Friday, June 24, 2016

ARGENTINA NA CHILE KUVAANA TENA KATIKA FAINALI YA COPA AMERICA KUPITIA STARTIMES




Na Dotto Mwaibale

 Michuano ya kombe la Copa America iliyokuwa ikitimua vumbi nchini Marekani kuanzia Juni 4 na kuonekana moja kwa moja kupitia ving’amuzi vya StarTimes itamalizika siku ya Juni 27 katika fainali itakayozikutanisha tena kwa mara nyingine timu za taifa za Argentina na Chile katika uwanja wa East Rutherford, New Jersey.

Katika fainali ya mwaka jana iliyofanyika Julai 4 timu ya taifa ya Chile ambao ndio walikuwa wenyeji waliweza kutumia vizuri fursa hiyo kwa kutwaa ubingwa baada ya kuwafunga Argentina katika hatua ya mikwaju ya penati.  

Wateja wa StarTimes na watanzania wapenda soka kwa mara ya kwanza mwaka huu wamepata fursa ya kujionea michezo yote moja kwa moja kupitia chaneli za Sports Focus na World Fooball kwa ving’amuzi vyote vya antenna na dishi kwa gharama nafuu kabisa ya kuanzia shilingi 12,000/-

Akizungumzia juu ya hatua ya kombe la Copa America ilipofikia, Makamu wa Rais wa StarTimes Tanzania, Bi. Zuhura Hanif amesema kuwa ilikuwa ni michuano bora na ya kusisimua wateja wao kupata kujionea huku ikipambwa na timu zenye ushindani mkubwa na nyota wengi wa dunia.

“Siku zote StarTimes tumejizatiti katika kuboresha huduma zetu hususani kuwapatia wateja vipindi wanavipendavyo na kuvifurahia. Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele ndivyo tunavyoboresha zaidi kile tunachokiahidi kila siku kwa wateja wetu. Tuliwaahidi kuwaletea vipindi bora vya michezo na hivi ndivyo tunavyotekeleza. Na ningependa kuwatoa hofu kuwa kumalizika kwa michuano hii ni mwanzo wa mambo mazuri zaidi kwani tunatarajia kuwa na michuano mingine ya soka tutakayowaletea watanzania moja kwa moja hivyo wakae mkao wa kula.” Aliongezea Bi. Hanif

“Copa America kwa sasa imefikia hatua nzuri ya fainali ambapo itazikutanisha tena timu za Argentina na Chile kama ilivyokuwa kwa mwaka jana. Mchezo huo wa fainali utatanguliwa na mechi ya kumpata mshindi wa tatu ambao utachezwa alfajiri ya kuamkia Jumamosi ya Juni 25 baina ya Marekani na Colombia. Mchezo huo pia utaonyeshwa moja kwa moja kupitia chaneli zetu za Sports Focus na World Football. Ningependa kutoa wito kwa wateja wetu mbali na kupata burudani hiyo pia wafuatilie kampeni zetu kuhusu michuano hii zinazoendelea kupitia mitandao yetu ya kijamii kama vile facebook na instagram ili waweze kujishindia zawadi kemkem ikiwemo fedha taslimu, tiketi ya ndege kwenda Ujerumani kutazama mechi za Bundesliga msimu ujao pamoja na simu za mkononi za kisasa.” Alimalizia Bi. Hanif

Timu ya taifa ya Argentina imetinga hatua ya fainali baada ya kuibamiza Marekani magoli manne bila ya mujibu huku nahodha na mchezaji nyota Lionel Messi akivunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote. Messi alifikisha magoli 55 moja zaidia ya mchezaji Gabriel Batistuta aliyekuwa akiishikilia rekodi hiyo kwa muda wa miaka 15.

Chile ambao ni mabingwa watetezi nao wameingia hatua hiyo kwa kishindo na kudhihirisha kuwa hawakubahatisha hatua hiyo baada ya kuilaza timu ya Colombia magoli mawili kwa bila kupitia kwa wachezaji wake Charles Aranguiz na Jose Fuenzalida.

Wapenda soka wote ulimwenguni wanatarajia kuona fainali kali na ya aina yake baina ya timu hizo hususani ushindani mkali kutoka kwa kikosi cha Argentina kilichopo kwenye ubora wa hali ya juu kikiongozwa na nyota wake Lionel Messi huku kikiwa na kiu kubwa ya ubingwa kwa takribani muda wa miaka 23.

Pia mashabiki wanasubiria kwa hamu kuona Lionel Messi kama ataweza kuiongoza timu yake kutwaa kombe hilo na pia kuchukua ufungaji bora kwa kumzidi mchezaji wa Chile Eduardo Vargas mwenye magoli sita huku yeye akiwa na matano.


No comments: