Monday, August 10, 2015

Habari za michezo leo Tanzania


TWIGA STARS YAENDELEA KUJIFUA ZANZIBAR

Kikosi cha timu ya Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kinaendelea na mazoezi katika uwanja wa Amani na uwanja wa Mafunzo vilivyopo kisiwani Zanzibar.

Twiga Stars iko kambini kisiwani Zanzibar kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofanyika nchini Congo- Brazzavile kuanzia Septemba 04 – 19 mwaka huu.

Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ameendelea kukinoa kikosi chake cha wachezaji 25 waliopo kambini kisiwani Zanzibar kujiandaa na michuano hiyo ya Afrika.

Twiga Stars itakua kambini kisiwani Zanzibar kwa kipindi cha mwezi mmoja, kujiandaa na fainali hizo za michezo ya afrika, ambapo imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Congo – Brazzavile, Ivory Coast na Nigeria.



KIHANGA MWENYEKITI FA MOROGORO
Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Morogoro (MRFA) jana kilifanya uchaguzi wa viongozi wake katika nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu, mweka hazina, mjumbe wa mkutano mkuu pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Katika uchaguzi huo Paschal Kihanga aliibuka na ushindi katika nafasi ya mwenyekiti, huku Gracian Max Makota  akishinda nafasi ya makamu mwneyekiti, nafasi ya katibu mkuu imechukuliwa na Charles Mwakambaya na katibu msaidizi Jimmy Lengme.

Nafasi ya Mweka Hazina imechukuliwa na Peter Mshigati, Mjumbe wa mkutano mkuu ni Hassan Mamba na mwakilishi wa vilabu ni Ramadhani Wagala, Kamati ya utendaji wamechaguliwa Mrisho Javu, Rajabu Kiwanga na Boniface Kiwale.

TFF inawapongeza viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kazi za kila siku za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

TFF YATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI MALAWI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za rambi rambi kwa Rais wa Chama cha Soka nchini Malawi (FAM), Walter Nyamilandu kufutia kifo cha aliyekua Rais wa chama hicho John Zingale.

John Zangale alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi wiki iliyopita katika hospitali ya  Mlambe iliyopo Blantyre nchini Malawi na kuzikwa mwishoni mwa wiki alikuwa Rais wa FAM mwaka 1998- 2002.

Katika salam zake kwenda kwa Rais wa FAM, Malinzi amewapa pole familia ya marehemu pamoja na chama cha soka nchini Malawi kwa msiba huo, na kusema TFF kwa niaba ya Watanzania iko pamoja nao katika kipindi hicho cha maombelzo.


WATANZANIA SABA WAULA KAMATI ZA CAF
Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF ) kilichokutana mwishoni mwa wiki jijini Cairo nchini Misri, kimewateua watanzania saba kuwa wajumbe wa kamati zake mbali mbali kwa kwa kipindi cha miaka miwili 2015-2017.

Walioteuliwa pamoja na kamati zao katika mabano ni:

1. Leodeger Tenga- (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Fedha, Mjumbe wa Kamati ya Uendeshaji Mashindano ya fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa ndani (CHAN), Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Wanawake, na Mjumbe wa Kamati ya Ushauri na Vyama Wanachama).

2. Jamal Malinzi - (Mjumbe kamati ya Uendeshaji Mashindano ya Vijana Umri chini ya miaka 20)

3. Mwesigwa Selestine - (Mjumbe Kamati ya Uendeshaji Mashindano ya Vijana Umri chini ya Miaka 17).

4. Richard Sinamtwa -(Mjumbe Kamati ya Rufaa)

5.Dr Paul Marealle -(Mjumbe Kamati ya Tiba)

6. Lina Kessy -(Mjumbe ya Soka la Wanawake)

7. Crescentius Magori-(Mjumbe Kamati ya Soka la Ufukweni na Soka la Ndani)

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania - TFF linawapongeza wajumbe wote walioteuliwa kuingia katika kamati mbali mbali na linawatakia kila la kheri wanapoiwakilisha nchi yetu.
TFF.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: