Friday, August 12, 2016

WACOMORO KUWAAMUA SERENGETI BOYS, AFRIKA KUSINI


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limemteua Noiret Jim Bacari wa Comoro kuwa mwamuzi wa kati katika mchezo wa marudiano utakaozikutanisha timu za taifa za vijana za Serengeti Boys ya Tanzania na Amajimbos ya Afrika Kusini, utakaofanyika Agosti 21, 2016 Kwenye Uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala - nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAF iliyofika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) mapema wiki hii, waamuzi wasaidizi pia wanatoka Comoro. Waamuzi hao ambao ni washika vibendera ni Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.


Jumamosi iliyopita, ikicheza mbele ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kadhalika Naibu Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Rosemary Chambe Jairo, timu ya soka ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys ilitoka sare ya 1-1 na Afrika Kusini.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Dobsonville ulioko Soweto, Mji ulioko Kusini – Magharibi mwa jiji la Johannesburg, mabao yote yalipatikana kipindi cha pili yakiwa ni ya penalti kwa kila upande. Afrika Kusini ndio walioanza kupata penalti katika dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.
Penalti ya Afrika Kusini ilitokana na mmoja wa mabeki wa Serengeti Boys kumfanyia madhambi Linamandla Mchilizeli wa Amajimbos ndani ya eneo la hatari wakati ile ya Serengeti Boys ilitoakana na beki Luke Donn wa Amajimbos kunawa mpira eneo la hatari. Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa, William Koto kutoka Lesotho.
Itakumbukwa kwamba Afrika Kusini ilianza kwa kasi dakika 10 za mwanzo wa mchezo huo, ilipotea dakika zote 30 za kipindi cha kwanza ambao kukosa bahati na umakini kidogo tu kwa nyota wa Serengeti Boys kulisababisha kukosa mabao matano yakiwamo mawili yaliyogonga mwamba hivyo kuwatia hasira Serengeti Boys ambao walionyesha kuwa na njaa ya mabao.
Kubanwa katika kipindi cha kwanza, kulisababisha Kocha Mkuu wa Amajimbos kufanya mabadiliko ya wachezaji wote watatu kipindi cha pili, wakati Bakari Shime kwa upande wake alimpumzisha Ibrahim na nafasi yake kuchukuliwa na Muhsin ambaye alisaidia kuendedlea kuwabana Afrika Kusini waliokjuwa wanawategemea nyota kama na Mswati Mavuso na Lethabo Mazibuko.
Shukrani za pekee zinaweza kwenda kwa Kipa Ramadhani Kabwili aliyeokoa hatari nyingi ikiwamo mpira uliokuwa unakwenda golini uliotokana na adhabu ndogo. Kadhalika Msengi aliyekuwa nyota wa mchezo huo akimiliki vema idarta ya ulinzi akishirikiaana nDickson Job.
Shime maarufu kama Mchawi Mweusi alisema: “Nashukuru kwa matokeo . Si mabaya kwangu. Tunarudi nyumbani kujipanga. Afrika Kusini ilikuwa inanitia hofu ndio maana nilisema mechi itakuwa ngumu.”
Kwa upande wake, Naibu Balozi Rosemary alisema: “Ahsanteni vijana (Serengeti Boys) kwa kulinda heshima yangu,” wakati Malinzi alisema: “Sina mengi. Mkiwafunga Afrika Kusini Agosti 21, 2016 kambi inapigwa tena nje ya nchi. Sijui ni nchi gani, lakini mtakwenda kujiandaa nje ya nchi.”

No comments: