Friday, May 27, 2016

Hotuba ya Zitto Kabwe kuhusu elimu


Watanzania wenye ujuzi wa juu milioni Tatu ifikapo mwaka 2025. Pia Tanzania inahitaji watu wenye ujuzi wa ufundi (kutoka VETA  na Technical Schools) wapatao milioni 7 ifikapo mwaka 2025.

Ni muhimu sana kufungua macho na kufanya maamuzi mahususi kuhusu Elimu. Tunahitaji uwekezaji wa angalau 20% ya Bajeti yetu kwenda kwenye Elimu kwa miaka 10 ijayo ili kuweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye Elimu. Hata hivyo, kipimo cha msingi cha mafanikio katika mfumo wa elimu ni kama watoto wanaotoka kwenye mfumo huo wa Elimu wana maarifa, ujuzi na uwezo kwa ulimwengu watakaoukabili.

Hatuwezi kupata mafanikio haya bila kufumua mfumo wetu wa Elimu, kupanua demokrasia ya utoaji Elimu na kuhakikisha walimu wanapata motisha. Moja ya motisha tunayoweza kupawa Walimu ni kuwalipa vizuri, kuwasimamia vizuri na kuwapa mitihani maalumu kila wakati ili kuwapandisha madaraja.

Napendekeza ‘salary scale ya Walimu’ iwe sawa na angalau nusu ya salary scale ya Wabunge na viwango vya mishahara kati ya Walimu wanaofundisha ngazi yeyote ile iwe sawa kulingana na usawa wa elimu, muda kazini na juhudi ( performance based remunarations).

Najua haya yanaweza kuonekana magumu lakini naamini maneno aliyoyema mwanaharakati wa Elimu Nchini Rakesh Rajani aliyepata kusema “More of the same won’t cut it anymore”. Kama Elimu ndio silaha kubwa ya kuleta maendeleo, ni lazima tufanye tofauti ili kuboresha Elimu.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo  ya Jamii kwamba Taifa liunde Tume ya Wataalamu ili kuweza kutafuta Nyufa za Elimu yetu na kutoa mapendekezo yanayotokana Na ushahidi wa kisayansi. Tuunde Tume ya Elimu sasa ili tuweze kuwa na muda wa kutosha wa kutatua changamoto za Elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, katika pendekezo la kuanzisha Vyuo vya Ufundi kila mkoa natoa maombi maalumu kwa mkoa wa Kigoma kuanzisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji (UjijiInstitute of Technology – UIT). Mji wa Ujiji ni moja ya miji mikongwe nchini ambayo inasinyaa kama sio kufa. Uanzishaji wa Chuo utakaowezesha kudahili angalau wanafunzi 5000 itakuwa ni chachu kubwa ya Maendeleo Mji huu na Tanzania kwa ujumla.
Taasisi ya Teknolojia ya Ujiji itaweza kusaidia sana kuziba mianya ya wataalamu wa katika kwenye sekta ya usafirishaji (Logistics) kwa kuzingatia kuwa Kigoma ni Lango la Magharibi la Taifa letu. Napendekeza kuwa Serikali ilitazame kwa kina ombi hili ili kuweza kuongeza wataalamu wa kati katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninapendekeza pia Serikali itazame upya suala la Sera ya Vitabu ili kuhakikisha kuwa uwekezaji katika uchapishaji unaongezeka nchini. Nadhani ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ubora wa vitabu badala ya yenyewe kuhangaika na kuandika na kuchapisha vitabu. Sera ya Vitabu inazalisha ajira kwenye nchi na inawezesha Watanzania kutafuta fursa kwenye maeneo hayo pia. Wachapishahji wa ndani wanashindwa kukua kwa sababu Serikali imewabana.

Serikali haipaswi kubana inapaswa kuchochea ukuaji wa sekta ya uchapishaji. Vilevile, napendekeza sana tuwekeze kwenye maktaba za kijamii kwenye kata zetu na miji yetu. Maktaba hizi ziwe na vitabu na tuhamasishe watu wenye vitabu kutoa vitabu kwa maktaba hizi. Tujenge Taifa la wasomaji kwa kuhamisha usomaji kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Mheshimiwa Spika, nasisitiza kuwa mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu namna ya kutoa mikopo na kuikusanya yachukuliwe kwa uzito unaostahili. Mikopo isiwe sehemu ya Bajeti ya Wizara badala yake Bodi ipewe fedha moja kwa moja kutoka Hazina ( Direct Transfer ) na mfumo wa malipo udhibitiwe.

Ni lazima tufanye tafiti kuhakikisha kuwa ifikie wakati Bodi ya Mikopo iweze kujiendesha yenyewe kutokana na fedha zinazorejeshwa. Mfumo wa kutumia Credit Reference Bureau na Vitambulisho vya Taifa na hata mobile technology kuhakikisha mikopo inarejeshwa ni mfumo ambao utakuwa na mafanikio makubwa sana.

 Serikali ifanyie kazi pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, nasisitiza pia kuwa pendekezo la Kamati kuanzisha President Magufuli Scholarship Award lianze mara moja. Tuchukue watoto waliofanya vizuri angalau 50 kila mwaka na kuwasambaza kwenye Vyuo Vikuu vikubwa Duniani. Ndani ya Miaka 10 tutakuwa tumetengeneza mamia ya Watanzania wenye uwezo mkubwa kwenye Nyanja zote nchini. Rais atakuwa ameacha jambo kubwa na la kukumbukwa.
Zitto Kabwe Ruyagwa
Mei 27,2016

No comments: