Monday, August 8, 2016

Sikusoma High School na Ndugu Juma Mwaka" Dk. Kigwangalla

Baada ya sakata la Tabibu Juma Mwaka la kutakiwa kujisalimisha mikononi mwa Jeshi la Polisi kutolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamisi Kigwangalla kwa kile kukiuka taratibu za ufanyaji wa shughuli za tiba mbadala na tiba asili, na baadae kuwapo kwa habari zilizoonea kwa mitandao ya kijamii kuwa Naibu Waziri huyo na Tabibu Mwaka kuwa wana mambo yao binafsi, hatmaye leo Agosti 8.2016, Dk. Kigwangalla ametoa taarifa ya ufafanuzi wa jambo hilo.
Dk.-Juma-MwakaTabibu Juma Mwaka
Soma hapa chini taarifa ya Dk. Kigwangalla.
Kuna baadhi ya magazeti na mitandao imekuwa ikiandika kuwa Dkt. Kigwangalla amesoma high school na aliyekuwa 'Tabibu', Ndg. Juma Mwaka, shule ya Kigoma Sekondari na kwamba walikuwa marafiki; hizi ni habari za uongo, za kupika zenye kupotosha ukweli ili kuwaaminisha watu kuwa 'wanajuana' na pengine wana ugomvi 'binafsi'.
Nimekuwa nikimpuuza kwa sababu sikuwa na haitotokea nikawa na nia mbaya dhidi ya mtanzania mwenzangu yeyote kwa sababu tu mimi nina dhamana ya uongozi. Sinaga tabia hiyo.


Uongo ukirudiwa rudiwa hubadilika na kuwa ukweli. Leo nimeamua, hapa chini, kukanusha ili watanzania pia mumpuuze, tuendelee kuimarisha huduma za tiba asili na tiba mbadala kutoka kwa matabibu wa kweli wanaofuata taratibu na siyo wasanii kama huyu. Uongo ama uzushi dhidi yangu mimi binafsi kamwe hautonirudisha nyuma mimi kama mtumishi wa umma. Lazima ifike mahali tujenge nchi ya watu 'serious' wanaofuata Sheria, Kanuni na Taratibu. Wanaoheshimu Serikali. Kwenye Afya za watanzania hatuwezi kuvumilia usanii, lazima tuwalinde walaji. Hili ni jukumu tulilopewa na Mhe. Rais. Tutasimamia Sheria ipasavyo. Hatutolegeza hata kidogo.

1. Sikusoma 'high school' Kigoma Sekondari. Nimesoma O'level (form I - IV) Kigoma Sekondari. High School nilisoma Shinyanga Sekondari. Sikumbuki kusoma katika shule zote hizi mbili na mtu mwenye Jina Hilo. Kama alisoma Kigoma Sekondari labda mbele yangu ama nyuma yangu. Pia kipindi nasoma Kigoma Sekondari, hakukuwa na 'high school'.
2. Ndg. Juma Mwaka hajawahi kuwa rafiki wala adui yangu. Sina ugomvi binafsi. Nafanya kazi ya kusimamia Sheria ya tiba asili na tiba mbadala ipasavyo.

3. Naithamini tiba asili na tiba mbadala na Ndiyo maana nimeongoza Wizara ya Afya kufanya Mapinduzi makubwa kwenye eneo hili, ikiwemo kuweka utaratibu mzuri na rahisi zaidi wa kusajili watoa huduma, dawa zao, mazingira wanapotunzia dawa, wasaidizi wao, viwanda vyao, na pia kuweka mikakati ya uanzishwaji wa viwanda vya dawa za tiba asili na tiba mbadala sambamba na kufanyia utafiti dawa zao na kudhibiti ubora wa dawa zenyewe na dozi wanazowapa wateja.

4. Muulizeni Ndg. Juma Mwaka anaposema ana ugomvi 'binafsi' na mimi, anamaanisha nini, ugomvi upi? Juu ya nini? Awape taarifa kamili. Mimi Sina ugomvi naye. Kwanza sikuwahi kumjua kabla ya ziara yangu ya kikazi pale Foreplan, ntakuwaje na ugomvi na mtu nisiyemjua? Si utakuwa ujuha huo?

5. Mnaofuatilia suala hili mtakeni Ndg. Juma Mwaka awape majibu ya Msingi ya hoja za wakaguzi kutoka Wizara ya Afya. Mimi nilikuwa msimamizi nikiwapa nguvu wataalam wafanye kazi yao. Wataalamu walikuwepo, nao ana ugomvi nao 'binafsi'? Mwambieni awajibu kama dawa za tiba ya kisasa kukutwa kwenye eneo lake la kazi ilikuwa halali? Alikuwa na vibali vya kutunza zaidi ya maboksi 200 ya dawa? Alikuwa na vibali vya kutunza zaidi ya magunia 10 ya dawa za tiba asili na tiba mbadala baada ya kufutiwa usajili? Alikuwa na uhalali wa kuendelea kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa wateja wake wafuate dawa pale ili wasikatishe dozi? Tena kinyume na katazo la Baraza la tiba asili na tiba mbadala! Yeye yuko juu ya Serikali? Yuko juu ya Sheria? Ama anadhani anaweza kuidhihaki na kuiogofya Serikali?

6. Baada ya ziara yangu ya December 2015, ambapo sikutoa maelekezo ya kumfungia wala kumfutia kibali, niliwaelekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala kuwa wawaite wawaelekeze matabibu wote wafuate Sheria, kanuni na taratibu. Waliitwa. Wakaelekezwa. Waungwana wakatii. Yeye hakutii, wakamfuta. Baada ya kufutiwa usajili, akaendelea kujitangaza na kutoa huduma, yeye ni nani?

7. Kufanya haya ni kuvunja sheria za nchi. Na makosa haya yana adhabu zake. Sisi kama Serikali tumeagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Serikali ina mkono mrefu, itamkamata. Itamtia nguvuni na atafikishwa mahakamani. Ataenda kujitetea huko kuwa ana 'ugomvi binafsi' na Naibu Waziri Kigwangalla!
Mwisho, aende akafuatilie kisa cha mfanyabiashara wa kigiriki aliyesema ameiweka Serikali mfukoni - Mwalimu Nyerere alimfanya nini!
Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB.
dk kigwangallaDkt. Hamisi Kigwangalla, (MB) Nzega Vijijini.

No comments: