Na. Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.
…………………………………………..
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki amewataka askari polisi kote nchini kufanya kazi kwa weledi ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Mhe.John Pombe Magufuli ambayo lengo lake ni kuwatumikia wananchi.
Hayo aliyasema wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano kwa askari polisi watakaokuwa wakitoa huduma katika vituo vya kuhamishika (mobile police station) vinavyotarajiwa kuanza kazi katika mkoa wa kipolisi Kinondoni (mkoa wa mfano) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa kuboresha usalama wa raia na mali zao nchini, mpango ambao unatekelezwa na Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais, Usimamizi na utekelezaji wa miradi (PDB).
Alisema katika kipindi hiki kila askari anatakiwa kufanya kazi kwa kasi na kufuata maadili ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora kwakuwa ndio lengo la Jeshi la Polisi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vyema na kwa wakati katika vituo vya Polisi kwakufuata taratibu na misingi ya kazi za Polisi.
Aidha, aliwataka askari hao ambao watakuwa wakitoa huduma katika vituo hivyo vya kuhamishika kuhakikisha kuwa lengo la kuwepo kwa vituo hivyo linatimia kwa kutoa huduma bora na ya haraka ili kujibu yale yote yaliyoainishwa katika mpango huo.
“Jambo kubwa lililoainishwa katika maabara iliyoandaa mpango huu ni suala la kuchelewa kufika katika matukio ya kiuhalifu hivyo kwa kutumia raslimali zilizopo pamoja na vituo hivi vya kuhamishika ni wazi kuwa sasa tutajitahidi kufika katika matukio mapema”Alisema Kaniki.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha kusimamia mpango huo ndani ya Jeshi la Polisi, Naibu kamishna wa Polisi DCP Goodluck Mongi alisema, lengo la mafunzo hayo ya siku tano ni kuwapa utayari askari katika kutekeleza majukumu yao ili kuleta matokeo makubwa katika mkoa wa kipolisi Kinondoni ambao ni mkoa wa majaribio wa mpango huo ndani ya Jeshi la Polisi.
Alisema mpango huo umeainisha mambo mengi ikiwemo kuwepo kwa vituo vya kuhamishika ili kuweza kuwafikia wananchi kwa haraka na vituo hivyo vitawekwa kwa awamu ili kuhakikisha kila anayehitaji huduma za Kipolisi hapati shida kwa kwenda umbali mrefu kuzitafuta hali itakayopelekea kudhibiti na kuzuia uhalifu wa aina zote.
No comments:
Post a Comment