Friday, March 20, 2015

SIO SIRI TENA ZITTO KABWE RASMI ACT TANZANIA



Pamoja na mpango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana, Chama cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa huyo kuanzia leo.


Mbunge huyo alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.


Tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka mmoja uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha, hivyo kitendo chake cha kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa mashabiki wake waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.

Akizungumza na baadhi ya wanahabari jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila kuuma maneno alisema: “Hahahaa… tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi yamekamilika.”

Alipotakiwa kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi, yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku akitajwa kuwa ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati zake za siasa.


Hivi karibuni, chama hicho kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu kutokana na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.

Tayari washirika wa Zitto waliohusishwa naye kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na baadaye kufukuzwa uanachama, Mwigamba na Prof. Kitila Mkumbo wametua ndani ya chama hicho kipya.


Chama hicho ambacho kinaendelea na uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita unaofanya uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.

Akizungumzia uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”

No comments: