Balozi Seif Ali Iddi akinukuu kifungu cha Katiba ya Zanzibar kinachomruhusu Dkt. Ali Muhamed Shein kuendelea kuiongoza Zanzibar mpaka atakapoapishwa Rais mwengine.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kufikia miaka 52 Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa Makamu wa Pili wa Rais w Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakifuatiliia mkutano huo uliofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
……………………………………………………………………………………………….
Na Khadija Khamis – Maelezo
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuwa Maadhimisho ya Shereha za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yapo kama kawaida na yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 3.12.2016 kwa kazi za usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya makaazi pamoja na sehemu za kutolea huduma za kijamii kama vile Hospitali Sokoni na maeneo mengine.
Kauli hiyo imetolewa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema ingawa zoezi la usafi hufanyika kila tunapoanza maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi lakini kwa muda huu wananchi wanapaswa kuchukuwa juhudi maalum ili kuhakikisha kuwa maeneo yote yanakuwa safi muda wote kwa vile hivi sasa nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la kuenea kwa maradhi ya kipindupindu.
“Zoezi la usafi wa mazingira litakuwa la lazima na kutaandaliwa utaratibu maalum kwa kila Mamlaka za Mikoa ,Wilaya Baraza la Manispaa Mabaraza ya Miji na Halmashauri za wilaya kuratibu zoezi la usafi na viongozi Wakuu wa Kitaifa wataungana nasi katika katika maeneo watakayopangiwa, “Alisisistiza.
Amesema mbali na usafi wa mazingira, katika maadhimisho ya mwaka huu kutakuwa na shughuli mbali mbali zikiwemo ujenzi wa Taifa ,uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na burudani na michezo na kilele cha maadhimisho hayo itakuwa siku ya Jumanne katika Kiwanja cha Amaani.
“Kama kawaida kila ifikapo tarehe 12 Januari ya kila mwaka nchi yetu huadhimisha sherehe za Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa mwaka 2016 tutakuwa tunatimiza miaka 52 tangu viongozi na wazee wetu walivyokomboa nchi yetu,” alisema Balozi Seif Ali Iddi.
Alikumbusha kuwa mafanikio na maendeleo yaliyopatikana Zanzibar yanatokana na imani na jitihada kubwa za viongozi ambao ni wanamapinduzi chini ya uongozi wa Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume aliyeweka msingi imara wa mashirikiano .
Alisema siku ya kilele cha maadhimisho hayo katika Uwanja wa Amaani kutakuwa na Gwaride la Vikosi vya Ulinzina Usalama , Burudani ya Ngoma za Utamaduni pamoja na Maandamano ya Wananchi wa Mikoa Mitano ya Zanzibar.
Makamo wa Pili Balozi Seif Ali Iddi alisema kuwa sherehe hizo zitahudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa kutoka Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya miaka 52 ya Mpinduzi ya Zanzibar na amewahakikishia Serikali imejipanga kikamilifu kuona kunakuwa na hali ya utulivu na usalama mkubwa katika maeneo yote ya Zanzibar wakati wa maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment