Kiongozi Mkuu wa kiroho
wa waislam wa dhehebu la Shia ITHNASHERIYA Tanzania Sheikh HEMED JALALA
ameibebesha mzigo wa lawama serikali ya Saudi Arabia kufwatia vifo vya watu
zaidi ya elfu nne vilivyotokea siku chache zilizopita wakati wa Ibada ya hija iliyofanyika
nchini humo huku akisema kuwa vifo hivyo ni uzembe wa wazi wa waandaaji wa
ibada hiyo.
Lawama hizo amezitoa
leo Jijini Dar es salaam mara baada ya kuwasili nchini Tanzania pamoja na
waumini wengine wa dhehebu hilo wakitokea katika ibada hiyo ambapo amesema kuwa
ni wazi mauaji yaliyotokea katika ibada hiyo ni ya kusikitisha sana na
yalitokana na uzembe wa waandaaji wa ibada hiyo kutokana na kasoro nyingi
zilizoonekana.
Amesema kuwa moja ya
sababu kubwa iliyosababisha mauaji ya waumini wengi ni kufungwa kwa njia kubwa
za kutoka na kuingilia wakati wa urushwaji wa mawe kumpiga shetani jambo ambalo
lilisababisha msongamano mkubwa wa watu na kusababisha vifo vingi.
Aidha Sheikh JALALA
ameongeza kuwa katika maeneo yote ya ibada hiyo kulikuwa kumezungukwa na kamera
eneo lote lakini watu walikuwa wakifariki kwa mfululizo kwa kila baada ya
dakika tatu lakini wahusika hawakuona na hakuna msaada wowote ambao ulikuwa
unatolewa na wahusika licha ya kuwepo kwa kamera kila kona.
Baada ya tukio hilo Sheik
jalala amesema kuwa kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa ni lazima serikali ya
Tanzania iungane na nchi ambazo zina idadi kubwa ya mahujaji ambao wanaenda
katika ibada hiyo waweze kushirikishwa katika mipango ya ibada hiyo ili kuweka
mipango ambayo itawafanya waumini kuwa salama wakati wa ibada hiyo kwa kuwa
hakuna mtu anayekwenda katika ibada hiyo kwa ajili ya kufa.
No comments:
Post a Comment