Sunday, September 13, 2015

OLE GABRIEL AZINDUA FAINALI ZA AIRTEL RISING STAR


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Elisante Ole Gabriel leo Jumapili, Septemba 13, amezindua rasmi michuano ya Airtel Rising Stars kitaifa kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Ole Gabreil ameipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel nchini kwa kuendesha michuano hiyo, ambayo inawapa nafasi vijana wa kike na kiume kuonyesha vipaji vyao vya kucheza mpira wa miguu.
Ole Gabriel ameiomba Airtel kuendelea kudhamini michuano hiyo na kutanua wigo zaidi kwa mikoa mingi kuweza kushiriki kwenye mashindano hayo.
Aidha Ole Gabriel ameiitaka TFF kuwasiliana na Wizara yake pindi wanapoagiza vifaa vya michezo nje ya nchi mapema, ili ofisi yake iweze kulisadia Shirikisho katika suala la ushuru wa vifaa vya michezo vinapoingia nchini.
Naibu katibu mkuu huyo aliyasema hayo wakati akijibu ombi la Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia aliyeiomba Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuisaidia TFF kupata msamaha wa kodi pindi inapoingiza vifaa vya michezo nchini kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu.
Jumla ya timu saba za vijana wa kike na kiume zinashiriki fainali hizo za Taifa za Airtel Rising Stars zinazodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, ambapo vijana wenye vipaji huchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na vituo vya michezo (Academy) za Dakara – Senegal na Doha – Qutar zinazomilikiwa na kampuni hiyo.
Mikoa inayoshiriki fainali hizo ni Arusha, Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Mbeya.


No comments: