Monday, March 9, 2015

KAULI YA WAPIGWE TU YAZIDI KULITESA TAIFA,ASKARI WAWASHUSHIA KIPIGO WAANGALIZI KUTOKA TACCEO,WATANGAZA KUSIMAMISHA KWANZA ZOEZI KWA MUDA


Mwenyekiti wa mtandao wa asasi za kiraia za kuangalia chaguzi nchini tanzania MARTINA KABISAMA akizungumza na wanahabari muda mfupo uliopita
 Jeshi la polisi nchini Tanzania kwa mara nyingine limeingia katika lawama kubwa baada ya askari wake kuwashushia kipigo waangalizi wanaofwatilia zoezi la uandikishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR waangalizi ambao wanatoka mtandao wa asasi za kiraia wa kuangalia chaguzi Tanzania TACCEO.

Akizungumza na wanahabari asubuhi ya leo tarehe 9 mwenyekiti wa mtandao huo ambao unaratibiwa na kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC  ms MARTINA KABISAMA amesema kuwa tarehe saba mwezi wa tatu mwaka huu majira ya saa tano kasoro robo usiku waangalizi wawili kutoka katika mtandao huo wakiwa wanaandaa taarifa yao ya uangalizi wa siku wakiwa chumbani kwao (chumba namba 5)kwenye  nyumba ya wageni iitwayo NETO GUEST HOUSE walivamiwa na askari polisi wapatao wanne,ambao waliwashambulia na kuwapiga na kuwaumiza vibaya.

Amesema kuwa kabla ya uvamizi huo askari hao ambao kwa ujumla wao walikuwa sita (6) waliwaweka kwanza chini ya ulinzi mhudumu na mlinzi wa nyumba hiyo ya wageni ambapo mlinzi alifungiwa chooni na kisha askari wawili walibaki kuwalinda mhudumu na mlinzi ili wasitoke na ndipo askari wengine wanne waliingia ndani na kuanza kuwashambulia waangalizi hao.

Amewataja waangalizi hao kuwa ni HAMFREY JOSIAH na WILISON RAFAEL ambapo amesema  askari hao waliokuwa na silaha aina ya SMG waliwavamia vijana hao na kuanza kuwashambulia na kuwapiga mateke na marungu kwa madai kuwa waangalizi hao walikuwa wameiba kompyuta mpakato yani laptop,ambapo askari hao waliendelea kuwapiga huku wakiwataka wawaonyeshe walipoficha vifaa hivyo walivyodai viliibiwa mufindi.

Aidha amesema kuwa askari hao wakati wakitekeleza kitendo hicho ambacho amekiita cha kikatili walikuwa wamevalia kiraia na hawakujitambulisha kama taratibu zinavyoelekeza huku muda wote wakiwa wanawatishia kuwaua kama wangeleta ubishi.

Amesema kuwa baada ya kipigo kikali kutoka kwa askari hao waliwafunga pingu vijana hao na kuwapekua kama walikuwa wameiba mali zao na baada ya kukuta hawana mali yao na wakagundua kuwa ni waangalizi na sio wahalifu askari hao waliomba radhi na kutoweka eneo la tukio huku wakiiwaacha wangalizi hao katika majeraha na maumivu makali.

Baada ya tukio hilo waangalizi wa uandikishwaji huo waliopo makambako na njombe walikusanyika na kuanza kuwasaidia wenzao ambao mmoja wao ambaye ni Wilson aliyekuwa ameumia vibaya kutokana na kipigo hicho.

Katika hatua nyingine baada ya tukio hilo kamati ongozi ya TACCEO imetangaza kusimamisha mara moja zoezi la uangalizi uliokuwa unaendelea makambako na kuwataka waangalizi wote kurejea jijini Dar es salaam haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha yao.

  Bi KABISAMA amesema kuwa kufwatia tamko hilo wanasitisha zoezi la uangalizi kwa muda mfupi hadi watakapokuwa wamechukua hatua na taratibu za kisheria na kiutawala ili kuwa na uhakika wa usalama kwa waangalizi wao wamapokuwa katika maeneo ya kazi.

Aidha maazimio mengine ambao TACCEO wamefikia ni pamoja na kulitaka jeshi la polisi kuwataja hadharani askari wake sita (6) ambao walishiriki katika tukio hilo la kiinyama,ikiwa na pamoja na sheria ionekane ikifanya kazi juu ya askari hao kwani ni kinyume na maadili ya kazi yao.

Pamoja na hayo TACCEO wameitaka serikali hususani jeshi la polisi kuwahakikishia wadau wote wa uchaguzi ndani na nje ya nchi usalama wao kipindi chote cha uandikishwaji wapiga kura,kura ya maoni pamoja na uchaguzi mkuu.
Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC ambao ndio waratibu wakuu wa mtandao huo  Bi HELLEN KIJO BISIMBA
Akizungumzia tukio hilo mbele ya wanahabari  mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC ambao ndio waratibu wakuu wa mtandao huo  bi HELLEN KIJO BISIMBA amesema kuwa kupigwa kwa waangalizi hao na askari  ni mwendelezo wa kutekeleza amri aliyowahi kuitoa waziri mkuu bungeni kuwa watakao kaidi amri wapigwe tu na hakuna namna nyingine kwani serikali imechoka na kilichobaki ni kuwapiga tu.KAMA ILIVYO KWENYE VIDEO HAPO CHINI
“ hivi vipigo mimi sishangai alishasema waziri mkuu kuwa watu wapigwe tu na ushahidi ndio huu kuwa watu wanapigwa bila makosa,saa tumechoka na hivi vipigo visivyo na sababu na tunataka sheria ichukue kondo wake”alisema BI HELLEN.
Aidha mtandao wa asasi za kiraia za kuangalia uchaguzi nchini Tanzania TACCEO umedhamiria kuitisha mkutano mkubwa wa wadau wa chaguzi ndani na nje ya nchi ili kujadili tishio la usalama wanapokuwa katika uangalizi wa chaguzi mbalimbali nchini.

No comments: