Friday, March 6, 2015

HABARI PICHA--KAMATI YA KUDUMU YA MIUNDOMBINU WAITEMBELEA TMA LEO

Murugenzi wa mamlaka ya hali ya hewa Tanzania bi AGNES KIJAZI akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo mapema leo mbele ya wabunge ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya miundombinu waliofika katika nofisi za mamlaka hiyo leo katika ziara za kamati hiyo za kutembelea mamlaka zilizo chini yake.

Mjumbe wa kamati hiyo mh SAID HARFI na wajumbe wengine wakisiliza kwa makini katika mkutano huo

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya miundombinu ya bunge JUMA KAPUYA akizngumza katika kikao cha kamati hiyo wakati walipotembelea mamlaka ya hali ya hewa jijini Dar es salaam leo

Wajumbe hao wakaamua kutembelea na kuona jinsi utendaji kazi wa mamlaka hiyo unavyoendelea ambapo hapa wanashughudia moja ya vituo vya kupima hali ya hewa Tanzania kituo ambacho kinaendeshwa na wataalam kutoka Tanzania 

SOMA TAARIFA NZIMA JINSI TMA WANAVYOENDESHA KAZI ZAKE



1.0    UTANGULIZI


1.1     Historia Fupi


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa rasmi mwaka 1999 kwa Sheria Namba 30 ya uanzishwaji wa Wakala (Executive Agencies Act Na.30 of 1997) kuchukua nafasi ya iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa (Directorate of Meteorology). Mabadiliko hayo yalilenga kuongeza ufanisi katika kutoa huduma za hali ya hewa.

 Idara kuu ya Hali ya Hewa ilianzishwa Mwaka 1978 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ikiwa na jukumu la kupima, kukusanya, kuchambua, kuhifadhi na kutoa taarifa za hali ya hewa nchini. Kabla ya hapo huduma hizo zilikuwa zikitolewa na Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Mashariki (EAMD).  

1.2     Dira na Dhamira

1.2.1        Dira ya TMA:

Dira ya Mamlaka ya Hali ya Hewa ni  ‘Kuwa kitovu bora cha utoaji wa huduma za hali ya hewa zenye hadhi ya kimataifa ifikapo mwaka 2015’.

1.2.2        Dhamira ya TMA

Dhamira ya Mamlaka ya Hali ya Hewa ‘Kutoa huduma za hali ya hewa zilizo bora, zinazokidhi matarajio ya wadau na hivyo kuchangia katika kulinda maisha yao, mali, mazingira na pia kuchangia katika azma ya Taifa ya kupunguza umaskini’.

1.2.3        Kaulimbiu ya utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa (Quality Statement)


Kaulimbiu ya Mamlaka katika utoaji huduma bora za hali ya hewa kulingana na viwango vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Viwango Ulimwenguni (ISO) ni ‘Sisi, wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania tumedhamiria kutoa huduma bora zenye kukidhi matarajio ya wadau wetu kwa kufuata misingi na viwango vilivyokubalika kitaifa na kimataifa kwa kuendelea kuboresha taratibu zetu za kazi’

1.3     Muundo wa TMA


Kwa sasa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Uchukuzi. Mamlaka inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu ambaye anawajibika kwa Katibu Mkuu wa Wizara. Mamlaka ina Bodi ya Ushauri (MAB) ambayo inaundwa na wajumbe saba akiwemo Mwenyekiti ambapo Mkurugenzi Mkuu ni katibu wa Bodi.

Mamlaka imegawanyika katika Divisheni nne ambazo ni: Huduma za Utabiri, Huduma za Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Huduma za Ufundi na Huduma Saidizi na ofisi ya Zanzibar ambazo huongozwa na Wakurugenzi wakisaidiwa na Mameneja wa Idara mbalimbali kama inavyoonekana kwenye Jedwali Na.1. Mamlaka pia ina Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma.

Jedwali Na.1: Muundo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania [TMA]

                                                                                                                                                                                               

           






































SURA YA PILI



2.0     UBORESHAJI WA  HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI


Mamlaka imeendelea na utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya maendeleo (Vision 2025), MKUKUTA na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.

Katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano, Mamlaka imetengewa maeneo 8 ya utekelezaji ambayo yanatekelezwa kwa awamu mbalimbali ili kuhakikisha vipaumbele vya Mamlaka vinazingatiwa na kutekelezwa kikamilifu. Aidha, maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2015/16 yamezingatia mahitaji na vipaumbele hivyo katika kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.

2.1     Majukumu ya Mamlaka.


Katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa inao wajibu mkubwa wa kusimamia masuala yote yanayohusiana na hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa tahadhari ya majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa pamoja na matukio ya TSUNAMI na kubadilishana taarifa na data za hali ya hewa katika mtandao wa dunia kulingana na makubaliano ya kimataifa.

Katika kutimiza wajibu huo, Mamlaka inatekeleza majukumu yafuatayo:-

1.1     Kuanzisha na kuendesha vituo vya hali ya hewa ili kupata data na taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kutoa huduma za hali ya hewa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii hasa katika sekta za kilimo, usafiri na uchukuzi, miundombinu, maji, nishati, mazingira, utalii, n.k.

1.2     Kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, muda wa siku 10, mwezi na wa msimu na kutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa na kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia walengwa katika muda muafaka.

1.3     Kufuatilia, kupima na kufanya utafiti wa kisayansi kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini (Climate change).

1.4     Kuendeleza na kutunza mtandao wa vituo vya kupima na kuangaza hali ya hewa ili kukidhi makubaliano ya kimataifa ya kushirikiana katika kubadilishana data na taarifa za hali ya hewa na nchi nyingine duniani kwa usalama wa watu na mali zao.

1.5     Kushirikiana na taasisi za kanda na za kimataifa kuhusu shughuli za hali ya hewa kama vile (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC); Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

1.6     Kuiwakilisha nchi katika masuala yote yanayohusu hali ya hewa kimataifa ambapo Mkurugenzi Mkuu ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika shirika la Hali ya Hewa Duniani (Permanent Representative of Tanzania with the World Meteorological Organization (WMO)).

1.7     Kuhakikisha Mamlaka ina wataalamu wa kuiwezesha kutimiza majukumu yake kulingana na makubaliano ya kimataifa.

2.2     HUDUMA ZITOLEWAZO NA MAMLAKA


Mamlaka katika utekelezaji wa majukumu yake hutoa huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kilimo, usafiri wa anga, usafiri wa kwenye maji na usafiri wa nchi kavu; ulinzi na usalama, ujenzi, maji, nishati,  utalii, utaratibu wa kukabiliana na maafa na nyinginezo kama zinavyooneshwa kwenye Jedwali namba 2. Huduma za hali ya hewa zitolewazo na Mamlaka kwa sekta ya Usafiri wa Anga zimefikia viwango vya kimataifa (ISO 9001:2008 certified Aeronautical Meteorological Services).

Jedwali Na.2: Huduma zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini.

Na.
SEKTA
HUDUMA ZITOLEWAZO
1.
KILIMO
·         Taarifa za hali ya hewa zinazomsaidia mkulima kupanga shughuli za kilimo, hususani utayarishaji wa mashamba, muda wa kupanda, aina ya mbegu, upaliliaji, unyunyiziaji dawa, uwekaji mbolea na uvunaji na uhifadhi wa mazao.
·         Mwanzo na ukomo wa misimu ya mvua humsaidia mkulima kupanga aina za mazao.
·         Kuwajengea wafugaji uwezo wa kuratibu shughuli za ufugaji kulingana na taarifa za hali ya hewa za misimu.
·         Nguvu na Mwelekeo wa upepo kwa ajili ya shughuli za uvuvi
·         Taarifa za mnururisho (evaporation) na upepo kwa ajili ya Kilimo cha umwagiliaji.

2.
NISHATI


·         Taarifa kuhusu mielekeo ya upepo kwa ajili ya uzalishaji wa nishati itokanayo na upepo.
·         Taarifa kuhusu upatikanaji wa nguvu ya mionzi ya jua kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jua.
·         Taarifa za hali ya joto kwa ajili ya kazi za kikemikali, mvua kwa ajili ya “river discharge” na hali ya hewa kwa ujumla kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya gesi (natural gas).
·         Taarifa za mnururisho (evaporation) kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya maji.
·         Mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kuathiri uzalishaji wa nishati mbali mbali.

3.
MADINI
·         Utabiri wa hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa madini.
·         Utabiri kuhusu mafuriko kwa usalama wa wachimbaji.
·         Urefu wa vipindi vya kiangazi na masika katika kupanga muda wa kuchimba madini.
·         Hali ya bahari kwa ajili ya uzalishaji wa madini ya chumvi.
·         Data za hali ya hewa kuhusu unyevunyevu (humidity), joto, upepo na mvua kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.
4.
ULINZI NA USALAMA
·         Utabiri wa hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za kijeshi angani.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya mipangilio ya shughuli za kijeshi kama vile mazoezi porini, kulenga shabaha n.k.
·         Mafunzo kwa wanajeshi kuhusu namna ya kutabiri hali ya hewa kama sehemu muhimu ya operesheni za kijeshi.
·         Mafunzo na mitihani ya kupima uelewa wa hali ya hewa kwa marubani wa ndege za kijeshi.

5.
USAFIRI WA ANGA
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kupaa na kutua kwa ndege.
·         Utabiri wa hali ya hewa kwa ajili ya usalama wa njia za ndege (route forecast).
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kuegesha ndege.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya huduma mbalimbali za wasafiri.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za uokoaji na utafutaji (Search and Rescue).
·         Taarifa za hali ya hewa hususani mwelekeo wa upepo kwa ajili ya usalama wa ndege na abiria.
·         Mafunzo na upimaji viwango vya ubora kwa marubani wa ndege za kiraia katika taaluma ya hali ya hewa.
·         Mafunzo kwa maafisa waongoza ndege.

6
USAFIRI WA NCHI KAVU NA KWENYE MAJI
·         Taarifa za utabiri na viwango vya mvua wakati wa kupanga na kujenga miundombinu ya barabara
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya huduma mbalimbali za wasafiri.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za uokoaji na utafutaji (Search and Rescue).
·         Taarifa za upepo na mwelekeo wake
·         Taarifa za urefu wa Mawimbi
·         Taarifa ya hali ya joto la bahari
·         Taarifa ya unyevu ili kutambua hali ya barabara
·         Taarifa za upeo wa kuona (visibility)
·         Taarifa za mvua


7.
VIWANDA
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kuzuia uchafuzi wa mazingira.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa viwanda, sehemu ya kujenga viwanda hivyo na matumizi sahihi ya mashine za ujenzi kulingana na hali ya hewa.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya utupaji na uteketezaji wa taka za viwanda.

8.
UTALII
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kupanga shughuli za utalii kama vile muda mzuri kwa watalii ambapo wanyama wengi wapo katika mbuga zetu za Taifa ukizingatia wanyama huhama kulingana na hali ya hewa (movement of wildlife) hata wakati mwingine kuvuka mipaka.
·         Mwelekeo wa upepo kwa ajili ya safari za Maputo (hot air balloons), n.k.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa usalama wa watalii na mali zao.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya usimamizi wa rasimali ya wanyamapori.
9.
UJENZI
·         Kiasi cha mvua kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
·         Hali ya joto kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
·         Taarifa kuhusu mielekeo na kasi ya upepo.
·         Maelezo kuhusu joto na unyevunyevu wa anga.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya mipango ya ujenzi.

10.

TAASISI ZA ELIMU NA UTAFITI
·         Kutoa waalimu wanaofundisha masuala ya hali ya hewa.
·         Mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi.
·         Kushirikiana katika tafiti mbali mbali.
·         Data za hali ya hewa kwa utafiti wa kilimo, afya, uvuvi, maji, mifugo nk..
·         Kushiriki katika uchambuzi wa tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi.
11.
MAJI NA MAZINGIRA
·         Taarifa za mvua.
·         Taarifa za mnururisho (evaporation) na joto.
·         Taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua.
·         Utabiri kuhusu mafuriko, mipango ya umwagiliaji na kupungua kwa vina vya maji katika mito sehemu mbali mbali nchini.
·         Taarifa ya hali ya hewa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya maji.
·         Mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la joto duniani. (Global Warming).
·         Taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake katika mazingira.
12.
MENEJIMENTI YA MAAFA
·         Utabiri wa hali ya hewa ya mwelekeo wa misimu mbali mbali ya mvua.
·         Taarifa za nyongeza kuhusu mwenendo wa msimu hutolewa mara kwa mara.
·         Taarifa za kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.
·         Tahadhari dhidi ya hali mbaya ya hewa, hususani vimbunga, upepo mkali, mvua kubwa, ukame nk.
·         Mamlaka ya Hali ya Hewa hushiriki kama mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Maafa.
13.
UMMA
·         Utabiri kwa ajili ya shughuli za kila siku za wananchi kama vile sherehe, mikutano nk..
·         Mipangilio ya shughuli za kitaifa.
·         Machweo na mawio ya jua.
·         Tahadhari dhidi ya majanga kama vile mafuriko, kiangazi, radi n.k.
·         Utabiri kwa ajili ya uandaaji wa ratiba za michezo mbali mbali ambayo inaweza kuvurugwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
14.
MENGINEYO
·         Makampuni ya Bima na Mabenki.
·         Shule za msingi na sekondari.
·         Taasisi za Kimataifa.
·         Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs)
·         Taasisi za dini
·         Nk.

2.3     Malengo ya Mamlaka:


Katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinakuwa endelevu na zinaboreshwa, Mamlaka imejiwekea malengo makuu tisa (9) ya utekelezaji wa shughuli zake kupitia Mpango Mkakati ambayo ni:-
                    i.            Kutoa huduma bora na za uhakika za hali ya hewa;
                  ii.            Kuajiri wafanyakazi wa kutosha, kutoa mafunzo na kuhakikisha matumizi ya nyenzo mbalimbali yanafanyika;
                iii.            Kuwa na Vifaa na mitambo ya kisasa ya hali ya hewa;
                iv.            Uboreshaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa utoaji wa huduma za hali ya hewa;
                  v.            Kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya hali ya hewa;
                vi.            Kuongeza uelewa wa huduma za hali ya hewa kwa wananchi;
              vii.            Uboreshaji wa mahusiano ya kimataifa katika masuala ya hali ya hewa;
            viii.            Kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa; na
                ix.            Kutoa elimu kwa wafanyakazi ili kupunguza madhara yatokanayo na UKIMWI na kuboresha huduma.





SURA YA TATU

3.0     MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MALENGO YA MAMLAKA KATIKA KIPINDI CHA FEBRUARI 2014 MPAKA FEBRUARI 2015

3.1     UTAYARISHAJI NA USAMBAZAJI WA TAKWIMU NA TAARIFA ZA HALI YA HEWA


3.1.1        UPIMAJI  WA HALI YA HEWA


Chanzo kikuu cha taarifa za hali ya hewa ni kazi ya upimaji ambayo hufanywa katika vituo mbalimbali vya hali ya hewa nchini vinavyojumuisha vituo vikuu 29, vituo vya hali ya hewa na kilimo 15 n.k. Upimaji wa hali ya hewa hufanyika katika uso wa dunia (bahari na nchi kavu) na Anga za Juu kama inavyooneshwa kwenye picha namba 1.

Upimaji wa hali ya hewa ya Anga za Juu huhusisha vifaa na njia mbalimbali ikiwemo Satelaiti, Ndege, Maputo Makubwa n.k. Uangazi kwenye uso wa dunia (bahari na nchi kavu) huhusisha vifaa na vituo mbalimbali vya nchi kavu na kwenye maji.

Picha Na.1: Mtandao wa Uangazi Duniani

GOS-fullsize 2007
gos

Mamlaka inamiliki na kuendesha Mtandao wa Vituo vya kupima na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa nchini kama inavyooneshwa kwenye picha namba 2 hadi 4. Baadhi ya vituo katika mtandao huo hasa vile vya kupima mvua na vile vya hali ya hewa na kilimo, huendeshwa kwa ushirikiano na baadhi ya taasisi hapa nchini kama vile shule, vijiji, vituo vya utafiti, taasisi za dini, Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya Maji na Umwagiliaji n.k. Hata hivyo vituo vilivyopo havikidhi mahitaji. Hali halisi ya vituo na mahitaji imeonyeshwa kwenye Jedwali namba 3.




Jedwali Na.3 Mtandao wa Vituo na Mahitaji halisi:

Aina ya vituo
Vilivyopo
Pungufu
1.
Vituo Vikuu vya Hali ya Hewa
29
3
2.
Vituo vya Kupima Hali ya Hewa ya Anga la Juu
1
3
3.
Vituo vya Hali ya Hewa na Kilimo
15
5
4.
Vituo vya Klaimatolojia
60
100
5.
Vituo vya Hali ya Hewa vinavyojiendesha vyenyewe (AWS).
13
88
6.
Vituo vya Rada ya Hali ya Hewa
1
5
7.
Vituo vya kupimia Mvua
500
-
8.
Vituo vya kupima Mvua vinavyojiendesha vyenyewe
0
2500

Picha Na 2: Vituo vya Hali ya Hewa vilivyopo na vinavyotarajiwa kuanzishwa
Stations-expected-7-5





































Picha Na.3: Baadhi ya vifaa vya hali ya hewa


dsc01519
dsc01522
dsc01520
dsc01507




















Picha Na 4: Mtambo wa kupima hali ya hewa ya anga ya juu (Upper Air) uliopo JNIA

Katika kuboresha mtandao wa vituo vya hali ya hewa nchini, Kituo kipya cha hali ya hewa cha Songwe kimeanza kutoa huduma katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe. Mamlaka imefanikiwa pia kufanya ukarabati wa vituo na Ofisi za hali ya hewa katika maeneo ya Dodoma, Tabora na Mlingano. Huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa maji zimeboreshwa kwa kuanzisha ofisi huko Mwanza. Maandalizi ya  kuanza kutoa huduma hizo huko Kigoma yapo kwenye hatua za mwisho.

Mamlaka kupitia miradi ya washirika wa maendeleo pia imefanikiwa kununua na kufunga Mitambo 8 ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe katika sehemu mbalimbali nchini kama na pia iko katika mchakato wa ununuzi wa Mitambo mingine 16 kupitia miradi ya washirika wa maendeleo. Picha namba 5 inaonesha mtambo wa kupima hali ya hewa unaojiendesha wenyewe.


Picha Na. 5: Mtambo wa kupima hali ya hewa unaojiendesha wenyewe.

Aidha, Mamlaka kupitia karakana yake iliyoko katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa JNIA imefanikiwa kutengeneza ‘standard raingauges’ zaidi ya 150 na minara ya vifaa vya hali ya hewa. Karakana hiyo imeongezewa uwezo wa kutengeneza baadhi ya vifaa ambavyo ni  ‘Stevenson screen’ pamoja na ‘evaporation pan’.Picha namba 6 ni sehemu ya ‘standard raingauges’ zilizotengenezwa.


Picha Na.6: Vifaa vilivyotengenezwa katika karakana ya Mamlaka.

Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa (barometers) unaendelea kufanyika kupitia mtambo wa Mamlaka ulioko JNIA. Uhakiki wa vipima joto (Thermometers calibration) umefanyika kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).Picha Namba 7 ni mtambo wa uhakiki wa barometers.


Pressure Calibration Unit

Picha Na 7: Pressure Calibration Unit iliyopo katika karakana ya Mamlaka JNIA

Mamlaka imekamilisha ufungaji wa rada ya pili ya hali ya hewa huko Kiseke, Mwanza. Rada hiyo imeishafanyiwa majaribio na sasa inafanya kazi chini ya kipindi cha uangalizi wa mtengenezaji kulingana na taratibu. Miundombinu ya Kituo cha Radar Kiseke imekamilika ikihusisha uzio, kibanda cha mlinzi pamoja na uwekaji wa umeme. Picha namba 8-10 ikionesha kituo cha Radar Kiseke Mwanza na ramani ya mtandao wa rada nchini.

DSC07129
20140912_123816

Picha Na.8: Kituo cha Radar Kiseke Mwanza.

DSC02171
Picha Na.9: Barabara ya kuelekea eneo la kituo cha Radar ya Hali ya Hewa Kiseke, Mwanza.
Kulingana na mahitaji ya kufuatilia mifumo ya hali ya hewa nchini Mamlaka inatakiwa kuwa na mtandao wa Rada saba za hali ya hewa .
radar6
               Picha Na. 10: Maeneo ya mtandao unaohitajika wa Vituo vya Rada nchini.

3.1.2        MAWASILIANO YA DATA NA TAARIFA ZA HALI YA HEWA


Taarifa za hali ya hewa hazina mipaka, hivyo ni jukumu la Mamlaka ya Hali ya Hewa kubadilishana data  na taarifa za hali ya Hewa kikanda na kimataifa kwa kutumia mtandao wa mawasiliano wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani. Picha namba 11 ikionesha Mtandao wa Mawasiliano ya hali ya hewa Duniani



Picha Na 11: Mtandao wa Mawasiliano ya hali ya hewa Duniani

Aidha, upimaji hufanyika vituoni ambapo mtandao wa mawasiliano husaidia kufikisha data hizo katika Kituo Kikuu cha Utabiri nchini kwa uhakiki na uchambuzi kwa ajili ya kubadilishana kikanda na kimataifa na kwa ajili ya kuandaa utabiri wa hali ya hewa. Picha namba 12 ikionesha Mtandao wa Mawasilano ya hali ya hewa Tanzania.


Picha Na 12: Mtandao wa Mawasilano ya hali ya hewa Tanzania

Mamlaka imeendelea kuboresha mitambo yake ya mawasiliano, na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa inayohusisha mitambo ya TRANSMET na AFTN . Picha namba 13 ikionesha Mtambo wa Mawasilano ya hali ya hewa TRANSMET

Katika kuhakikisha kunakuwa na utayarishaji endelevu wa taarifa za hali ya hewa, Mamlaka imenunua na kufunga Mtambo wa kuhifadhi umeme pindi unapokatika ili kuhakikisha data na taarifa za hali ya hewa zinapokelewa kutoka vituoni na kutumwa katika mfumo wa Kimataifa.

Aidha, kwa kutumia wataalamu wake, Mamlaka imefanikiwa kubuni na kutengeneza mfumo wa mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa kutoka vituoni unaoitwa DMO ambao umerahisisha upatikanaji wa data za hali ya hewa.


Picha Na 13: Mtambo wa Mawasilano ya hali ya hewa TRANSMET

3.1.3    UCHAMBUZI WA DATA ZA HALI YA HEWA


Uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa hufanyika baada ya kukusanywa kwa takwimu za hali ya hewa katika kituo kikuu cha utabiri nchini. Uchambuzi huu hufanyika ndani ya saa 24 kwa kutumia mitambo mbalimbali ya hali ya hewa kama vile Aeromet web, SYNERGIE na Kompyuta (Computer Clusters) ukihusisha pia na wataalamu waliobobea. Matokeo ya uchambuzi huo hupelekea kupatikana kwa utabiri wa kila siku, siku 5, 10, mwezi na msimu pamoja na utoaji wa tahadhari ya hali mbaya ya hewa.

Mamlaka imeendelea kuboresha mifumo yake ya uchambuzi ikihusisha ununuzi wa mtambo mpya wa kisasa wa Aeromet web na pia kuboresha (upgrade) mtambo wa SYNERGIE. Uboreshaji huu umeendana na utoaji wa mafunzo kwa mafundi na wataalamu wa hali ya hewa ili kuwa na matumizi endelevu ya vifaa na mitambo ya hali ya hewa. Picha namba 14 ikionesha uboreshaji na mafunzo ya mtambo wa uchambuzi wa hali ya hewa SYNERGIE


Picha Na 14: Uboreshaji na mafunzo ya mtambo wa uchambuzi wa hali ya hewa SYNERGIE

Aidha, Mamlaka pia imekamilisha majaribio ya Mtambo wa kuchambua data za hali ya hewa (Computer Cluster).




















Picha Na 15: Mtambo wa kuchambua data za hali ya hewa (Computer Cluster) iliyofungwa huko JNIA

Uchambuzi wa taarifa za hali ya hewa kwa kutumia ‘Computer Cluster’ umeanza kusaidia kutoa utabiri katika maeneo madogo madogo ya nchi ikiwemo Ziwa Nyasa na Tanganyika.
















Picha Na 16: Utabiri kuhusu Upepo (10 meter winds) katika Ziwa Nyasa na mvua inayotarajiwa katika kipindi cha saa tatu (27/02/2015)

Uboreshaji huu wa mifumo ya uchambuzi wa data za hali ya hewa umesaidia katika ubadilishanaji wa data za hali ya hewa, uchambuzi wake na pia utabiri wa hali hewa na hivyo kuendana na ukuaji wa mahitaji ya huduma za hali ya hewa nchini. Picha namba 15-16 ikionesha mtambo wa Computer Cluster na utabiri kwa Ziwa Nyasa.

3.1.4        UTABIRI WA HALI YA HEWA


Mamlaka imeendelea kutoa utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku kumi, mwezi na msimu. Katika kipindi husika, viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka vimeendelea kuongezeka na kufikia asilimia 78.9 kwa utabiri wa siku na asilimia 87.5 kwa utabiri wa msimu. Picha namba 17 ikionesha utabiri wa Msimu wa Mvua za Masika (MAM, 2015)



















Picha Na 17: Utabiri wa Msimu wa Mvua za Masika (MAM, 2015)

Aidha, Mamlaka imeendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri na tahadhari ya hali mbaya ya hewa. Tahadhari hizi zimesaidia kupunguza na kuzuia madhara ya matukio yatokanayo na hali mbaya ya hewa katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Picha namba 18 ikionesha baadhi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa (Mvua kubwa Dar es Salaam 12 Aprili, 2014 na Kahama Shinyanga 03/03/2015)

 

Picha Na 18: Baadhi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa (Mvua kubwa Dar es Salaam 12 Aprili, 2014 na Tufani iliyotokea Kahama Shinyanga 03/03/2015)

3.1.5    USAMBAZAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA


Mamlaka imeendelea kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na Mamlaka na Taasisi za Serikali. Vyombo hivyo vinajumuisha magazeti 5, radio zaidi ya 23 na luninga  6 na mitandao karibu yote ya kijamii iliyopo nchini. Picha namba 19 ikioneshab njia zinazotumiwa na Mamlaka (TMA) kusambaza taarifa za hali ya hewa


Picha Na 19: Njia zinazotumiwa na Mamlaka (TMA) kusambaza taarifa za hali ya hewa

Mamlaka pia imeendelea kushiriki katika Siku ya Hali ya Hewa Duniani na maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na Nane nane ambapo katika maonesho ya Nane nane, Mamlaka ilishiriki katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro. Shughuli hizi zimekuwa zikielimisha  umma kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na umuhimu wa kutumia taarifa za hali za hewa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Picha namba 20 ikionesha wananchi wakitembelea banda la maonesho ya Nanenane huko Mbeya na kupata maelezo kutoka kwa mfanyakazi wa Mamlaka

DSC00129 

Picha Na 20: Wananchi wakitembelea banda la maonesho ya Nanenane huko Mbeya na kupata maelezo kutoka kwa mfanyakazi wa Mamlaka

Mamlaka imefanikiwa kuboresha studio ya hali ya hewa kwa kubadilisha Studio hiyo toka mfumo wa zamani wa Analojia kwenda mfumo wa kisasa wa digitali. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari, Mamlaka imekuwa ikiandaa warsha mbalimbali zinazowahusisha wahariri na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa namna ya kusambaza kwa usahihi taarifa za hali ya hewa kwa jamii na mrejesho wa mapokeo ya utoaji huduma za hali ya hewa nchini. Picha namba 21 ikionesha wadau wa sekta mbalimbali na wahariri wa vyombo vya habari wakati wa warsha inayohusu utabiri wa mvua za msimu MAM 2015

Picha Na 21: Wadau wa sekta mbalimbali na wahariri wa vyombo vya habari wakati wa warsha inayohusu utabiri wa mvua za msimu wa Machi-Mei 2015, iliyofanyika Kibaha, Pwani tarehe 26/02/2015.

Mamlaka imeanzisha utaratibu wa kupata mrejesho kutoka kwa jamii kwa njia ya mitandao ya kijamii na simu za mkononi kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa nchini. Mamlaka pia inatoa utabiri kwa sekta mbalimbali ikiwemo Afya na Kilimo kwa kutumia mfumo wa MAPROOM kama inavooneshwa katika picha namba 22.
Picha Na.22: Mfumo wa MAPROOM

3.2     MFUMO WA UTOAJI HUDUMA BORA KWA USAFIRI WA ANGA (QUALITY MANAGEMENT SYSTEM (QMS) FOR AERONAUTICAL METEOROLOGICAL SERVICES)


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea kutoa huduma bora za hali ya hewa kulingana na viwango vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Viwango Ulimwenguni (ISO). Utekelezaji wa mfumo huu (QMS) umefanyika kwa vituo saba vilivyo katika viwanja vya ndege kwa kuongezewa wafanyakazi, kufungwa baadhi ya vifaa vipya na vifaa kufanyiwa uhakiki (calibration). Ukaguzi wa awali wa Kimataifa ulifanyika mwezi Novemba, 2011 na Mamlaka ilifanikiwa kupata Cheti cha utoaji huduma bora za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa Anga (ISO 9001:2008). Ukaguzi huo umeendelea kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu (3)  ya uhai wa cheti hicho. Mwaka 2014 ukaguzi mwingine ulifanyika na Mamlaka kufanikiwa kupata cheti ambapo kitadumu kwa miaka mitatu ijayo kwa kufanyiwa ukaguzi wa ufuatiliaji kila mwaka kama picha namba 23 hadi 24  zinavyoonesha.






















Picha Na 23: Ukaguzi wa huduma za hali ya hewa kwa ajili ya Usafiri wa Anga (ISO 9001:2008) uliofanywa na Kampuni ya Certech kutoka Canada





QMS Certificate_2013

Picha Na 24: Cheti cha utoaji wa huduma bora za hali ya hewa kwa ajili ya Usafiri wa Anga (ISO 9001:2008)

3.3     KUSHIRIKI KATIKA MASUALA YA KITAIFA NA KIMATAIFA YANAYOHUSIANA NA HALI YA HEWA.


Mamlaka ya Hali ya Hewa inaiwakilisha Tanzania katika masuala yote yanayohusu hali ya hewa kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni na pia ni mjumbe katika Baraza Kuu la Shirika hilo (WMO Executive Council).

Katika kutekeleza jukumu hilo, TMA imeshiriki kikamilifu katika kutekeleza programu mbalimbali za Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni (WMO) ambapo wataalam wa Mamlaka ni wajumbe katika Tume (Commisions) mbalimbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani na pia wamekuwa wakishiriki katika semina na mikutano mbalimbali kikanda na kimataifa.  Aidha, Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya kikanda inayohusu masuala ya hali ya hewa. TMA imeendelea kutekeleza vyema jukumu iliyokabidhiwa na WMO la kutoa utabiri wa hali mbaya ya hewa (Severe Weather Forecast) katika nchi za Afrika Mashariki zilizoko katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Mkutano wa Waheshimiwa Mawaziri wa Afrika wanaosimamia taasisi za hali ya hewa ulifanyika Cape Verde huko Afrika ya Magharibi na kwa sauti moja waheshimiwa walikubaliana kuboresha huduma za hali ya hewa katika Afrika pamoja na kuzingatia ukomo wa muda “deadlines” zilizowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga duniani na Shirika la Hali ya Hewa duniani ambazo ni:-

·         Huduma za hali ya hewa kwa Usafiri wa Anga zinatakiwa ziwe zinatolewa na wataalamu wa hali ya hewa wenye shahada ya kwanza ya hali ya hewa kuanzia Disemba, 2016
·         Kuanzisha utaratibu wa kupima utendaji kazi wa wataalamu wa hali ya hewa (Competency Assessment) kuanzia mwezi Disemba, 2013
·         Kuanza kutumia mfumo mpya wa kutuma data za hali ya hewa (TDFC) kikanda na kimataifa kuanzia mwezi, Novemba, 2014
·         Kuwa na mfumo wa utoaji wa huduma bora zinazotambuliwa na Shirika la Viwango Duniani (ISO) kwa ajli ya Usafiri wa Anga kuanzia mwezi Novemba, 2012

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa imeweza kuzisaidia nchi nyingine kuboresha shughuli za hali ya hewa kwa kutoa utalaamu wa aina mbalimbali katika Nyanja za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na ufungaji wa vifaa vya kisasa vya mfumo wa kimahesabu wa utabiri (Numerical Weather Prediction) huko Uganda, Burundi na Rwanda. Kwa upande wa ‘Competency Assessment, nchi zilizosaidiwa ni pamoja na Saudi Arabia, Nigeria na Libya.

3.4     UTAFITI ULIO BORA WA HALI YA HEWA KWA LENGO LA KUBORESHA HUDUMA


Mamlaka katika kuboresha uhifadhi wa data zinazopokelewa kutoka vituo mbalimbali hapa nchini, imefanikiwa kuhama kutoka mfumo wa zamani wa CLICOM wa kuingiza na kuhifadhia data na kuhamia kwenye mfumo wa kisasa wa CLIDATA ambao umeleta ufanisi katika utendaji kazi na usalama wa data. Aidha, Mamlaka inaendelea na zoezi la kuokoa data (data rescue) na kuhifadhi data katika mfumo wa kidigitali (softcopy) kutoka katika hifadhi za karatasi (hardcopy) kama picha namba 25 inavyoonesha.


Picha Na.25:  Hifadhi ya data za hali hewa (Archive) na mfumo wa kigitali wa uhifadhi (CLIDATA)

Mamlaka imeendelea kufanya semina za mabadiliko ya hali ya hewa (Climate Change) na changamoto zake katika shule mbalimbali za sekondari hapa nchini ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kama picha namba 26 inavyoonesha.






Picha Na 26: Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti Dkt Ladislaus Chang’a akitoa maelezo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Nawenge huko Mahenge, Morogoro.

Mamlaka imeendelea kushiriki katika kufanya tathmini ya hali ya chakula nchini ikishirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ambapo kazi hii imesaidia katika uhifadhi na ugawaji wa Chakula pale inapohitajika.

Katika kuboresha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wakulima na wafugaji, Mamlaka kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine imetayarisha mfumo wa ujumbe mfupi kwa mkulima (Farm SMS) kupitia simu za mikononi ili kuweza kupata taarifa za hali ya hewa hadi ngazi ya vijijini kwa kuanzia na maeneo ya Same, Monduli, Longido, Kiteto, Chamwino, Ngorongoro Lushoto na Sengerema.

Mamlaka imefanikiwa kuanzisha utoaji wa matoleo ya taarifa ya mwaka ya hali ya hewa kwa Tanzania (TMA Statement on the Status of the National Climate). Mamlaka pia imefanikiwa kuanzishwa matoleo ya Jarida la Utafiti wa hali ya hewa nchini (TMA Research Journal) ambapo tayari matoleo mawili (2) yalishatoka na matayarisho kwa toleo la tatu (3) yako katika hatua za mwisho.

Mamlaka imefanikiwa kukamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa utabiri wa jadi (indigenous knowledge in weather and climate prediction) unaohusisha utafiti  uliokuwa unafanyika kwa Tarafa za Ismani na Mahenge kwa mafanikio makubwa. Aidha, Mamlaka inaendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ambayo imejikita zaidi katika utoaji wa elimu kwa wananchi wa Kata ya Ismani kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi (Climate Change Awareness). Mradi huu unafanywa kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine SUA).



3.5     KUJENGA UWEZO WA UTENDAJI NA RASILIMALIWATU


3.5.1        Watumishi na Ajira


Mamlaka ni taasisi ya Muungano yenye jumla ya Watumishi 593 walio katika vituo mbalimbali nchini ambapo 460 (77.6%) ni wanaume na 132 (22.4%) ni wanawake kama picha namba 27 inayoonesha. Watumishi 449 ni wenye fani ya hali ya hewa na 144 ni watumishi wenye fani za huduma saidizi (supporting services). Aidha, kutokana na kupanuka kwa huduma za hali ya hewa na hitaji la kuboresha huduma zitolewazo, Mamlaka inahitaji wafanyakazi wa kutosha wenye ujuzi wa fani ya hali ya hewa na wengine wa fani za huduma saidizi.



Picha Na 27: Mgawanyo wa wafanyakazi kijinsia

3.5.2        Mafunzo


Katika kuhakikisha kuwa Mamlaka inatoa huduma bora za hali ya hewa jitihada zifuatazo zilifanyika:-

Katika kipindi husika Mamlaka iliendelea kutekeleza mpango wake wa mafunzo ambapo wafanyakazi 56 wanaendelea na masomo yao katika ngazi mbalimbali ikijumuisha wafanyakazi 37 ambao wako katika ngazi ya shahada ya kwanza, 6 stashahada ya uzamili (Post Graduate Diploma), 1 shahada za uzamili (MSc) na 4 katika shahada ya uzamivu (PhD) .
  • Aidha jumla ya wafanyakazi 18 walihitimu masomo yao katika ngazi mbalimbali ikijumuisha wafanyakazi 11 katika shahada ya kwanza na 1 shahada ya uzamili (MSc) na 6 katika ngazi ya cheti .

  • Mamlaka pia imeendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika mafunzo ya muda mrefu ambapo Norway imefadhili wafanyakazi 2, WMO walifadhili wafanyakazi 6, Sweden 1 na Africa Kusini 1,

  • Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kuboresha na kuimarisha shughuli za Chuo cha Taifa cha hali ya hewa Kigoma kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo ambapo imekamilisha ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo la chuo pamoja na ukarabati wa Nyumba za kuishi wanafunzi kama picha namba 28 had 29 zinavyoonesha.


Picha Na 28: Kukamilika kwa ujenzi wa uzio wa NMTC


Picha Na 29: Kukamilika kwa ukarabati wa Nyumba za kulala wanafunzi NMTC

  • Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kimefanikiwa kupata usajili wa kudumu unaovuka mipaka (cross boarder registration) mwezi Machi, 2014 wenye namba REG/EOS/025. Usajili huu utawezesha Mamlaka kudahili wanafunzi kutoka katika nchi jirani kwa ajili ya masomo katika Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma.

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Dar es Salaam wamefanikiwa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza ya hali ya hewa nchini kuanzia Septemba, 2013. Aidha, watumishi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa wanashiriki kufundisha chuoni na pia Mamlaka inahusika katika kutoa mafunzo ya vitendo kuhusiana na fani ya hali ya hewa.

3.5.3        Taarifa ya hesabu zilizoishia Juni 2013/14


Taarifa ya hesabu za mwaka 2013/14 , Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali ameishakamilisha ukaguzi wake tayari kwa kutoa ripoti Mamlaka imeendelea kutumia mfumo wa IFRS katika uandaaji wa hesabu zake ambapo katika hesabu za mwaka wa fedha 2012/2013 zilizoishia Juni 2013, Mamlaka ilifanikiwa kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha, Mamlaka imekuwa ikipata hati safi tangu ilipoanzishwa mnamo mwaka 1999. .

3.5.4        Kupunguza madhara yatokanayo na UKIMWI na kuboresha huduma.


Mamlaka imeunda kamati inayoshughulikia masuala ya UKIMWI mahali pa kazi. Kamati hii kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi  (TACAIDS) imeendelea kuwaelimisha wafanyakazi juu ya janga la UKIMWI na kuwahamasisha kuhusiana na upimaji wa hiari wa maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kuwahudumia wafanyakazi wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa kuwapatia posho ya chakula.

3.5.5        MASUALA MTAMBUKA.


3.5.5.1  Kamati ya Maadili sehemu ya kazi


Mamlaka imefanikiwa kuanzisha kamati hii kwa msaada wa kiushauri kutoka Tume ya Maadili na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).  Kamati husika inaendela na kazi baada ya kupatiwa mafunzo ya kiutendaji.

3.5.5.2  Kamati ya Jinsia


Mamlaka imefanikiwa kuanzisha kamati ya Jinsia ambayo inashughulika na masuala ya jinsia. Mamlaka inazingatia uwiano wa kijinsia katika mafunzo na uongozi hususani katika ngazi za Wakurugenzi, Mameneja na Wakuu wa Vitengo. Pamoja na mafanikio hayo, Mamlaka inaendelea kuzingatia uwiano huo ili kufikia malengo iliyojiwekea. Hata hivyo changamoto kubwa ya kufikia uwiano wa jinsia katika Mamlaka ni uchache wa wasichana wanaochagua na kusoma masomo ya sayansi katika  ngazi ya kidato cha tano na sita.


SURA YA NNE

4.0     UTEKELEZAJI WA MRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA 2014/15

4.1     UTANGULIZI


Lengo la Mradi huu ni kuwa na Rada saba za hali ya hewa nchi nzima, kununua vifaa vya hali ya hewa na pia kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa ili kuboresha utabiri na utoaji wa tahadhari ya hali mbaya ya hewa.

4.1.1        Ujenzi wa Makao Mkuu na Kituo Kikuu cha Utabri nchini (NMC)


Mamlaka inamiliki kiwanja chenye Hati Na.80815 kilichoko mkabala na barabara ya Sam Nujoma ambapo inatarajiwa kujenga Kituo Kikuu cha Utabiri nchini. Mamlaka imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi huo (Feasibility Study) kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Utabiri nchini. Kazi ya Usanifu wa mradi huo imeanza kwa kupitia Mshauri Mwelekezi Ardhi University ambapo matokeo ya awali ya kazi hiyo (Sketch Designing) inatarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni.Uchambuzi wa kina (Detailed Design) utafanyika baada ya ule wa awali kukamilika.

4.1.2        Ununuzi na ufungaji wa Radar za hali ya hewa huko Kiseke, Mwanza


Mamlaka imefanikiwa kununua na kufunga rada ya pili ya hali ya hewa huko Kiseke, Mwanza Miundombinu ya Kituo cha Radar Kiseke imekamilika ikihusisha uzio, kibanda cha mlinzi pamoja na uwekaji wa umeme uliogharimu kiasi cha Tshs. Mkataba wa ununuzi huo ulihusisha pia mafunzo kwa mafundi na wataalamu wa hali ya hewa.

4.1.3        Uboreshaji na ununuzi wa mitambo na vifaa vya hali ya hewa


Mamlaka imekamilisha zoezi la kuboresha mfumo wa mawasiliano na uchambuzi wa data za hali ya hewa (upgrading of meteorological data synergy system). Aidha, Mtambo wa uchambuzi wa viashiria vya hali ya hewa na takwimu wa SYNERGIE umenunuliwa kwa ajili ya Kituo kikuu cha Utabiri na vituo vingine vinne  vya Zanzibar, JNIA, KIA na Mwanza.

Mamlaka pia imefanikiwa kununua mfumo wa Aeromet Web ambao utatumika katika kuboresha taarifa za hali ya hewa zitolewazo kwa ajili ya Usafiri wa Anga. Aidha, Mamlaka imenunua mitambo miwili ya kisasa ya TRNSMET kwa ajili ya kukusanya na kubadilishana data na taarifa za hali ya hewa. Mamlaka pia imenunua vifaa mbalimbali vya hali ya hewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya upimaji na utabiri wa hali ya hewa.

4.1.4        Uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha hali ya hewa Kigoma


Mamlaka ya Hali ya Hewa imeeendelea kuboresha na kuimarisha shughuli za Chuo cha Taifa cha hali ya hewa Kigoma kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo ambapo imekamilisha ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo la chuo pamoja na ukarabati wa Nyumba 4 za kuishi wanafunzi. Aidha, Mamlaka inaendelea na mchakato wa ujenzi wa Hosteli za wanafunzi ambapo iko katika hatua ya awali ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo.




















SURA YA TANO


5.0     CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI


5.1     Changamoto za Jumla


Pamoja na mafanikio ambayo Mamlaka ya Hali ya Hewa imepata bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo:

·         Kukosekana kwa jengo la kudumu la Makao Makuu ya Mamlaka na Kituo Kikuu cha Utabiri na hivyo kuathiri taratibu za kuweka mitambo ya kisasa ya utabiri kutokana na makubaliano ya kimataifa yanayotaka baadhi ya mitambo ikishafungwa isihamishwe. Aidha, jengo la kupanga linaigharimu Mamlaka fedha nyingi za Pango ambayo ni karibu 133 milioni kwa miezi mitatu.
·         Ufinyu wa Bajeti
·         Mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mifumo ya hali ya hewa kubadilika badilika na kusababisha kubadilika kwa misimu ya hali ya hewa na ongezeko la majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.

5.2     Changamoto za utekelezaji wa mradi wa rada


·         Wananchi wa Mwanza eneo ilipofungwa rada ya hali ya hewa wamekuwa na wasiwasi na rada za hali ya hewa kuhusu mionzi ya mitambo yake. Hata hivyo Mamlaka imetoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo Wizara ya Uchukuzi ikionesha kutokuwepo kwa mionzi inayoweza kusababisha madhara kwa wananchi. Sehemu ya maelezo hayo ya kitaalamu ni pamoja na

i.              Mawimbi ya Rada yanapungua nguvu kwa kufuata umbali kutoka eneo ilipo rada.
ii.            Eneo la zaidi ya mita 600 kutoka ulipo mtambo wa rada ni eneo lisilofikiwa na mionzi yenye ukali wa athari yoyote kwa wanadamu na viumbe wengine na hivyo ni salama.
iii.          Chini ya mita 600 kutoka ilipo rada eneo lenye athari ni lile ambalo liko katika urefu sawa na urefu wa antenna ya rada.
iv.          Kwa mji wa Mwanza ulivyo kwa sasa hakuna jengo lolote refu ambalo limefikia usawa wa urefu ilipo rada (mita 1285 kutoka usawa wa bahari) na ambalo liko ndani ya mita 600.
v.            Kwa wajenzi wa minara mirefu ya Mawasiliano ndani ya eneo la mita 600 kutoka ilipo rada ni vyema wakawasiliana na Mamlaka ili kuhakikisha ujenzi huo unafanyika katika  mazingira salama (kuzimwa rada watakapokuwa juu ya minara hiyo).

·          

5.3     Mikakati ya kuboresha huduma za hali ya  hewa ;-


·            Serikali inaandaa Sera ya Taifa ya Hali ya Hewa ambayo itafuatiwa na mapitio ya Sheria ya Hali ya Hewa kwa ajili ya kuboresha utoaji na usimamizi wa huduma za hali ya hewa nchini .
·            Kuongeza Bajeti ya Mamlaka kwa ajili ya kununua mitambo na vifaa na pia kuongeza mtandao wa vituo.
·            Kuandaa miradi mbalimbali yenye lengo la kupata rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.
·            Kuendeleza mpango wa kufundisha wataalamu wapya na kuwapatia Mafunzo wafanyakazi waliopo kwa kuongeza bajeti ya Mamlaka.
·            Kuongeza vyanzo vingine vya Mapato kwa ajili ya kuboresha huduma za hali ya hewa.


No comments: