Meneja wa kiwanda cha kubangua korosho cha Amama Farms Limited,Abdulrahman Sinani akimpa makamu wa rais maelekezo juu ya ufanyaji kazi wa kiwanda hicho hivi karibuni alipokitembelea. |
Tandahimba.Wakati serikali ikidhamiria kujenga viwanda vya kubangua korosho ili kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi,uongozi wa kiwanda pekee kinachobangua korosho kwa sasa cha Amama farms Ltd kilichopo wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara umesema utafunga kiwanda hicho kutokana na kuzuiliwa kununua korosho .
Kiwanda hicho ambacho kinawafanyakazi zaidi ya 230 na kwa mwaka kinabangua zaidi ya tani 1800 kimekuwa na utaratibu wa kununua korosho kupitia Amcos lakini kwa msimu huu imekuwa tofauti ambapo kimetakiwa kununua katika minada itakayotangazwa na serikali.
Akizungumza meneja wa kiwanda hicho Abdulrahman Sinani amesema kiwanda hicho kimeshindwa kufanya kazi kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu hali ambayo inadhorotesha utendaji kazi wake na badala yake ni bora kukifunga na kwenda kufungua katika nchi zingine zinazolima korosho.
"Upatikanaji wa korosho umekuwa mgumu kwasababu awali tulikuwa tunaingia mkataba na Amcos kupitia bei dira iliyopangwa na kuongeza Sh 50 wakati tukisubiri bonus,"alisema Sinani na kuongeza
"Suala hili limewahi kutokea na sasa hivi limejitokeza tena kwahiyo mmiliki anaona ni bora kiwanda kifungwe,"alisema Sinani
Wafanyakazi zaidi ya 230 ambao wanafanya kazi katika kiwanda hicho wamesema endapo kitafungwa utawasababishia kuyumba kiuchumi.
Mussa Bakari mfanyakazi Kiwanda cha Amama Farms Ltd alisema Tunamwomba mmiliki aache nia ya kukifunga kiwanda na badala yake wakutane na uongozi kuona ni kwa namna gani wanapata mzigo kwani sasa hivi tuna mwezi mmoja na nusu hatujafanya kazi, "alisema Bakari
Amina Ismail Mfanyakazi Kiwanda cha Amama Farms Ltd alisema ," Wengi tunategemea kiwanda hiki, Mtwara kilikuwepo kiwanda cha Olam nacho kikafungwa tukahamia huku sasa hiki nacho kikifungwa tutaathirika sana, "alisema Ismail
Akizungumzia juu ya taarifa za kufungwa kwa kiwanda hicho mkuu wa wilaya ya Tandahimba Sebastian Waryuba amesema bado hajapata taarifa hizo na kuwataka kuwa wavumilivu.
"Nikipata taarifa rasmi nitakuwa na la kusema , lakini serikali ina utaratibu wake cha msingi wavumilie na kama wana nia hiyo waache na wajifunze kufuata utaratibu kwani nia ya serikali ni kuona mkulima anapata bei nzuri,"alisema Waryuba
No comments:
Post a Comment