Wednesday, March 16, 2016

UDHAIFU(3),CHANGAMOTO & SIFA MUHIMU ZA KATIBU MKUU MPYA WA CHADEMA - DK. VINCENT BIYEGELA MASHINJI.


Newly appointed Chadema Secretary General, DrHISTORIA NA ELIMU


Dk. Vincent Biyegela Mashinji ni Katibu Mkuu wa nne wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akitanguliwa na Bob Makani, Dk. Walid Kabourou na Dk. Wilbroad Peter Slaa. Kwa hakika yeye ndiye Katibu Mkuu wa CHADEMA mwenye umri mdogo kuliko wote.
Mashinji alizaliwa tarehe 11 Januari 1973 wilayani Musoma Mkoa wa Mara. 

Wazazi wa Dk. Mashinji ni Raphael Biyegela (baba mzazi) na mama yake ni Katarina Mwire.
Mashinji alianza elimu yake ya Msingi mwaka 1981 na kuhitimu darasa la saba mwaka 1987 katika Shule ya msingi Iligamba. Kuanzia Januari 1988 hadi Oktoba 1991 Mashinji alipata elimu ya Sekondari katika Shule ya Seminari ya Makoko iliyoko Musoma Mjini (St. Pius Seminary), mkoani Mara. Ufaulu wake wa kidato cha nne ulimpa nafasi muhimu ya kuendelea na masomo ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Mzumbe iliyoko mkoani Morogoro. Alijiunga mzumbe mwezi Juni 1992 na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1994 akisoma mchepuo wa PCB.


Mwaka 1995 Mashinji alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na ilipohitimu mwaka 2001 alikutunukiwa shahada ya udaktari wa Binadamu (MD).
Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaethesiolojia (Anaesthesiology) katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) – Shahada hii ya uzamili ni ya Udaktari Bingwa wa Magonjwa ya Binadamu (MMED). Akiwa hapo Chuo Kikuu cha Muhimbili alisoma na kutunukiwa Cheti cha Utafiti

Mwaka 2007- 2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili akibobea kwenye Utawala na Biashara (MBA).
Kati ya mwaka 2008 hadi 2010 Mashinji amesoma katika Shule ya Menejimenti ya Evin iliyoko Mikocheni jijini Dar Es Salaam na kutunukiwa Shahada ya Uzamili ya Uhusiano wa Umma (Masters in Public Relations) – taasisi hii inashirikiana na baadhi ya taasisi na vyuo vya nchini Uingereza kuendesha na kutoa mafunzo yake.

Mashinji pia amepata kusoma katika Shule ya Anderson ya Chuo Kikuu cha California nchini Marekani na kutunukiwa Stashahada ya Usimamizi wa Maendeleo (Diploma in Development management) na mwaka 2008 alisoma na kuhitimu cheti cha Virolojia ya Mwanadamu (Human Virology) kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu Maryland kilichoko nchini Marekani.

Hadi anateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, yeye ni mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii anayosomea Chuo Kikuu cha Roehampton kilichoko London Uingereza na pia anaendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT). Amemuoa Happy na wana watoto kadhaa akiwemo Allen na Aaron.

UZOEFU
Uzoefu wa kitaaluma wa Dk. Mashinji ulianza mwaka 2001 kwa kufanya kazi katika Hospitali ya taifa Muhimbili kama Daktari wa Mazoezi (Mwanafunzi) na alidumu hapo hadi mwaka 2002. Kati ya mwaka 2002 hadi 2003 amefanya kazi kama Mtafiti wa Kujitegemea na baadaye mwaka 2003 alifanya kazi na Shirika la Healthscope Tanzania Limited kama Mtafiti Msaidizi.

Kuanzia mwaka 2003 hadi 2005 Mashinji aliajiriwa rasmi kama daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mwaka 2005 hadi 2006 akafanya kazi kama Daktari Bingwa wa hospitali ya Regency iliyoko Dar Es Salaam. Mwaka 2006 hadi 2008 amekuwa msimamizi wa mradi wa Shirika la Kimataifa la Afya la IMA World Health katika shughuli za miradi yake hapa Tanzania hasa akitumiwa kuanziasha ofisi ya shirika hilo mkoani Mwanza na kuwa kiongozi wa shirika mkoani hapo.

Kati ya mwaka 2008 hadi 2015 Mashinji amefanya kazi kama Mshauri Mtaalamu Mwandamizi wa Mpango wa Dunia wa Maryland nchini Tanzania (Maryland Global Initiative Tanzania - MGIT) uliokuwa unafanywa kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Maryland kilichoko Baltimore, nchini Marekani
Kuanzia mwaka 2008 hadi anateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA amekuwa Mshauri wa Tiba za magonjwa ya Kifua Kikuu (TB) na Virusi vya Ukimwi (HIV) katika shirika hilo hilo la IMA World Health. Kutokana na kazi yake ya miaka 10 kwenye eneo la TB na HIV Dk.
Mashinji amekuwa msaada mkubwa kwa taifa na Wizara ya Afya ya Tanzania imekuwa inatambua mchango wake mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kupambana na Kifua Kikuu na Ukimwi mara nyingi akifanya hivyo kama mtafiti, mkufunzi wa kitaifa n.k.

Tangu mwaka 2015 hadi anateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mashinji amekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kitaalamu katika Ushirika wa Imani Tanzania (Tanzania Interfaith Partnership - TIP). Ushirika huu unahusisha ofisi za CCT, BAKWATA, TEC na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar. Kwa kiasi kikubwa majukumu yake katika ushirika huu yalibakia kuwa ya taaluma yake ya afya hasa akitoa ushauri wa namna bora ambavyo taasisi hizo zinaweza kutoa mchango wake kwa jamii kwa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na kuimarisha ustawi wa afya za wananchi.

SIFA MUHIMU

Kwanza, Dk. Mashinji ni msomi wa haja. Na kwa rekodi za makatibu wakuu waliowahi kuwepo kwenye vyama vyote vya siasa hapa Tanzania (chini ya mfumo wa Chama kimoja na mfumo wa vyama vingi), huyu ndiye anaweka rekodi ya kuwa msomi aliyebobea zaidi kuliko wengine. Ana vyeti vya kitaaluma viwili, Stashahada moja, Shahada moja, Shahada za Uzamili tatu na hivi sasa anaendelea na masomo ya shahada moja ya uzamili pamoja na shahada ya uzamivu (PhD).

Bila shaka, akikamilisha masomo kwenye viporo hivi viwili atafikisha jumla ya shahada 6 za ngazi mbalimbali za Chuo Kikuu na hiyo inaweza kumfanya awe mmoja wa makatibu wakuu wa vyama wenye shahada nyingi sana hata katika ngazi ya dunia. Pamoja na kwamba elimu siyo kila kitu kwenye uongozi lakini kuwa na kiongozi mwenye elimu nzuri ni heri na muhimu kuliko kuwa na kiongozi mwenye elimu ya kubabaisha.

Pili, Mashinji anafahamika kwa ujasiri na weledi wa kioungozi. Wataalamu wengi wa tiba nchini Tanzania wanamuona kama kiongozi wao. Baada ya kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari, Ulimboka – Ni. Dk. Mashinji na wenzake ndiyo walisimama kidete kuanzisha mgomo wa madaktari ili kudai haki ya Ulimboka pamoja na kudai uboreshwaji wa mazingira ya huduma za afya kwa mgonjwa na daktari.

Madaktari nilioongea nao wameniambia kuwa pamoja na hali hatari iliyowakabili wakati huo huku vyombo vya dola vikiwasaka usiku na mchana, Dk. Mashinji na wenzake wachache ndio walionesha msimamo hata bila kuwepo Ulimboka na serikali ikawajibika kukaa nao chini ili kukubaliana hatua za kuchukua.

Pamoja na kuwa migomo ya madaktari huwaathiri wagonjwa na raia wa kawaida, haki na msingi wa walichokuwa wanakipigania kina Ulimboka na Mashinji kimekuwa dhahiri baada ya kuingia madarakani rais JPM na uamuzi wake wa kuanika hadharani na kuahidi kushughulikia mambo sugu ambayo kina Mashinji waliyapigania miaka kadhaa iliyopita.
Tatu, Dk. Mashinji ni miongoni mwa wanamkakati mahiri, muhimu na wazoefu ndani ya CHADEMA na hata katika uundaji wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). 

Kiongozi huyu anatajwa kuwa na dira na mlengo thabiti sana linapokuja suala la vyama kujiendesha kimkakati na ndiyo maana katika masuala yote muhimu ambayo CHADEMA ilipenda yatengenezewe mikakati imara na ya kudumu, Dk. Mashinji hakuachwa nje. Kwa miaka 10 iliyopita anatajwa kuwa mmoja kati ya wataalamu waliotumika vilivyo kuhuisha sera za CHADEMA wakimsaidia Prof. Kitila Mkumbo (sasa ACT – Wazalendo).

Hata katika uandishi wa ilani ya uchaguzi ya CHADEMA na UKAWA, Dk. Mashinji alishirikiana vilivyo na wataalamu kutoka vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR na NLD kuandika ilani hiyo.

Mwisho, kwa haiba Mashinji ana mambo kama matano muhimu yanayompa nguvu. Mvuto wa kiuongozi, mkweli, mtulivu, msikilizaji na mtu mwenye msimamo.
Ukikutana na Mashinji jambo la kwanza utagundua kuna “mtu” uko naye, kiongozi. Anao uwezo mkubwa wa kushawishi na hoja zake zikapendwa, ule mvuto na uonekenaji wa kiongozi ni mambo ambayo hakunyimwa na Mwenyezi Mungu. Nimewahi kufanya kazi kadhaa na daktari huyu na nikagundua anayo asili ya kusimamia ukweli, mkipeana miadi naye hutekeleza kama mlivyokubaliana na siyo mzungushaji wa mambo.

Tabia ya usikilizaji na utulivu vinambeba bila kusita na haya ni mambo muhimu kwa mtu anayepaswa kuongoza jahazi kubwa kama la CHADEMA. Waliofanya kazi naye kwa muda mrefu na padre mmoja aliyewahi kusoma na Mashinji katika Seminari ya Makoko ameniambia kuwa tangu zamani amekuwa ni mtu wa misimamo isiyoyumba na anayetaka kuona matokeo ya kazi yake.

UDHAIFU 
Udhaifu wa kwanza ambao unamkabili Mashinji ni kutokuwa maarufu ndani ya CHADEMA. Kwa kawaida na kwa vyama vingi duniani,viongozi pia huweza kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa sababu ya (umaarufu)“populism” yao ndani ya chama husika. Kisaikolojia, kiongozi maarufu ndani ya chama anao wafuasi wengi, sauti na uwezo wa kuwashawishi wengi bila kutumia nguvu kubwa. Kwa bahati mbaya sana, Mashinji siyo maarufu hata kidogo miongoni mwa wanachama wa chama hicho mikoani na kwenye wilaya mbalimbali hapa Tanzania.

Ni mtu mpya kwa asilimia 80 ya viongozi wa ngazi za chini wa CHADEMA na jambo hilo linamfanya awe na kazi kubwa ya kuanza kujijenga hivi punde mara baada ya kupewa wadhifa huu muhimu. Kutokuwa maarufu ndani ya CHADEMA kunaweza kumfanya awe kwenye wakati mgumu katika kipindi cha mvuto lakini kutaifanya kazi yake kuwa rahisi ikiwa atataka kuwa maarufu baada ya kazi kubwa ya mwaka mmoja au miwili hivi. Umaarufu wa mwanasiasa kawaida huhitaji muda mrefu wa kujijenga.

Udhaifu wa pili wa Dk. Mashinji ni kutowahi kupitia nyadhifa zingine za kisiasa ndani ya chama chake. Hili linamfanya aonekane kama mgeni sana au unaweza kutimiza ile kauli ya “usiyemtaka kaja” kwa viongozi ambao hawakuwa tayari kumuona mtu wa aina yake anapewa wadhifa alionao (kama wapo). Kiongozi huyu ametoka kwenye utumishi wa kitaaluma moja kwa moja na kuwa kiongozi wa juu mwenye maamuzi ya kiutendaji ndani ya CHADEMA.

Pamoja na kuwahi kuwa mtafiti na mpanga mikakati ya chama, kutokuwahi kushikilia uongozi kwa kipindi fulani ndani ya CHADEMA kunamuweka kwenye wakati mgumu. Atahitaji muda wa kutosha zaidi ya mwaka mmoja kujifunza na kusoma mifumo halisi ya kiuongozi ya CHADEMA, kiushiriki na kiutendaji bila kusahau hali halisi ya utendaji na usimamizi wa juu wa chama. Ikiwa hili hataliendea vizuri huwenda akapata shida sana kujiweka sawasawa kati ya mifumo aliyoikuta na ambayo huwenda atakuwa na kazi ya kuibadilisha.

Mwisho, watu wa karibu na Dk. Mashinji wanamtaja kama kiongozi mwenye hasira na asiyevumilia mambo asiyoyataka. Nimeambiwa kuwa si rahisi kumjua Dk. Mashinji na “nyongo” ya juu hadi uwe naye karibu na ufanye naye kazi kwa muda fulani. Sikuwahi kulithibitisha jambo hili tokea nimekuwa naye karibu na huwenda nikakubaliana kwamba hulifanya kwa akili na kwa ukimya ili asigundulike haraka. Hata hivyo udhaifu wa namna hii kwa kiongozi huhitaji tu ushauri au utulivu wa muda mfupi kabla hajaendelea na majukumu yake. Hili linaweza kutokuwa tatizo kubwa kwenye utendaji wake.

CHANGAMOTO.
Changamoto kubwa na ya kwanza ambayo watanzania na wapenzi wa CHADEMA wanaitizama ni ikiwa Dk. Mashinji ataweza kuvaa viatu vya Dk. Wilibroad Slaa na afanikiwe kutoa mchango mkubwa kwa ujenzi wa CHADEMA kama ilivyokuwa kwa nguli huyo wa kisiasa.

Kwa haiba Slaa na Mashinji ni watu tofauti sana na hata kwa vipaji vya uongozi kila mmoja amejaliwa cha kwake na kwa hakika havinani sana. Slaa anaonekana kama mchokozi, mfukunyuku, mfunua mambo, mtafuta mambo, muanzisha mambo n.k. huku Mashinji anaonekana kama mtulivu zaidi na anayesubiri kila kitu kwa uhakika. Ikiwa viatu vya Dk. Slaa vinamtosha au la ni suala la muda tu kabla wengi hawajajua mbivu na mbichi.

Mashinji anayo faida moja ambayo inaweza kumfanya afanye vizuri kuliko Dk. Slaa, ujana! Nina hakika akiamua atakuwa na uwezo wa kuchapa kazi kwa kasi, nguvu na ufanisi mkubwa akichanganya na kuwajua vijana na kizazi cha sasa.
Changamoto ya pili ambayo itamkabili Mashinji ni namna ya kufanya kazi na Freeman Mbowe. Pamoja na wamba Freeman amekuwa na mchango mkubwa kabisa kwenye uhuishaji wa siasa za upinzani hapa Tanzania, ukweli unabakia kuwa ni kiongozi asiyestahimili mambo mengi yanayosumbua kichwa na ni mfanya maamuzi kwa haraka sana.

Haiba hii ya Mbowe ndiyo imemfanya pia aonekane kama ana nguvu kubwa ndani ya CHADEMA, zisizodhibitika. Watu wengi huamini kuwa Mbowe ana nguvu kubwa ndani ya CHADEMA kiasi kwamba anaweza kufanya lolote lile akiona maslahi ya chama hicho yanachezewa.

Ikiwa ndivyo, Mashinji anayo kazi ya kujifunza namna ya kufanya kazi na Mbowe na hasa mambo ambayo anajua yanaweza kukatiza safari yake kisiasa ili asije kuingia kwenye kundi la wanasiasa walioshindwana na Freeman.

Changamoto ya tatu inayoweza kumkabili Mashinji ni ile dhana ya Wenye chama dhidi ya wageni. Hili litaweza kutokea tu endapo waliodumu ndani ya CHADEMA kwa muda mrefu hawataridhishwa na kupitishwa kwa Mashinji kuwa Katibu Mkuu huku wao wakiachwa. Ikiwa wataanza kumtengenezea “figisu” naamini jungu la kwanza atakalopigwa ni “ugeni wake ndani ya uongozi wa juu wa chama”.

Wanaweza kumtizama kama “wa kuja” na kumzulia mambo mengi ambayo hutokea kwenye vyama vya siasa. Mashinji anayo kazi ya kuwabaini watu wote ambao anahisi wanaweza kumletea michezo hiyo na achukue hatua za kuwa nao karibu na kujua “manung’uniko” yao mapema ili kisiasa ajue namna ya kuyapangua.

Ukiachilia mbali changamoto ya jumla ya vyama vya upinzani kupambana na CCM. Dk. Mashinji atakuwa na jukumu la kipekee la kuimarisha mahusiano ya CHADEMA ndani ya UKAWA na kuvifanya vyama vingine vilivyo ndani ya umoja hiyo vijisikie vimo kwenye umoja muhimu, thabiti na wenye maslahi mapana ya pande zote mbili.

Kwa kiasi kikubwa, mafanikio yatakayozaa matunda kutokana na utendaji wa Mashinji yatategemea pia ushiriki wa chama hicho kwenye UKAWA na kama ilivyo ada ndani ya umoja huo yeye Mashinji ndiye anaweza kujikuta anapewa jukumu la kuwaongoza makatibu wakuu wa vyama vingine kuimarisha sekretariati ya UKAWA. Hii ni changamoto ya kipekee sana ambayo inahitaji mtu ajivue “ukada” wa chama chake ili ayafikie mafanikio na kutimiza matakwa na malengo ya vyama vyote.

HITIMISHO
Dk. Mashinji ni kielelezo tosha cha namna ambavyo vyama vya siasa vya upinzani hapa Tanzania vilivyo na hazina za kutosha za mahitaji ya jamii ya kisasa. Huyu ni kiongozi ambaye atakuwa na uwezo mkubwa wa kuipeleka CHADEMA karibu na vijana na kizazi hiki.

Ni mwanamikakati ambaye anapewa kazi ya kukihuisha chama chake kimikakati ili kifanye kazi ya kujibadilisha na kuondoa taswira zote mbaya ambazo kimekuwa kikielekezewa na malengo makubwa yakiwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kushika dola. Namtakia kila la heri mpiganaji huyu, lakini akumbuke kwamba, “kuwa Katibu Mkuu wa chama kikubwa kama CHADEMA ni kujitoa sadaka isiyorudi nyuma”.
Source juliusmtatiro

No comments: