Msajili wa vyama vya siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi, akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni Zanzibar. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika picha ya pamoja na Msajili wa vyama vya siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi (wa pili kushoto) na baadhi ya wajumbe wa Ofisi hiyo. Kushoto ni msajili wa vyama Zanzibar Bw. Rajab Baraka. (Picha na Salmin Said, OMKR) Msajili wa vyama vya siasa Tanzania Jaji Francis Mutungi, amesema kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama vya siasa Zanzibar kukutana, ili kutatua mzozo wa kisiasa uliojitokeza. Amesema Zanzibar ni nchi amani, hivyo hakuna haja ya kuruhusu migogoro ya aina hiyo ambayo inaweza kupelekea kuvurugika kwa amani na kuipotezea sifa Zanzibar katika jamii ya Kimataifa. Jaji Mutungi akiambatana na baadhi ya wajumbe wa ofisi hiyo ya msajili pamoja na msajili wa vyama kwa upande wa Zanzibar Bw. Rajab Baraka, ametoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Amesema kuna kila sababu ya kulinusuru taifa kuingia katika migogoro isiyokuwa ya lazima, na kutaka juhudi za makusudi zichukuliwe ili kumaliza tatizo hilo. Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF, amesema amekuwa akichukua juhudi binafsi kukutana na wagombea wenzake kuzungumzia tatizo hilo, lakini baadhi yao wanaonekana kutokuwa tayari kulizungumza. Amesema hapendi kuona Zanzibar inaingia katika machafuko yanayoweza kuepukwa, na kwamba viongozi wengine pia wanapaswa kufikiria amani na maslahi ya Zanzibar kuliko maslahi binafsi. Katika hatua nyengine Maalim Seif amemshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha kwa kuiingiza nchi katika migogoro ya kisiasa na kikatiba. Akinukuu vipengele vya Katiba ya Zanzibar, Maalim Seif amesema kipindi cha Urais wa Zanzibar ni miaka mitano kuanzia tarehe ya kuapishwa, hivyo kuanzia tarehe 02/11/2015 kipindi cha Urais wa Zanzibar awamu ya saba kitakuwa kimemalizika. Hivyo amesema bila ya kuchukuliwa juhudi za dharura, kuanzia tarehe 02 mwezi ujao kwa mujibu wa katiba, Zanzibar itakuwa haina Rais, Serikali wala Baraza la Wawakilishi. |
No comments:
Post a Comment