Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa kwa miaka mitatu iliyopita katika kusikiliza na kuamua mashauri yaliyowasilishwa kwenye ngazi mbalimbali za mahakama nchini.
Hayo yamesemwa wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipowaapisha Jaji Shabani Ally Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji Ferdinand Wambali kuwa Jaji Kiongozi, Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza baada ya uapisho huo Jaji Kiongozi, Wambali alibainisha mafanikio hayo ya mahakama na kuahidi kuongeza kasi ya kutekeleza majukumu ya kusikiliza na kuamua mashauri yanaypowasilishwa mahakamani.
Alisema moja ya kazi kubwa ya mahakama ni kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
“Hakuna shaka kwamba zipo changamoto nyingi kuhusiana na uendeshaji wa mashauri lakini pia tumepiga hatua kubwa kwa miaka mitatu iliyopita katika usikilizaji wa mashauri” alisema Jaji Wambali na kuongeza:
“Kwa hiyo kasi ambayo imekuwa ipo mimi naahidi kufanya kazi kwa bidii na nguvu zote kwa jinsi Mwenyezi Mungu anavyonijalia kuhakikisha kwamba tunaendeleza pale ambapo wenzangu wamafikia”.
Jaji Wambali alifafanua kuwa mahakama inayo timu nzuri ya majaji na anaamini atashirikiana kwa dhati na watumishi wengine kuhakikisha kwamba anatatua matatizo ya wananchi.
“Lakini kama mnavyofahamu mahakama iko kwenye maboresho mengi na hasa kuhakikisha mahakama inakuwa karibu na wananchi na mimi nitalisimamia hilo kwamba mahakama isiwe chombo kinachoogopwa na wananchi bali kiwe chombo ambacho kinafikiwa na wananchi kwa karibu” alieleza Jaji Wambali.
Alisema mambo manne ya msingi aliyoyaapa ndiyo yatakamuongoza kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu bila woga, upendeleo, chuki wala huba.
“Hayo ndio mambo makubwa manne ambayo jaji yeyote yanamuongoza katika kutoa haki kwa hiyo hilo ndilo linaloahidi kulitekeleza kwa nguvu zangu zote” alisema.
Akizungumzia kesi kukaa muda mrefu bila kuamuliza, Jaji Wambali alisema sheria inataka kesi ya madai isikae zaidi ya miaka miwili na mahakama imejipangia muda wa miezi 18 wa kusikiliza kesi hizo, hata hivyo ameomba ushirikiano kwa wadau ili kufanikisha lengo hilo.
“Ndio maana nimesema ni lazima tushirikiano na wadau wote kwani wakati mwingine kesi zinaahirishwa kwa sababu ya wadau.Lakini katika miaka hii miwili iliyopita sasa wananchi wanatambua kwamba kesi zinaamuliwa kwa wingi sana kwa sababu kila Jaji, hakimu amepangiwa kesi za kusikiliza kwa mwaka” alisema Jaji Wambali.
Alisema vipo vituo ambavyo mahakimu na majaji wanamaliza kesi na wanatakiwa kwenda kwenye vituo vingine kusaidia, hivyo watajitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba wanalitekeleza hilo kwa nguvu zote.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama ya Rufani,Jaji Shabani Ally Lila, alisema kuwa anakwenda Mahakama ya Rufani kuongeza nguvu kwenye kusikiliza na kuamua mashauri.
“Najua Mahakama ya Rufani inashughulika na kusikiliza na kuamua mashauri, kwa hiyo tutashirikiana na wenzangu kuona namna ambavyo tutakabiliana na mashauri ambayo sasa hivi yana muda mrefu mahakamani” alisema Jaji Lila.
|
Friday, June 10, 2016
Rais Dkt John Pombe Magufuli awaapisha Majaji wawili June 10, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment