NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ameifungia bao klabu yake, KRC Genk ikishinda 4-1 dhidi ya KV Oostende katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, maarufu kama Pro League usiku huu Uwanja wa Cristal Arena mjini Genk.
Samatta aliyeanza kwa mara ya kwanza leo tangu asajiliwe Genk Januari kutoka TP Mazembe ya DRC, alifunga bao hilo dakika ya 24 kwa kichwa akiunganisha krosi ya mshambuliaji wa Jamaica, Leon Bailey.
Bailey naye akafunga mweyewe bao zuri la pili dakika ya 39, akimlamba chenga kipa Mbelgiji Wouter Biebauw baada ya pasi ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy.
Samatta akatoka dakika ya 74 kumpisha mshambuliaji Mbrazil, Igor Alberto Rinck de Camargo aliyekwenda kumsetia Mspanyola Alejandro Pozuelo kufunga bao la tatu dakika ya 81.
Pozuelo naye akamsetia Camargo kuifungia Genk bao la nne dakika ya 88, kabla ya kiungo Mcameroon, Sebastien Siani kuifungia KV Oostende bao la kufutia machozi dakika ya 90.
Kikosi cha Genk kilikuwa; M. Bizot, C. Kabasele, S. Dewaest, J. Uronen, T. Castagne, O. Ndidi/ Y. Buyens dk87, Pozuelo, N. Kebano, R. Malinovskiy/ B. Kumordzi dk81, M. Samatta/ I. de Camargo dk74 na L. Bailey.
No comments:
Post a Comment