Chama cha ACT – WAZALENDO kinafuatilia kwa karibu hatua zinazochukuliwa na serikali katika maeneo mbalimbali kama njia ya kuleta suluhu ya kudumu katika suala zima la utunzaji mazingira na hasa suala la usafi na utunzaji,usimamizi na uzalishaji wa taka ili kuimarisha mfumo wa taka kisera na kisheria.
ACT-Wazalendo,tunaamini mfumo wa kusimamia sera na sheria unatakiwa uendane na kiwango cha ukuaji na ongezeko la watu katika miji yote nchini.
Tanzania kama nchi tumekuwa nyuma katika kuhusisha ongezeko la watu na upatikanaji wa huduma za msingi zikiwemo huduma za usafi na mazingira yanayofaa kwa maisha ya binadamu.
Kwa sababu ya pengo hili la kisera na kisheria, tamko la Rais la kufanya usafi kama sehemu ya kusherehekea siku kuu ya uhuru ili kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi na kujikinga na maradhi yanayotokana na uchafu, lilikutana na pengo hili na kuleta matumaini na mkanganyiko wakati huo huo.
Wakati wengi tulifurahia kushiriki na kuokoa fedha za sherehe ya uhuru,pia tulihitaji kujua utaratibu wa kutimiza jukumu hili kwa umahiri, kitaalam na kisheria na kulifanya liwe endelevu zaidi.
Tulihitaji kujua mahali taka zitapelekwa baada ya kukusanywa, na maeneo ya ukusanyaji wa taka hizo. Tulihitaji pia kujua mpango wa kuchambua taka ili zitumike kwa makusudi mbalimbali endelevu na ya kuleta ajira za awali katika sekta hii.
Tulihitaji fedha pia za kuhakikisha zoezi linafanyika kwa umahiri zaidi. Baada ya hatua hizi kupita, ni wakati wa kujipanga kuhakikisha kuwa taka zinatuletea ajira na kuinua viwanda vitokanavyo na taka kama mbolea, chuma, chupa, na karatasi za aina mbalimbali.
ACT Wazalendo tunaamini maelekezo ya waziri ya kuliweka jukumu hili chini ya halmashauri zetu litagonga mwamba wa ufanisi kama halitafuata taratibu za kitaalam za kuhakikisha uwepo wa kutosha wa maeneo ya kuhifadhi taka na kuwa na fedha za wachambuzi wa taka waliolindwa dhidi ya mainzi, vumbi na uchafu mwingine hatarishi.
Tanzania inatumia mfumo wa aina mbili wa usimamizi wa usafi, na ukusanyaji taka:
sehemu moja imebinafsisha huduma hizi na sehemu zingine bado utaratibu wa umma unatumika kusimamia usafi wa mazingira na ukusanyaji taka.
Tunahitaji kuwa na taarifa kamili juu ya maeneo (kata na mitaa) iliyobinafsishiwa huduma hii na ile inayotegemea huduma ya umma, kwa baadhi ya maeneo na hasa ya mijini na manispaa.
Tunasema hivi kwa sababu Majiji yote na baadhi ya manispaa ni moja ya maeneo ambayo huduma ya taka imebinafsishwa kwa watu na makampuni binafsi.
Huduma ya wakandarasi binafsi haijaonekana kuwa suluhu ya ukusanyaji, utunzaji na uzalishaji wa taka licha ya wao kulipwa na serikali, ama na wateja wao kwa huduma hiyo.
Tamko la kufanya usafi likiunganisha jukumu la wakandarasi binafsi wa shughuli za usafi, litatupa sura tofauti na mgawanyo wa majukumu kati ya huduma binafsi na huduma za umma na jukumu la umma.
Hatua hii inaweza kupunguza gharama ambazo tayari zinachukuliwa na serikali kwa upande mmoja na wakandarasi binafsi kwa upande wa pili.
Tunaomba ofisi ya Makamu wa Rais kitengo cha mazingira kuhakikisha wakandarasi hawa wanatekeleza majukumu yao na kuwa thamani ya kazi yao inafahamika. Kwa hali ya sasa, ACT – WAZALENDO inamtaka waziri anayehusika na masuala ya mazingira kuhakikisha kuwa zoezi la kuweka usafi wa mazingira katika nchi yetu linachukua sura pana ya uendelevu, uzalishaji ajira, ukuzaji wa uchumi na hata uanzishaji wa viwanda vinayotokana na bidhaa za taka.
Taka ni Mali. Tuzalishe taka. Tuhifadhi taka mahali salama kwa maisha salama na tuzalishe taka kujiletea maendeleo endelevu. Pamoja na salaam za kumaliza mwaka 2015.
Mama Anna Elisha Mghwira
Mwenyekiti wa ACT –WAZALENDO
No comments:
Post a Comment