Saturday, July 30, 2016

SKY SPORTS YAUNGANA NA STARTIMES KUONYESHA LIGI YA CHINA



Na Dotto Mwaibale

Kituo cha matangazo ya luninga cha Sky Sports cha nchini Uingereza katikati ya wiki hii kilisaini mkataba mnono wa kuonyesha moja kwa moja ligi kuu ya China kwa misimu mitatu ijayo ambayo pia kwa Tanzania inaonekana kupitia visimbuzi vya StarTimes.

Sky Sports wameamua kuanza kuionyesha ligi hiyo baada ya kuvutiwa na jitihada kubwa zinazofanywa na China katika kukuza soka la nchini mwao hususani kupambana sambamba na vilabu vikubwa vya barani Ulaya katika kusajili wachezaji nyota kutokea ligi hiyo.

Ligi hiyo imeanza kujizolea umaarufu na kuvuta hisia za watu baada ya kuona majina ya wachezaji wakubwa yakielekea huko kama vile Ramires aliyetokea Chelsea, Gervinho aliyewahi kuchezea Arsenal, Obafemi Martins aliyechezea Newcastle United na hivi karibuni nyota wa Italia Graziano Pelle aliyetokea Southampton na kujiunga na Shandong Luneng.

Akizungumzia juu ya taarifa hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu wa StarTimes Tanzania,  Lanfang Liao ameelezea kuwa hiyo ni habari njema kwetu sisi pia kwani mapema mwaka huu tuliingia makubaliano ya kuitangaza ligi hiyo pia baada ya kuona mbali kuwa itakuja kuwa maarufu na hilo linaanza kujidhihirisha.

“Ukiwa unazungumzia ligi ambazo zinakua kwa kasi duniani kwa sasa hutoacha kuizungumzia ligi kuu ya nchini China au maarufu kama ‘Chinese Super Cup’. Na hii ni kutokana na ushindani uliopo hivi sasa unaopelekwa na wachezaji pamoja na makocha wazuri katika soka ukiachilia mbali malipo makubwa wanayoyapokea ambayo yanakwenda sambasamba na vilabu vikubwa vya barani Ulaya. Mashabiki wa soka hivi sasa wanaweza kutazama mechi za ligi hiyo na kuziona sura ambazo awali walikwishaziona barani Ulaya kama vile Graziano Pelle, Ramires, Gervinho, Hulk, Asamoah Gyan, Jackson Martinez, Ezequiel Lavezzi na wengineo wengi.” Alifafanua  Liao

“StarTimes kadiri siku zinavyokwenda mbele ndivyo tunazidi kuboresha zaidi huduma zetu hususani ligi mbalimbali za soka kwani tunatambua watanzania ni wapenzi wakubwa. Na kwa kuwa na wigo mpana wa mashindano mbalimbali kunawafanya waweze kufurahia zaidi huduma zetu. Ligi ya China kwa sasa ni ligi kubwa duniani na ndiyo maana Sky Sports wameamua kuinonesha barani Ulaya huku kwa sisi Tanzania na Afrika kwa ujumla ni kupitia visimbuzi vyetu pekee unaweza kutazama mechi zote moja kwa moja.” Alihitisha Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo ya matangazo ya dijitali nchini

Baada ya kusaini makubaliano hayo kwa mara ya kwanza kabisa Sky Sports wataingia mzigoni kuanza kuonyesha mechi za ligi hiyo siku ya Jumamosi ya Julai 30, 2016 ambapo timu za Shanghai Greenland Shenhua itakuwa kiburuani kuwakabili Jiangsu Suning FC (saa 8:35 mchana) na siku ya Jumapili, Julai 31 timu ya Guangzhou R&F inayonolewa na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza, Sven Goran Eriksson kumenyana na Shanghai SIPG (saa 8:35 mchana).

Mechi hizo zote kwa hapa nchini Tanzania zitaonekana moja kwa moja kwenye visimbuzi vya StarTimes kupitia chaneli za Sports Focus na World Football.

No comments: