Friday, October 30, 2015

CUF wapigilia Msumari mwingine sakata la zanzibar na ZEC

Pichani ni Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi  wa Chama cha wananchi CUF,Twaha Taslima akizungumza
na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam
kupinga uamuzi wa ZEC
CHAMA cha wananchi CUF kimesema hakipo tayari kuingia tena kwenye uchaguzi  mkuu visiwani Zanzibar .

       Kauli hii ya CUF inakuja baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC) Bwana  Jecha Salim Jesha kufuta uchaguzi wote na kutangaza kufanyika tena ndani ya siku 90.
 
     Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa kamati ya Uongozi ya CUF,Twaha Issa Taslima amesema Chama chake hakioni sababu ya kuingia kwenye uchaguzi kutokana na mwenyekiti wa ZEC kutokuwa na mamlaka ya kikatiba  na sheria ya kufuta uchaguzi.

   Amesema jambo linaloshangaza ni kuona mwenyekiti wa ZEC kutangaza kufuta uchaguzi bila ya kuwashirikisha makamishna wake,

     “Hili linathibitishwa na taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa na makamishna wa zec kukanusha kuhusika na uamuzi huo wa mwenyekiti wa zec,ambapo hatua hii ni uvunjwaji wa katiba ya Zanzibar (1984) ibara ya 119(10)  inayotaka vikao vya ZEC kuhudhuriwa na mweyekiti na makamu mwenyekiti na wajumbe wanne na uaamuzi kuungwa mkono na walio wengi”amesema Taslima.

      Taslima amesema CUF wamepitia katiba zote  mbili,katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania,(1977),katiba ya Zanzibar ya (1984) sheria ya uchaguzi sura 343 (2010),sheria ya uchaguzi ya Zanzibar Na.11/1984 na kanuni za uchaguzi wa Rais na Wabunge za  2025 na kujiridisha kuwa hakuna kifungu chochote kinachozipa Mamlaka ZEC ya kufuta uchaguzi uliokwisha Fanyika.

    “Kwa Mantiki hiyo uamuzi uliochukuliwa na mwenyeikiti wa ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake yote ni batili na hauwezi kukubalika”amesema

     Hata hivyo amesema kitendo cha mwenyekiti wa ZEC kutangaza kurejea kwa uchaguzi mkuu siku (90) tangu tarehe 28/10/2015 alipofuta huu uliomalizika ni kuvunja katiba kwani katiba ya Zanzibar ibara ya 90 inatamka bayana kuwa mara baada ya kuvunjwa kwa baraza la wakilishi uchaguzi mkuu utaitishwa ili kuliwezesha baraza jipya ndani ya siku 90.

      “Baraza la wawakilishi lilivunjwa rasmi tarehe 13/8/2015 na hivyo baraza jipya linapashwa kukutana si zaidi ya tarehe 13/11/2015.kwa Tangazo la mwenyekiti wa ZEC,la kurejewa uchaguzi wa siku 90 baadaye,katiba ya Zanzibar itakuwa imevunjwa jambo ambalo haliwezi kukubalika.

KUHUSU MADAI YA KASORO  ZILIZOKUWEPO.
  
Kuhusu madai ya kuwepo kasoro kwenye uchaguzi huo zilizotolewa na mwenyekiti wa ZEC,Cuf wamesema kasoro hizo haziwezi kupeleka uchaguzi kufutwa kwani kasoro za uchaguzi au malalamiko yoyote ya uchaguzi lazima yawasilishwe kwa fomu maalum zinazohusika na kuambatanishwa na matokeo na sio kufuta uchaguzi.
Vilevile Chama cha CUF kimewataka waananchi kuwa watulivu katika kipindi hichi ambapo juhudi kubwa inafanyika.

No comments: