Mume wa marehemu akiwa pembeni ya mwili wa mkewe.
Na Dustan Shekidele, UWAZI
MOROGORO: Ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni! Kijana Said Ally Mwinyimvua anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro akidaiwa kumuua kwa kumcharanga mapanga mama yake mzazi, Sikuzani Said (70), kisa kikidaiwa kuwa ni kunyimwa wali (ubwabwa) na kupewa mdogo wake, Abass ambaye ni mziwanda, Uwazi linakupasha.
Tukio hilo lililoacha majonzi, lilijiri wiki iliyopita nyumbani kwa familia hiyo, Kijiji cha Kungwe, Kata ya Tomondo, Wilaya ya Morogoro Vijijini.
Uwazi lilifika eneo la tukio na kuwakuta viongozi wa kijiji hicho kwa kushirikiana na mgambo wakimpeleka mtuhumiwa huyo kwenye Kituo cha Polisi Mkuyuni ambako anashikiliwa hadi sasa.
Abass anayedaiwa kumuua mamaake.
Kwa upande wake, mume wa marehemu, Ally Mwinyimvua Dugulu ‘Mzee Kisauti’ (80), alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alikuwa na haya ya kusema:
”Mimi na mke wangu tumejaliwa kuzaa watoto tisa, wa kike wanne na wa kiume watano. Wakike wote wameolewa huko mijini na wa kiume watatu wameoa pia hukohuko mjini. Hapa nyumbani tumebaki na watoto wawili, Said na Abass ambaye ndiye mtoto wa mwisho.
“Kwa muda mrefu Said amekuwa akitulalamikia sisi wazazi kwamba tunampenda zaidi mdogo wake kuliko yeye, jambo ambalo si la kweli.
“Hawa watoto waliwekewa zamu ya kupika. Siku ya tukio ilikuwa zamu ya Said, alipika ubwabwa, akaubeba wakaenda shamba. Ubwabwa mwingine waliubakisha kwa ajili ya jioni. Mimi kutokana na kazi zangu nilibaki hapa nyumbani, wakaniwekea ubwabwa wangu.
Polisi wakiwa eneo la tukio.
Saa 11 jioni, Abass na mama yake walirudi huku wakimuacha Said shambani.
“Saa moja usiku, Said alirudi, akaenda kwenye kabati na kukuta ubwabwa umekwisha. Alimuuliza mama yake, akamjibu kwamba mdogo wake amekula wote hivyo yeye ale kiporo cha jana, jambo ambalo lilimkera sana. Alichukua panga alilotoka nalo shamba na kuanza kumcharanga mama yake mwili mzima.
“Mimi kutokana na uzee, nilishindwa kumsaidia mke wangu mpaka anakata roho alikuwa akipiga kelele,” alisema Mzee Kisauti.Kwa upande wake, Abass alipohojiwa, alisema alijaribu kumsaidia mama yake bila mafanikio kwani kaka yake alitishia kumuua na yeye.
“lshu kama ni ubwabwa angeniambia ningemuachia ale kuliko kumuua mama. Nilijitahidi sana kumtetea mama lakini kaka alitaka kunikata na panga hivyo nilikwenda kuita majirani ambapo walipofika tulikuta mama ameshafariki dunia huku kaka akikimbia,” alisema Abass.
Alipoulizwa kama kaka yake anakunywa pombe au kuvuta bangi, Abass alisema hatumii vitu hivyo.Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, diwani wa kata hiyo, Hamis lssa Msangale alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema:
“Mtuhumiwa baada ya kumuua mama yake kwa kumcharanga mapanga zaidi ya 20 mwilini, usiku huohuo alitoweka nyumbani na kwenda kujificha huku wananchi wenye hasira wakimsaka kijiji kizima kwa lengo la kulipa kisasi.
“Kwa bahati nzuri alfajiri, raia wema walitujulisha kwamba Said amepitiwa na usingizi amelala chini ya mwembe. Nilimjulisha mwenyekiti wa kijiji, tukachukua mgambo tukaenda kumkamata na kupita naye vichakani mpaka Kituo cha Polisi Mkuyuni tukiwakwepa wananchi wenye hasira,” alisema kiongozi huyo.
Akaendelea: “Kwa sasa tukio hili ndiyo gumzo kata nzima na ni tukio la kwanza kutokea kwenye kata yetu. Tunashukuru mtuhumiwa tumemkamata na muda huu tunafanya utaratibu wa kumzika marehemu kwenye makaburi ya kitongojini hapa.
No comments:
Post a Comment