Friday, September 9, 2016

BAYERN UGENINI KUVAANA NA SCHALKE 04 IJUMAA HII






Na Dotto Mwaibale

BAADA ya kufungua pazia la ligi ya Ujerumani Bundesliga kwa ushindi wa magoli 6-0 dhidi 
ya Werder Bremen, Bayern Munich watakuwa ugenini Ijumaa hii kuvaana na Schalke 04 mchezo utakaoonekana moja kwa moja kupitia visimbuzi vya StarTimes


Katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika dimba la Allianz Arena, Bayern walianza kwa kishindo mbio za kuunyakua tena ubingwa wa ligi hiyo kwa mchezo waliokuwa wakicheza kwa kujiamini kabisa. 

Mshambuliaji hatari wa Bayern, Roberto Lewandoski, alifunga magoli matatu na kushika usukani wa ufungaji wa magoli huku akifukuziwa kwa karibu na muafrika Pierre Emerick Aubameyang ambaye naye alitupia magoli mawili wakati timu yake ya Borrusia Dortmund ilipoilaza 2-1 Mainz 05.

Akizungumza Dar es Salaam leo kuhusu msimu mpya wa ligi hiyo ambayo inaonekana kupitia visimbuzi vya StarTimes pekee, Makamu wa Rais wa kampuni ya StarTimes Tanzania, Zuhura Hanif amebainisha kuwa hii ni fursa nyingine tena kwa wateja wao na watanzania wote kwa ujumla kufurahia mechi zote moja kwa kupitia chaneli mahususi za michezo kama vile SPORT FOCUS, SPORT ARENA, WORLD 
FOOTBALL, SPORT PREMIUM na SPORT LIFE kwa gharama nafuu kabisa ambazo kila mtu anaweza kumudu.

“Ningependa kuchukua fursa hii kuwafahamisha wateja wetu na watanzania kwa ujumla kuwa msimu wa ligi kuu ya Ujerumani msimu wa mwaka 2016/2017 maarufu kama Bundesliga umerudi tena. 

Kama kawaida yetu mechi zote tutazionyesha moja kwa moja kupitia chaneli tano kwa msimu wote ambapo tayari pazia lilishafunguliwa Agosti 26 na kushudia mabingwa watetezi Bayern Munich ikiibuka na ushindi mnono wa magoli 6 bila ya majibu dhidi ya Werder Bremen.” Alisema, Hanif

“Ninaamini huu utakuwa ni msimu mwingine tena wa kufurahia na kupata msisimko wa ligi hii ambayo inazidi kujizolea umaarufu mkubwa barani Afrika ambapo tunawakilishwa vema na mchezaji kutoka Gabon, Pierre Emerick Aubameyang. 

Na StarTimes kama ndio wenye haki miliki pekee ya kuionyesha ligi hiyo tutahakikisha 
kila mtanzania anapata fursa ya kuitazama na kufurahia. Mchezaji huyo ameingia kwenye historia ya soka la Ujerumani kwa kuwa muafrika wa kwanza kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi ya Bundesliga kwa msimu wa 2015/16 na kuingia kwenye kikosi cha ligi hiyo cha mwaka. 

Hili ni jambo la kujivunia kwetu sisi waafrika kwamba soka letu linathaminiwa na vipaji 
vyetu kuonekana. Na ninaamini siku za usoni tutawaona watanzania wakipenya na 
kufikia viwango hivyo.” Aliongezea, Hanif

Mbali na mechi kati ya Schalke 04 na Bayern Munich itakayoonekana kupitia chaneli ya World Football siku ya Ijumaa saa 3:30 usiku, pia siku za Jumamosi na Jumapili kutakuwa na michezo mingine itakayopigwa katika viwanja tofauti.

Siku ya Jumamosi kutakuwa na mechi zifuatazo: Bayer Leverkusen na Hamburger SV (saa 10:30 jioni, World Football), Darmstad na Eintracht Frankfurt (saa 10:30 jioni, Sports Premium), Freiburg na Borussia Moenchengladbach  (saa 10:30 jioni, Sports Arena), Ingolstadt na Hertha Berlin (saa 10:30 jioni, Sports Life), Wolfsburg na FC Cologne (saa 10:30 jioni, Sports Premium) na RasenBallsport Leipzig na Borussia Dortmund (saa 1:30 usiku, Sports Premium).

Na siku ya Jumapili wikiendi itaisha kwa mechi zifuatazo: Werder Bremen na Augsburg (saa 10:30 jioni, World Football) na Mainz 05 na Hoffenheim (saa 12:30 jioni, Sports Life).  “StarTimes siku zote inajitahidi kuhakikisha inawapatia wateja wake maudhui bora ya michezo hususani mpira wa miguu. Mbali na Bundesliga pia liga ya Italia nayo inaonekana moja kwa moja na pekee kupitia 
visimbuzi vyetu na mwishoni mwa wiki hii kutakuwa na michezo mbalimbali ikiendelea 
ambapo vilabu vikubwa kama vile Juventus, SSC Napoili, AC Milan, Inter Milan, AS Roma na Fiorentina vitakuwa vikimenyana. 

Ningependa niwakumbushe kuwa mechi zote hizi zinaonekana kwa ubora wa hali ya juu kabisa na kwa gharama nafuu kabisa za vifurushi vya mwezi kwa kuanzia malipo ya shilingi 12,000 tu.” Alisema, Hanif


No comments: