Chama
cha ACT Wazalendo kinaipa uzito wa kipekee ziara ya kwanza nchini na barani
Afrika ya rais wa taifa la Kisoshalisti la Vietnam Truong Sang anayezuru
Tanzania kuanzia siku ya Jumatano tarehe 9 Machi, 2016.
Kwetu
Chama cha Wazalendo, Vietnam ni mfano wa kuigwa na nchi zinazoendelea juu ya
umuhimu wa sera bora na usimamizi thabiti wa rasilimali katika kuipaisha nchi
kiuchumi.
Tanzania
na Vietnam zilipopata uhuru, zilikuwa katika kiwango kinachokaribiana kiuchumi.
Sasa Vietnam imesonga mbele kiuchumi mara dufu zaidi ya Tanzania karibu kwenye
kila nyanja.
Mifano
ni mingi: Vietnam iliyokuja kuchukua mbegu na kujifunza upandaji wa mikorosho
nchini Tanzania ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa korosho ghafi
kwa sasa. Tofauti na Tanzania ambayo huuza sehemu kubwa ya korosho zake zikiwa
ghafi, nchini Vietnam korosho hubanguliwa kabla ya kuuzwa ndani na nje ya nchi
ili kuziongezea thamani.
Haya yamewezekana
kwa sababu, pamoja na mambo mengine, Vietnam imewekeza katika uendelezaji wa
teknolojia rahisi ya ubanguaji wa korosho vijijini ambapo korosho zinabanguliwa
vijijini zinakozalishwa na kuongeza ajira.
Pia, Vietnam
iliyokuja kuchukua mbegu ya kahawa Tanzania ndiyo nchi ya pili kwa uzalishaji
wa kahawa duniani kwa sasa ikitanguliwa na Brazil. Vietnam imewahi pia kuchukua
samaki aina ya Sato ili kuendeleza sekta yao ya uvuvi. Swali la kujiuliza, sisi
tunachukua nini kutoka Vietnam?
Vietnam
inafanya vyema zaidi pia kwenye maeneo ya viwanda, usalama wa chakula,
teknolojia ya mawasiliano na ustawi wa watu wake.
Wakati
Tanzania ikikumbatia masharti ya soko huria na kubinafsisha kiholela viwanda,
mashamba ya umma na makampuni kwa maelekezo ya mashirika ya fedha ya kimataifa,
Vietnam ilibuni mfumo wake wa mageuzi ya kiuchumi (“Doi Moi”) unaovutia mitaji binafsi ili ishindane na mitaji ya
dola.
Maono na
msimamo wa kiuchumi wa ACT Wazalendo daima umekuwa ni ujenzi wa uchumi unaostawisha
sekta binafsi bila kuathiri jukumu la dola kuhodhi sekta nyeti za kiuchumi kwa
manufaa ya umma.
Ziara ya
Rais wa Taifa la kijamaa la Vietnam ifumbue macho serikali ya CCM kutoka kwenye
maneno matupu ya uchumi wa viwanda na kwenda kwenye vitendo. Mawaziri wa CCM
wamekuwa wakiendelea kutoa ahadi za ujenzi wa viwanda kana kwamba bado tupo
kwenye kampeni. Chama cha ACT kinawashawishi wananchi kuhitaji utekelezaji wa
ahadi sasa.
Tunachukua
fursa hii kukukaribisha sana Tanzania Rais Truong Sang.
Imetolewa
leo tarehe 9, Machi 2016.
Ado
Shaibu,
Katibu,
Itikadi, Mawasiliano kwa Umma na Uenezi.
Simu:
0653619906
No comments:
Post a Comment