HABARI YA UPOTOSHWAJI ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA
NIPASHE
KUNIHUSISHA NA KASHFA YA MABEHEWA FEKI YA TRL
Gazeti la Nipashe la tarehe 9/03/2015 toleo Na.
0578413 ambalo limeandika habari yenye kichwa cha habari “Mwakyembe atajwa
Kashfa ya TRL”.
Napenda
kutoa ufafanuzi kuwa habari hiyo iliyoandikwa ni uzushi mtupu wa kutaka
kunichafua. Nachelea kusema habari hii ni uzushi na porojo za kisiasa haswa
katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa
kunihusisha kwenye mchakato wa zabuni ya TRL ambao Waziri hana mamlaka nao
kikanuni na kisheria.
Kama
Waziri mwenye dhamana na Wizara baada ya kupokea malalamiko kuhusu mabehewa
yaliyonunuliwa na TRL kutokuwa na viwango vinavyokubalika, nilichukua hatua za
awali za kuunda tume ambayo ilanza mara moja kuchunguza suala hili ili
kujiridhisha na kutafuta ukweli wa jambo hilo.
Baada
ya kupokea taarifa ya awali ya uchunguzi uliofanywa na tume hiyo, nilichukua
uamuzi wa kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kuivunja Bodi ya Zabuni. Baada ya
bodi hiyo zabuni kuvunjwa, niliagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TRL iwasimamishe
kazi maafisa waandamizi wote wa TRL waliohusika katika mchakato wa manunuzi wa
mabehewa hayo ili kupisha uchunguzi uliokuwa ukiendelea kufanywa na tume.
Aidha, niliiagiza Wizara na Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kuiomba Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)ifanye uchunguzi wa kina wa mkasa
mzima, kazi ambayo nafahamu inaendelea kufanyika hadi sasa. Kwa msingi huo
habari iliyoandikwa kwenye gazeti la NIPASHE ya kunihusisha na kashfa ya sakata
hilo imenishtua na kunishangaza kwa kuwa kama ningekuwa nahusika kwa namna moja
au nyingine nisingeweza kuchukua hatua nilizozieleza hapo juu.
Gazeti la NIPASHE pia limehusisha suala la
mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yalyofanywa na Mhe. Rais, ambayo mimi
nimehamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwamba ni kwa sababu ya
kuniepusha na kadhia ya kashfa hiyo ya ununuzi wa mabehewa feki.
Hilo
ni jambo la kushangaza na uelewa mdogo wa mwandishi wa kutoelewa namna Serikali
inavyofanya kazi. Uamuzi wa kunihamisha Wizara umefanywa na Rais kwa sababu
tofauti kabisa na hizo za kusadikika zilizoandikwa na gazeti la NIPASHE. Kama
Rais aliona nina dosari, hakuwa na sababu kabisa kuniteua kumsaidia kuendesha
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imepata
fursa ya kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya.
Hivi
karibuni Mhe. Waziri Mkuu, alifanya ziara katika Mkoa wa Mbeya na wakati
akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kyela, Waziri Mkuu alitoa ufanunuzi mzuri
wa uamuzi uliochukuliwa na Mhe. Rais wa kuniamisha kutoka Wizara ya Uchukuzi
kwenda Wizara ya Ushirikano wa Afrika Mashariki, maelezo ambayo sina haja ya
kurudia kuyaeleza kwa sababu yalishatolewa kwenye vyombo vya habari.
Nimalizie kwa kusema kuwa Watanzania tuamke kwani
hakuna dosari yoyote ya mimi kuhamishiwa
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kupelekwa kwangu Afrika ya Mashariki
ambako nilianzia Ubunge, ni mkakati mzuri tu wenye tija.
Wenye
nia njema na nchi yetu wataafiki”.Naomba ifahamike kwamba sehemu kubwa ya nguvu
ya fedha ya washiriki wetu wa maendeleo sasa inapitia kwenye Jumuiya za kanda
kama Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo kwa sasa Mhe. Rais ni Mwenyekiti wa
Marais wa Jumuiya na mimi ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Hivi sasa niko njiani
natokea Marekani ambako niliongoza ujumbe mkubwa wa Mawaziri wan nchi tano (5)
za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadiliana na Serikali ya Marekani, pamoja na
mambo mengine, kuongeza muda wa sheria inayozipa fursa nchi za EAC kupeleka
bidhaa za biashara Marekani bila ushuru
(AGOA).
Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb)
WAZIRI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
No comments:
Post a Comment