Saturday, November 28, 2015

NI HUZUNI--SAFARI YA MWISHO YA KAMANDA ALPHONCE MAWAZO


Mwili wa marehemu Alphonce Mawazo ikiwasili nyumbani kwa baba mdogo (Charles Lugiko) Nyegezi jijini Mwanza ukitokea Hospital ya Bungando kwaajili ya ibada fupi.


Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo ukitolewa Hospital ya Bugando kuelekea nyumbani kwa Baba Mdogo ( Charles Lugiko) huko Nyegezi na kurudi katika viwanja vya Furahisha ili kupata heshima za mwisho kitaifa.





Familia ya Marehemu Alphonce Mawazo wakiendeshwa na mchungaji kwa ibaa fupi iliyofanyika nyumbani kwa baba Mdogo wa Marehemu.



Wananchi wanazidi kufurika uwanja Wa furahisha kwa kuaga mwili WaAlphonce Mawazo
Aliyekuwa Mgombea Urais wa CHADEMA na kupeperusha bendera ya UKAWA, Mhe. Edward Lowassa akitoa salamu zake za mwisho kwa aliyekuwa M/kiti CHADEMA moa wa Geita Alphonce Mawazo aliyeuwawa kikatili kwa kukatwakatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM huko Busanda Mkoani Geita.
Tendo hili lilifanyika muda mfupi uliopita katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza baada ya mapema leo asubuhi mwili kutoka Bugando hospital na kuelekea nyumbani kwa baba yake mdogo ( Mchungaji Charles Lugiko) Nyegezi jijini Mwanza na kupelekwa katika viwanja vya Furahisha ambapo ibada nzima na salamu za mwisho kitaifa zilifanyika mahali hapo

Mwenyekiti CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akitoa salamu za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita kamanda Alphonce Mawazo ambaye ameagwa kitaifa katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza 
Mawazo aliuwawa tarehe 14/11/2015 kikatili kwa kukatwakatwa mapanga na wafuasi wa CCM huko Busanda Mkoani Geita akitekeleza majukumu yake ya Chama.


ALIYEKUWA mgombea Urais wa Chadema, Edward lowassa, amelitaka jeshi la Polisi nchini kuwachukulia hatua wale wote wanadaiwa kumuua, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo na kwamba kama hawatafanya hivyo, watachukua hatua wao wenyewe. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku mbili sasa tangu Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kutoa hukumu kwa chama hicho kikuu cha upinzani kumuaga na kumzika Marehemu Mawazo bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Marehemu Mawazo, alifariki Novemba 14 mwaka katika kijiji na kata ya Katoro, wilaya na Mkoa wa Geita na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.

Lowassa ametoa kauli hiyo leo wakati akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kuaga mwili wa Mawazo kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa Chadema na kuungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) amesema polisi wasipochukua hatua kwa waliomuua marehemu Mawazo watajichukulia hatua wao.
Amesema kuwa watu waliomuua Mawazo wanafahamika majina yao lakini Polisi kwa kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kuwachukulia hatua zozote zile mpaka sasa.
“Hawa Polisi wanafanya mambo yao kiimra-imra, kiujanja ujanja, wao wameleta magari ya washawasha yaliyonunuliwa kwa Dola za Kimarekani 282 milioni, hawana nama ya kuyatumia, wameamua kuwachokoza wananchi ili waweze kuyatumia.
“Wananchi nawaomba sisi tuache vurugu ili sasa hayo magari yao walionunua tuone watakavyo yatumia, wananua magari alafu shuleni hakuna madawati na barabara hakuna,” amesema Lowassa.
Pia amesema baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kutoa haki kwa familia na chama hicho kumuaga Mawazo, imeonekana jeshi la polisi halina intelejensia wanayodai bali ni waongo watupu.
Lowassa amesema hukumu ya Jaji Lameck Mlacha wa Mahakama Kuu, iwe somo kwa polisi wa Tanzania kutokana na kujawa wivu usiofahamika.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akizungumza katika shughuli hiyo ya kuaga mwili huo, amesema haki imepatikana mahakamani na kuwaumbua polisi.
“Wananchi wamechoka kuuliwa kama ilivyotokea kwa wafuasi wa Chadema tangu mwaka 2011 mpaka sasa wakati huu wa Mawazo…tumechoka kufa, mwenye akili na afahamu,” amesema Mbowe.
Hata hivyo, amesema wapo baadhi ya askari polisi wema na wenye kutekeleza weledi wa kazi zao kiufasaha, lakini wapo ambao hawafai kuwatumikia na kuwaongoza wananchi.
Aidha, aliwashukuru watu wote waliojitolea kuisaidia familia ya Marehemu Mawazo hasa mtoto wake Precious Mawazo (9) anayesoma darasa la nne akiwamo Lowassa pamoja na wabunge 113 wanaotoka vyama vya Ukawa, kwa kila mmoja kujitolea Sh. 300,000 na kupatikana 36 milioni.
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema chama hicho kinajiandaa kumfungulia mashitaka ya madai Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, baada ya kuweka zuio la mwili wa Mawazo kutoagwa jijini Mwanza hadi Mahakama Kuu ilipotupilia mbali zuio hilo.
“Kamanada Mkumbo lazima alipe gharama zote za siku nane za kumweka Lowassa, Sumaye, Mbowe na wabunge zaidi ya 50 jijini Mwanza wakisubiri mahakama itende haki na hatimaye kushinda kesi,” amesema mwenyekiti Mbowe.
Frederick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, amesema nchi yetu awali ilikuwa inasifiwa kwa amani na utulivu, lakini sasa inawaua watu wanaodai haki.
“Hii ni kama ilivyokuwa Afrika Kusini wakati wa utawala wa Makaburu, mpigania haki Steve Bicco, aliuawa kama alivyouawa Mawazo, lakini mwisho wake makaburu hao walitoa haki kwa waliowengi licha ya kuwa na bunduki na polisi wengi kuliko kwetu,” amesema Sumaye.
Sumaye amesema Marehemu Mawazo alikuwa akidai haki majukwaani, lakini watu waliotaka kudaiwa haki waliamua kumuua huku vyombo vya dola vikipindapinda ili haki isipatikane kwa amani.
“Lazima tusimamie amani na tupinge kuonewa maana ipo simu moja watu watachoka kuonewa kama ilivyo sasa,” amesema.
Mtoto wa Mawazo 
Mtoto wa marehemu Mawazo, Precious Mawazo (9), amesema waliomuua baba yake hawajakatisha ndoto yake ya kuwa mwanasiasa kwani siku moja atakuwa mwanasiasa mkubwa.
“Wakati wa uhai wa baba, ndoto yangu ilikuwa niwe mwanasiasa, lakini nitaendelea na hiyo ndoto hadi niwe mwanasiasa mkubwa nchini…katuacha na mdogo wangu akiwa na miaka miwili tunaamini Mungu atatusaidia,” amesema Precious.
Godbless Lema 
Godbless Lema wa Arusha akitoa salamu za rambirambi uwanjani hapo, amesema marehemu Mawazo alikuwa rafiki yake wa damu tangu akiwa jijini Arusha na kumshawishi kuingia kwenye siasa, lakini aliuliwa kinyama na watu wasiopenda haki.
Lema amesema ukimya wa wananchi katika mauaji wanayofanyiwa, si uoga bali ni unatokana na uchungu walionao, kwani wauaji wakiwa huru hakuna atakayekuwa salama.
Mchungaji Swai 
Mchungaji Bernard Swai wa kanisa la Winners jijini Mwanza, akihubiri katika misa ya kumuaga, amesema wanadamu hawajumbwa na Mungu kwa ajili ya kuuana bali kupendana.
“Lazima wanadamu wajiulize kwanini vijana wengi wanatumiwa ili kuwaua wengine, tunaiomba serikali iliyopo madarakani isimamie na kukomesha kabisa mauaji yasiyo na hatia,” amesema Mchungaji Swai.
Amesema damu ya Mawazo inalia mbele ya Mungu na wale waliofanya kitendo cha kinyama kwa mtu huyo macho ya Mungu yanamuona popote alipo.
Hata hivyo wengine waliotoa salamu za rambirambi ni Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), Baraza la Wanawake (Bawacha) na chama cha NCCR Mageuzi kilichosimama kuwakilisha vyama vinavyounda Ukawa (CUF na NLD).


No comments: