Saturday, January 9, 2016

Kuhusu Sakata La Bomoa Bomoa hii ni kauli ya ACT wazalendo



Chama cha ACT WAZALENDO kimeitaka serikali ya awamu ya tano wakati ikiendelea na zoezi la bomoa bomoa kuhakikisha kuwa linawajali wananchi ambao wanabomolewa nyumba zao kwa kuhakikisha wanapata sehemu za kujenga na kendeleza maisha yao kwani kushindwa kufanya hivyo hakutoondoa mwanya wa wananchi kuendelea kujenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Naibu katibu mkuu wa chama hicho (bara) Bwana MSAFIRI  MTEMELWA wakati akizungumza na waandishi wa habari Kuhusu maswala mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwemo swala la bomoa bomoa.

Akizungumza amesema kuwa swala la wananchi kukaa mabondeni sio kosa la wananchi hao pekee kwani kuna baadhi ya watendaji ambao walikosa utu na uzalendo wa nchi yao na kuamua kuwauzia wananchi maeneo hayo hatarishi hivyo ni bora serikali ikaanza kuhakikisha kuwa inawakamata baadhi ya watendaji hao ambao kwa sasa wamesababishia wananchi hao hasara kubwa ikiwemo kibomolewa nyumba zao.

“Tunaamini mpaka kufikia hatua ya wananchi kubomolewa nyumba zao kuna watu walikosa uzalendo kwa taifa lao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa wakati unaotakiwa na hawa ni watendaji kuanzia ngazi ya mtaa mpaka ngazi ya taifa hivyo ni lazima serikali iwawajibishe”Amesema kiongozi huyo wa ACT –wazalendo.

Amesema kuwa watendaji hao sio kwamba wamewaingizia wananchi hasara kubwa bali pia wameshiriki kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unahujumiwa kwa kuruhusu ujenzi wa maeneo yasiyoruhusiwa ambapo leo yanabomolewa.

Aidha ACT-Wazalendo wameitaka serikali kufanya uchunguzi na kujiridhisha kama viwanja vya mabwepande vilivyotengwa kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Jijini Dar es salaam ziliwafikia walengwa ambao leo wanasema hawajawahi kupewa viwanja hivyo.

TUZO YA SAMATTA

Katika hatua nyingine chama hicho kimempongeza mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea katika club ya TP MAZEMBE ya congo MBWANA SAMATTA ambaye mwishoni mwa wiki hii ametangazwa kuwa mchezaji bora barani Africa kwa wachezaji wanaoshiriki katika ligi za ndani ya bara hili.

Msafiri Mtemelwa ambaye ni naibu katibu mkuu(Bara) wa chama hicho akitoa pongezi hizo amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa tunawapa wakina Samatta wengi ni lazima serikali kujikita katika kuhakikisha kuwa mifumo ya michezo mbalimbali inaboreshwa pamoja na kuanza kwa kurudisha maeneo ya wazi yaliyokuwa yakitumiwa na vijana kwa ajili ya michezo mbalimbali.

Hata hivyo ACT wazalendo wamemtakia kila la kheri mchezaji huyo katika harakati zake za kimichezo na kuitangaza Tanzania zaidi.

No comments: