetangaza.
Naye Mbatia alisema Katiba haitakuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Hatuwezi kushiriki kwenye Kura ya Maoni kwa sababu muda uliobaki hauruhusu, tunawaachia wenyewe CCM waendelee kuchakachua, sisi tunaona tusijihusishe kuleta Katiba haramu,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa NLD, Makaidi alisema amegundua mbinu za kuanza kuwasafirisha wananchi wa Bara kwenda kuishi Zanzibar kwa lengo la kupiga kura za ndiyo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Maoni ya wadau
Baadhi ya wasomi walioongea na gazeti hili jana, walikuwa na mawazo tofauti kuhusu tamko hilo.
Profesa Aidan Msafiri wa Chuo Kikuu cha Mtwara, alisema Serikali ni lazima izungumze na Ukawa ili kueleza kuhusu mchakato huo.
“Tunajenga nyumba moja kwa nini tugombanie fito, Serikali ni lazima iangalie hoja za Ukawa kama ni za msingi na ichukue hatua.”
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema Ukawa wameshaandaa ajenda yao ya kutokea katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema Ukawa hawana hoja na hawana huruma na mamilioni ya fedha zilizotumika katika mchakato wa Katiba mpya.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wameshasema kwamba muda uliobaki unatosha kufanya kampeni na kutoa elimu lakini wao wanajitoa,” alisema Bashiru.
Alisema siasa za Tanzania hivi sasa zimekuwa za vituko na matukio kwa sababu walitakiwa kusubiri ili kuona Nec wameshindwa kutekeleza zoezi hilo ndipo waamue kususia.

No comments: