Thursday, October 1, 2015

U15 YAICHAPA KOMBAINI TANGA 4-0


Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 (U-15) leo imeendeleza wimbi la ushindi katika mechi zake za kujipima nguvu, baada ya kuichapa mabao 4-0 kombaini ya U-15 ya Tanga Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ushindi huo umetokana na mabao mawili ya Issa Abdi dakika ya 21 na 23, Frank George dakika ya tisa na Ibrahim Abdallah Ali dakika ya 80.
Pamoja na ushindi huo, lakini vijana wa U-15 ya Taifa walikutana na ushindani kutoka kwa wachezaji wenye vipaji wa U-15 ya Tanga.
Kivutio zaidi alikuwa ni kiungo Joseph Yakobo ambaye Tanga wanamuita ‘Sure Boy’ na mshambuliaji George Chande aliyeisumbua mno ngome ya timu ya taifa iliyoongozwa na Nahodha, Maulid Lembe.
Wachezaji wote waliokwenda majaribio Orlando Pirates ya Afrika Kusini mwezi uliopita, Asad Ali Juma, Issa Abdi Makamba, Kevin Deogratius Kahego, Amani Amede Maziku na Athumani Maulid Rajab walicheza leo.  
Huo unakuwa mchezo wa tano kushinda, kati ya mechi saba tangu kuundwa kwa timu hiyo Aprili mwaka huu, ikifunga jumla ya mabao 15 na kufungwa mawili tu.
Timu hiyo iliifunga 4-1 na 3-0 Mbeya, ikaifunga 4-0 na 1-0 Zanzibar na kutoa sare ya 0-0 na 1-1 na Morogoro kabla ya ushindi wa leo.
U15 inayoandaliwa kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za vijana Afrika mwaka 2017 nchini Madagascar zitakazoanza Juni mwakani, imekuwa ikiweka kambi kila mwishoni mwa mwezi kwa ajili ya michezo ya kujipima nguvu chini ya kocha Sebastian Nkoma.
Kesho U15 Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wake wa mwisho mjini hapa, itakapomenyana na U-17 ya mkoa Tanga hapa hapa Mkwakwani.
Wachezaji wa kikosi cha U15 ya Taifa wote ni wanafunzi wa sekondari mbalimbali nchini na ndiyo maana hukutanishwa mwishoni mwa mwezi tu kwa mazoezi ya pamoja.

No comments: