Saturday, August 8, 2015

Kauli ya JULIUS MTATIRO baada ya jimbo la segerea kupangiwa CHADEMA.

HONGERENI TENA SEGEREA: NINA FURAHA TELE NA SIJATETEREKA!

Ndugu zangu, nimejulishwa na mtu muhimu sana kwamba jimbo la Segerea limeachwa chini ya CHADEMA lakini ndani ya UKAWA, nimeshazithibitisha taarifa hizi kwa viongozi wangu.
Kwanza niwapongeze viongozi wote wa UKAWA kwa kufikia makubaliano hayo muhimu, mimi ni muasisi wa UKAWA na nimekuwa Katibu wa UKAWA katika Bunge Maalum la Katiba, naipenda UKAWA na naamini katika UKAWA; Kama viongozi wameweza kukubaliana jambo hili mimi bila KINYONGO chochote kile naunga mkono mapendekezo na maamuzi yao.

Pili nawataka wananchi wa Segerea, wanachama wa CHADEMA, CUF, NCCR na NLD na vyama vingine vyote waende kwenye vituo vya kupigia kura tarehe 25 Oktoba na kuchagua Diwani, Mbunge na Rais aliyesimamishwa na chama chochote cha UKAWA bila kujali mambo mengine, huu ni mwaka wa mabadiliko na lazima tuyasimamie.
Tusikubali kupumbazwa na janja za CCM kuwa angekuja Mtatiro huku Segerea tungewaunga mkono! CCM ni ileile na mtu yeyote anayegombea kupitia CCM anakwenda kuimarisha mfumo uleule uliochoka, unaonuka na kukumbatia rushwa na ufisadi, wagombea wa CCM ni walewale wanaotetea mfumo uleule ambao umelifikisha taifa letu hapa tulipo. CHAGUA vyama vya UKAWA hapa Segerea na nchi nzima bila kujali kuwa MTATIRO siyo mgombea tena.
Kwa sababu siasa siyo ajira mimi ntajikita katika masuala mengine ya ujenzi wa taifa langu ikiwemo kuelimisha wananchi katika uchaguzi na kusimamia kampuni yangu na kisha ntajipanga kuingia bungeni mwaka 2020. Nataka kuwaonya wale wenzangu na mimi ambao wako katika siasa kwa ajili ya KUTAFUTA MKATE WA KILA SIKU watambue kwamba SIYO MAHALI PAKE na kwamba wataumbuka! Ukifanya siasa usiitegemee kama sehemu ya kipato chako hata siku moja ili usijekuathirika sana kila unapokosa fursa kama nilivyokosa mimi pale Segerea.
Natoa wosia na wito kwa wagombea wote wa vyama vya UKAWA nchi nzima ambao hawatapitishwa kuwa wagombea kwenye uchaguzi huu washirikiane na wagombea waliopo ili tutafute ushindi, huu ni mwaka wa mabadiliko na mwaka wa maamuzi, shiriki kuleta mabadiliko hayo.
Na wale watakaotimkia ACT, ADC, CCM na kwingineko kwa sababu hawakupata majimbo ndani ya UKAWA nawatakia kila la heri na kuwakumbusha kuwa KIMBUNGA CHA UKAWA kitawasambaratisha kokote kule waliko bila kujali walipewa nyadhifa gani.
Nawaahidi kuendelea kusimamia ukweli na kulipigania taifa langu hadi mwisho wa dahari,
Julius Mtatiro – B.A, M.A, LLB, 
Mtia nia atakayewaunga mkono wagombea wa UKAWA jimbo la Segerea na nchi nzima,


No comments: