Mwenyekiti wa mtandao wa asasi zaidi ya 17 zinazoangalia chaguzi TACCEO Bi MARTINA KABISAMA akizungumza na wanahabari mapema leo Jijini Dar es salaam |
Mtandao wa asasi za Kiraia
wa kuangalia chaguzi nchini Tanzania TACCEO ambao unaratibiwa na kituo cha
sheria na haki za binadamu LHRC ambao ni waangalizi wa ndani wa uchaguzi unaoendelea nchini wamewataka wasimamizi wa
uchaguzi ambao bado hawajatangaza matokeo ya wabunge katika majimbo mbalimbali
kufanya hivyo mara moja kwa kuwa ucheleweshaji wa matokeo hayo unaweza
kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani katika maeneo hayo.
Rai hiyo imetolewa leo
Jijini Dar es salaam kupitia kwa mwenyekiti wa mtandao huo wa TACCEO Bi MARTINA
KABISAMA wakati wakitoa tathmini ya uchaguzi huo hadi sasa ambapo amesema kuwa
ucheleweshwaji wa kutangazwa kwa matokeo ya ubunge katika maeneo mbalimbali
umekuwa ni changamoto kubwa ambayo imekuwa ikisababisha kutumika kwa nguvu ya
polisi pamoja na vurugu kubwa kutokana na wananchi kukosa uvumilivu wa matokeo
hayo.
Amesema kuwa kwa mujibu
wa sheria ya uchaguzi sura namba 343 ya sheria za Tanzania katika kifungu cha
8(a) inatamka kuwa msimamizi wa uchaguzi analazimika kutangaza matokeo ya
uchaguzi mara moja pasipo kuchelewa baada ya kukamilisha kujumlisha kura
hizo,huku akisema taarifa walizonazo kutoka kwa waaangalizi wao zinaonyesha kuwa
kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo ni katika majimbo zaidi ya 21.
Kaimu Mkuruhenzi wa kituo cha sheria na haki za Binadamu LHRC Bi IMELDA LULU URIO akizungumza wakati wa kutoa report ya maendeleo ya uchaguzi wa mwaka huu nchini kwa mujibu wa waangalizi wao mbalimbali nchi nzima |
Ametolea mfano baadhi
ya majimbo ambayo tatizo hilo lilijitokeza na kusababisha taharuki kubwa kuwa
ni Temeke,Ilala,Simanjiro,na Zanzibar ambapo kumekuwa na sababu mbalimbali
zinazochangia ikiwemo wagombea kudai kurudiwa kuhesabu kura,wagombea kukataa
kusaini,kupotea kwa baadhi ya nyaraka husika,kupotea kwa baadhi ya masanduku ya
kura,kuchelewa kupokea vifaa kutokana na changamoto za kijografia,ambapo hali
ya kuchelewa huko kumesababisha wananchi kukosa uvumilivu na kuhisi kuwa kuna
mbinu chafu zinazofanywa na kuamua kufanya fujo ikiwemo kuchoma baadhi ya ofisi
za serikali.
Aidha katika hatua
nyingine mtandao huo umebaini kuwepo kwa matumizi makubwa ya nguvu za dola
kutoka kwa polisi kwa wananchi wasio na hatia wanaofurahia matokeo yao ya
ushindi,huku wakisema matumizi hayo ya nguvu yanawafanya hata raia wema kuzoea
vurugu na fujo na kuona kama mchakato wa democrasia ni mchakato wa fujo na
vurugu,ambapo amelitaka jeshi la polisi kuhakikisha linatenda haki kipindi
hiki.
No comments:
Post a Comment