Monday, June 27, 2016

JESHI LA POLISI MKOA WA ILALA LINAMSHIKILIA MTUHUMIWA WA UTAPELI ANAYETUMIA MAJINA YA VIONGOZI


Jeshi la Polisi Mkoa ILala mnamo tarehe 16/06/2016 maeneo ya Mtaa wa Samora lilifanikiwa kumkamata mtu mmoja anayefahamika kwa jina la IMAROCK  PAULA  RUTASHOBYA@ISSA MOHAMED JIUNGA  kwa tuhuma za kujipatia fedha  kwa njia ya udanganifu wa kutumia  jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mheshimiwa PAUL MAKONDA.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kumpigia simu mkurugenzi  wa kampuni ya JONES LOGISTICS LTD ndugu JAMES  RODRICK LUPONDO na kujitambulisha kwakwe kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa lengo la kumsaidia kijana ambaye amepata SCHOLARSHIP lakini anahitaji achangie asilimia 30% ya  gharama za chuo kilichoko nchini Ufilipino baada ya kupata ufadhili wa asilimia 70%.
Aidha katika maongezi yao mtuhumiwa huyo alimueleza ndugu JAMES kuwa kuna namna tofauti za kutuma fedha hizo za msaada ikiwa ni pamoja na kuweka kwenye akaunti KENYA, ECO BANK Dar es salaam Tanzania au kutoa pesa hizo taslimu huku akimtajia namba ya simu ya kijana anayehitaji msaada kuwa ni  0717 338473 na kusema kuwa huyo kijana atafika ofisini kwakwe baada ya masaa mawili  akiwa na nyaraka zote za fursa ya hayo masomo pamoja na akaunti namba za benki hizo alizozitaja.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linatoa onyo kali kwa watu wote wenye tabia ya namna hii ya kutumia majina ya viongozi wakubwa wa serikali kwa lengo la kujipatia fedha, aidha wananchi wanatakiwa kuwa makini wanapopigiwa simu na watu wasiowafahamu na kujitambulisha kwao kwa majina ya viongozi.

Mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa ili kuwatambua watu wengine anaoshirikiana nao katika utapeli wa namna hiyo,upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakani kwa hatua zaidi.



No comments: