Na mwandishi wetu
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora inayoendelea mjini Kigoma, imemtia hatiani David Kafulila na kumtaka kulipa gharama kutokana na kukiuka kanuni ya kuwasilisha hati za kiapo mahakamani, zikiwa zimethibitishwa kama Sheria ya Makosa ya Uchaguzi inavyoelekeza.
Hata hivyo, kiwango cha faini anachotakiwa kulipa hakikutajwa. Kosa hilo halikuzuia ushahidi wake kupokewa upya mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo aliyoifungua kupinga ushindi wa Hasna Mwilima (CCM) kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, Kafulila aliyegombea kwa tiketi ya NCCR Mageuzi analalamika kupokwa ushindi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwilima ambaye ni mshtakiwa namba moja wakati msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni washtakiwa namba mbili na tatu.
Jaji wa Mahakama Kuu, Ferdinand Wambali alisema Kafulila aliwekewa pingamizi na mawakili wa utetezi wakimlalamikia kuwasilisha hati ya kiapo iliyokiuka kanuni za uwasilishwaji kwa mujibu wa sheria.
Katika hoja yao mawakili hao waliiomba Mahakama hiyo kutozipokea hati hizo.
Jaji alisema Kafulila hakutekeleza matakwa ya kisheria ambayo yanaagiza anayewasilisha haki za viapo kuhakikisha kuwa zimethibitishwa kabla, kwa ajili ya shahidi kuanza kutoa ushahidi wake.
“Pingamizi la wajibu maombi linakubaliwa kwa upande mmoja, lakini pia linaachwa. Uamuzi wa Mahakama ni kwamba mleta maombi awasilishe upya hati za kiapo mbele ya Mahakama zikiwa zimethibitishwa,” alisema jaji.
“Lakini pia mleta maombi atalazimika kulipa gharama za usumbufu wa kesi kwa wajibu maombi kutokana na shauri kuahirishwa kwa siku mbili mahakamani.” Kufuatia mjadala huo kuwa mkali na mawakili wa kila upande kujenga hoja, jaji aliahirisha kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment