RAMBIRAMBI KWA JOHN MABULA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha John Mabula - mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar ya Morogoro inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mbali ya Mtibwa Sugar, taarifa za Mabula ambaye pia amewahi kuchezea Moro United ya Morogoro na Shinyanga Shooting ya Shinyanya kwa mafanikio nafasi ya ulinzi kwa muda mrefu katika timu hizo, aliuawa kwa kuchomwa kisu na mwenzake alipokuwa akiamulia ugomvi huko Kitunda - nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Rais Jamal Malinzi amemwelezea Mabula kuwa ni mchezaji aliyekuwa na uwezo na uadilifu na mchango wake katika soka utabaki katika dhana ya kumbukumbu ya wachezaji mahiri wa Tanzania waliotokea kucheza nafasi ya ulinzi japokuwa ametangulia mbele za haki.
Rais Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa uongozi wa timu ambazo alicheza ambazo ni Mtibwa Sugar, Moro United na Shinyanga Shooting; kadhalika familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki walioguswa na msiba huo wa gwiji huyo aliyepata pia kucheza timu ya taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ ya mwaka 2002-2004.
Rais Malinzi amewaasa wadau wote kuwa watulivu wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wetu Mabula hasa kutokana na mazingira ya kifo. Bwana alitoa, Bwana Ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe. Amina.
MAKUNDI LIGI DARAJA LA KWANZA YAPANGWA
Bodi ya Ligi (TPLB) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza makundi matatu ya timu zitakazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes msimu wa 2016/2017. Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu mara baada ya kukamilisha mchakato wa usajili unaoanza Juni 15, 2016.
Makundi hayo yenye timu nane (8) kwa kila moja, yamegawanywa kwa alama ’A’, ‘B’ na ‘C’.
Kundi A lina timu za:
1 Abajalo ya Dar es Salaam
2 African Sports ya Tanga
3 Ashanti United ya Dar es Salaam
4 Kiluvya United ya Pwani
5 Friends Rangers ya Dar es Salaam
6 Lipuli ya Iringa
7 Mshikamano FC ya Dar es Salaam
8 Polisi Dar ya Dar es Salaam
Kundi B
1 JKT Mlale ya Ruvuma
2 Coastal Union ya Tanga
3 Kimondo FC ya Mbeya
4 Kinondoni Municipal Council ya Dar es Salaam
5 Kurugenzi ya Iringa
6 Mbeya Warriors ya Mbeya
7 Njombe Mji ya Njombe
8 Polisi Morogoro ya Morogoro
Kundi C
1 Alliance Schools ya Mwanza
2 Mgambo Shooting ya Tanga
3 Mvuvumwa FC ya Kigoma
4 Panone FC ya Kilimanjaro
5 Polisi Dodoma ya Dodoma
6 Polisi Mara ya Mara
7 Rhino Rangers ya Tabora
8 Singida United ya Singida
ZAWADI ZA LIGI YA VODACOM KUTOLEWA MWEZI UJAO
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Young Africans SC na timu nyingine zilizoshiriki katika msimu ulioisha wa 2015/2016 zitakabidhiwa zawadi zao mapema mwezi ujao na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amesema kuwa ucheleweshaji wa kutoa zawadi hizo baada ya kumalizika, umetokana na baadhi ya timu zinazoshiriki kwenye mechi za mashindano ya kimataifa kama vile mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuingia kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Tunaomba radhi kwa timu husika, wachezaji na wadau wa soka kwa zoezi hili kuchelewa ila tunawahakikishia kuwa zawadi ziko tayari na zitakabidhiwa mwezi ujao,” alisema Nkurlu.
Pia alishukuru wadau wote waliofanikisha ligi hiyo hadi kufikia mwisho ambapo Young Africans ya jijini Dar es Salaam iliibuka tena bingwa kwa mwaka huu.
“Licha ya changamoto zinazoendeleza kujitokeza katika ligi yapo mafanikio makubwa na ligi hii inazidi kuwa na msisimko mkubwa nchini tunawashukuru wadau wote na tuna imani kuwa itazidi kuwa bora katika siku za usoni,” alisisitiza Nkurlu.
Alisema kuwa Vodacom Tanzania itaendelea kutoa udhamini wa ligi hii hata katika msimu ujao kwa mujibu wa mkataba wake na TFF na aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi hii ikiwemo kuwawezesha wachezaji kunufaika zaidi katika ushiriki wake.
No comments:
Post a Comment