Tuesday, May 31, 2016

DAR BREW YAZINDUA MUONEKANO MPYA WA CHIBUKU SUPER

 Meneja Masoko wa Kiwanda cha Dar Brew, Oscar Shelukindo (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu uzinduzi wa chupa mpya yenye ujazo wa ml 750 za bia aina ya Chibuku. Kulia ni Meneja Mauzo na Usambazaji wa kiwanda hicho, Fredy Kazindogo.
 Meneja Mauzo na Usambazaji wa kiwanda hicho, Fredy Kazindogo (kulia), akizungumza katika uzinduzi huo.
 Ofisa Mauzo wa Kiwanda hicho, Agripina Kusaga (kushoto), akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 Taswira meza kuu. Kutoka kulia ni Ofisa Mauzo, Neema Mvungi, Meneja Mauzo na Usambazaji, Fredy Kazindogo, Meneja Masoko, Oscar Shelukindo na Ofisa Mauzo, Agripina Kusaga.
Mkutano ukiendelea.


Na Dotto Mwaibale

KAMPUNI ya Dar Brew jana ilizindua chupa mpya ya bia ya asili ya Chibuku Super yenye ujazo wa milimita 750, ambayo mtumiaji halazimiki kurudisha chupa pale anapoitumia.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Meneja Masoko wa Dar Brew, Oscar Shelukindo alisema, bia hiyo iliyopo katika chupa nzuri ya plastiki inayovutia, itauzwa kwa bei ya Sh 1,000 tu kwa kila chupa.

“Leo (jana) ni siku ya furaha kubwa sana kwetu Dar Brew na kwa watumiaji wote wa bia, kwani tumefanikiwa kuzindua chupa hii itakayouzwa kwa bei nzuri ya Sh 1,000 tu na kwa ujazo unaotosheleza.

“Bia hii imetengenezwa kwa utaalam wa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa, hivyo tunawahakikishia watumiaji ubora wa hali ya juu,” alisema.

Shelukindo alisema, bia hiyo imetengenezwa kwa kutumia malighafi za hapa nyumbani, ikiwemo nafaka ya mtama ulio bora, hivyo kuna kila  sababu kwa Watanzania kujivunia kilicho chao na kukumbuka asili yao, kwani hii ni bia yao ya asili.

“Chibuku Super ina kilevi cha asilimia 4, kinachokufanya uitumie kwa muda mrefu ukiwa na marafiki, lakini inakupa lishe nzuri kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika nafaka zilizotumika kutengeneza bia hii.”

Naye Meneja Mauzo na Usambazaji wa Dar Brew, Fred Kazindogo alisema, bia hiyo itaanza kupatikana nchi nzima katika baa, maduka makubwa (Super Markets), katika maduka ya jumla na rejareja na sehemu zinazouzwa vileo kuanzia leo.

“Tunatarajia wateja na wapenzi wa bia wataifurahia chupa hii mpya na kwa wauzaji wa jumla, tunaamini watahamasika kuuza Chibuku Super kwani ina faida nzuri na haina usumbufu wa kununua chupa,” alisema.

Kazindogo alisema, ana imani kubwa wapenzi wa bia wataipokea kwa shangwe na wataitumia ili kuonesha wanajali asili yao. 

No comments: