Na Athumani Shomari- Bagamoyo
Mapato ya halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo yameongezeka kutoka bilioni 1.2 hadi kufikia bilioni 6.6 ikiwa ni mapato ya ndani huku ruzuku kutoka serikali kuu imeongezeka kutoka bilioni 4 hadi kufikia bilioni 18 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2010 mpaka 2015
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo Shukuru Mbato wakati wa akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika mkutano wa kuvunja baraza la madiwani wa wilaya ya Bagamoyo.
Amesema kiwango hicho kimeongezeka chini ya utawala wa madiwani hao wanaomaliza muda na kuwataka wananchi waelewe kuwa viongozi wao wameweza kusimamia miradi ya halmashauri kwa kiwango kinachohitajika.
Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio hayo yaliyopatikana kwa kuongezeka mapato ya halmashauri kuna changamoto kadhhaa ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo ikiwemo serikali kuu kuingilia mapato ya ndani na kupungua kwa makusanyo kunakotokana na hali ya hewa.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali shukuru Mbato amesema miradi mingi imefikia kiwango kizuri cha utekelezaji na kwamba miradi michache ambayo haijakamilika ipo katika mchakato wa kukamilishwa.
Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo limevunjwa rasmi na kusubiri uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment