Tuesday, May 31, 2016

UBABE NDANI YA BUNGE WAWAIBUA LHRC-WATAKA WABUNGE KUFUTIWA ADHABU MARA MOJA NA KURUDISHWA BUNGENI

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha Sheria Na haki za binadamu Nchini Tanzania Bi HELLEN KIJO BISIMBA akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es salaam hukusu sakata llinaloendelea Bungeni ambalo limesababisha wabunge takribani saba kufukuzwa ndani ya bunge kwa vipindi Tofauti Tofauti hapo jana

 Wakati sakata la wabunge saba wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania jana kusimamishwa kuingia bungeni kwa vipindi tofauti Kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania LHRC kimelitaka bunge la Tanzania kuwarudisha bungeni wabunge hao mara moja kwani kufanya hivyo ni kuwarudisha nyuma wananchi katika haki zao za kuwakilishwa.


Jana bunge la Tanzania kupitia kwa kamati ya uongozi ya bunge hilo ilitangaza rasmi kuwafungia wabunge saba wa bunge hilo ambao wote ni kutoka vyama vya upinzani kuingia bungeni kwa vipindi tofauti kwa kile kilichotajwa kuwa ni kitendo chao cha kufanya vurugu ndani ya bunge wakati wa sakata la kuwatetea wanafunzi wa UDOM waliotimuliwa chuoni Ghafla na kuzua taharuki nchini.
GELINE FUKO ni mwanasheria wa LHRC akiwa anaeleza mambo kadhaa mbele ya wanahabari muda mfupi uliopita
Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini HELLEN KIJO BISIMBA mbele ya wanahabari ameeleza kuwa kitendo cha bunge kuwasimamisha wabunge ambao wamechaguliwa na wananchi ni kitendo cha kukiuka sheria na haki za msingi za uwakilishi kwa wananchi ambao ndio wapiga kura na ukizingatia kuwa sababu zilizotajwa hazina uzito kulinganisha na adhabu iliyotajwa.


Ameleza kuwa Naibu spika wa bunge hilo ambaye ni mwanamke alitegemewa sana na watanzania kuwatetea watanzania wote hususani maskini lakini kinyume na hivyo kiti chake kimekuwa kikiongoza bunge hilo kibabe tangu lianze kwa awamu hii ya tano jambo ambalo linaleta wasiwasi kama bunge hilo litakuwa na uwezo wa kuisimamia na kuishauri serikali ipasavyo.
Wanahabari kazini
Akizungunzia chanzo cha mgogoro wa jana amesema kuwa kitendo cha serikali kuwatimua wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma bila utaratibu maalum  sio kitendo cha kuungwa mkono na kila mtanzania anayependa haki za watanzania kwani kuwepo kwao chuoni hawakujipeleka bali walipekwa na serikali ambayo sasa imewageuka na kuwatimua.


Ameongeza kuwa kituo hicho kwa hatua za haraka wanaitaka serikali isitishe uamuzi wake wa kuwafukuza wanafunzi wote wa UDOM na badala yake itafute suluhu kwa njia ya Amani na iwaadhibu wale wote watakaobanikia kuhusika na sakata hilo.
Amesema kuwa ni kitendo kisicho cha kiungwana kilichofanywa na Naibu spika kushindwa kujadili swala ambalo linaendelea huku wanafunzi ambao ni Zaidi ya elfu Saba kuwa katika maeneo hatari barabarani na wengine wakiwa hawana hela  ya kujikimu jambo ambalo ni hatari kwao na kumtaka Naibu spika huyo kuwa na utu na kujali maisha ya watoto hao.

Aidha katika upande mwingine kituo hicho kimewapongeza wabunge wote wa bunge la Tanzania ambao jana walionyesha kugushwa na sakata hilo la wanafunzi na kuamua kutoka nje ya bunge kushinikiza bunge kujadili kwa dharura swala hilo bila woga kitendo ambacho kilifanywa na wabunge wa kambi zote za bunge yani wa chama tawala na wale wa upinzani jambo ambalo wamesema linapaswa kuendelezwa kuwatetea wanafunzi hao ambao wanateseka katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma.

Habari hii imeandaliwa na Mwandishi EXAUD MTEI-0712098645

No comments: