Monday, November 30, 2015

Zitto Kabwe aibua tena Ufisadi wa $600m,soma story nzima hapa


Ufisadi wa $600m hati fungani za Serikali: Tusikubali ya Rada, hatua zichukuliwe

Taasisi ya Serious Fraud Office ya Uingereza ( SFO ) inafanya mazungumzo na Benki ya Standard Group ya Afrika ya Kusini Lakini iliyoorodheshwa katika soko la hisa ya Uingereza ( London Stock Exchange ) ili kumalizana kuhusu tuhuma za rushwa katika ununuzi wa hati fungani za Serikali ya Tanzania yenye thamani ya dola za kimarekani milioni Mia Sita ( $ 600m ). Mazungumzo hayo yanafanywa mbele ya Jaji katika mji wa London.

Ndugu wanahabari, ni jambo la kawaida kwa serikali yoyote duniani kuuza hati fungani. Mnamo mwaka 2011/2012 Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliuza hati fungani ( Bonds ) zenye thamani ya dola za kimarekani 600 milioni ($600 million), dhamana hizo za serikali zilinunuliwa na benki ya kigeni  (Stanbic) ambayo ni mali ya Standard Group ya Afrika ya Kusini, yenye makao makuu yake huko London, Uingereza.

Hata hivyo, sehemu ya fedha hizo haikuingia kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na pia gharama za Bond hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati kati ( middle men ) na hivyo kupelekea rushwa ya takribani $60 milioni kutolewa Kwa maafisa waliothibitisha biashara hiyo.

Ndugu wanahabari, taasisi za kiuchuanguzi za nchini Uingereza, hasa ile ya kushughulikia makosa ya rushwa (Serious Fraud Office-SFO) tayari imeshafanya uchunguzi wake wa awali kwa kuhusisha pande zote zinazohusika, na wamegundua kuwepo kwa rushwa kubwa katika mchakato huo, jambo ambalo liliwafanya washauri uongozi wa benki hiyo hapa nchini kuondolewa na kurejeshwa nchini Uingereza kwa hatua zaidi. Hata hivyo SFO na Standard Group wanataka kulimaliza jambo hili Kwa mtindo wa walivyomaliza suala la radar.

Ndugu wanahabari, Chama changu cha ACT-Wazalendo, kinazitaka mamlaka za kiuchunguzi hapa nchini, kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na upotevu wa $600 milioni, ambazo kwa pesa ya Tanzania ni zaidi ya shilingi 1.2 trilioni.  Hicho ni kiwango kikubwa sana cha fedha, ikilinganishwa na makusanyo ya Mamlaka ya Maapato Tanzania (TRA). Tunaitaka Benki Kuu ya Tanzania, FIU Tanzania na PCCB kuweka hadharani taarifa ya chunguzi zao na kueleza ni kwanini hawajachukua hatua mpaka sasa.

Ndugu wanahabari, chama cha ACT-Wazalendo, kinaunga mkono jitihada za Rais wetu Dr John Pombe Joseph Magufuli, za kutumbua majipu, hivyo tungependa kuona Mheshimiwa Rais akichukua hatua kwenye jambo hili ambalo lina maslahi mapana ya nchi yetu, hasa ikizingatiwa na uzoefu tulionao katika masakata kama hayo yanayohusisha nchi za kigeni, mfano mmojawapo ni sakata la rada, ambalo vyombo vyetu vya uchunguzi vilisema hakukuwa na rushwa, na baadaye serikali ya Uingereza ilithibitisha pasina shaka kwamba kulikuwa na rushwa, na baadaye serikali yetu ilirudishiwa sehemu ya fedha zilizozidi kwenye manunuzi ya rada ( chenji ya rada ).

Chama cha ACT Wazalendo kinasubiri taarifa ya makubaliano ( settlement ) Kati ya SFO na Benki ya Standard Group ( Benki mama ya Stanbic ) ili kushauri zaidi hatua za kuchukua. Ikumbukwe kuwa Benki ya Stanbic ndio ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow na mpaka sasa haijachukuliwa hatua zozote kama ilivyoagizwa na Bunge. Benki hiyo imewaficha waliochota fedha za escrow mpaka Leo.


( imesainiwa )
Masasi, 30 Novemba 2015
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb

No comments: