Wednesday, October 19, 2016

Nimekuandalia Report Nzima ya Wanawake waliopanda mlima Kilimanjaro kusimika Madai ya wanawake wa Afrika juu ya haki ya umiliki wa ardhi


Hatimaye baadhi ya wanawake waliopanda mlima kilimanjaro kusimika madai ya wanawake wa afrika juu ya haki ya umiliki wa ardhi wameeleza maswala kadhaa yaliyojitokeza katika zoezi hili ambalo pia lilifwatiwa na kongamano kubwa la ardhi kwa wanawake wa Afrika lililojulikana kama Wazo la Kilimanjaro kongamano ambalo lilifanyika mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na takribani wanawake 500 kutoka nchi 22 barani Africa.

Wakizngumza na wanahabari mapema leo Jijini Dar es salaam wanawake wa Tanzania ambao walipata nafasi ya kushiriki kupanda mlima Kilimanjaro na kushiriki kongamano hilo wameleza kuwa changamoto za ardhi ambazo zinawakabili wanawale wa Tanzania ndizo zinazowakabili wanawake wa Africa nzima jambo ambalo liligundulika katika kongamano hilo.
Judith Severin ambaye ni msichana  aliyeshiriki kupanda mlima Kilimanjaro akisoma Tamko Leo kwa niaba ya wanawake hao.

Akisoma tamko kwa niaba ya wanawake hao Judith Severin ambaye ni msichana ambaye alishiriki kupanda mlima amesema kuwa changamato kama haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake,urithi wa ardhi kwa wanawake,na utumiaji wa ardhi ni jambo ambalo limekuwa changamoto kwa mataifa mengi afrika kutokana na shughuda mbalimbali walizozipata katika kongamano hilo ambapo wameomba serikali kurekebisha baadhi ya sharia za ardhi ili ziweze kumpa nafasi mwanamke ya kumiliki ardhi na kuitumia katika uzalishaji.
SOMA KWA UNDANI TAMKO LA WANAWAKE HAO HAPA----

SAUTI YA WANAWAKE WA AFRIKA TOKA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO OKTOBA 2016.

Ardhi ni rasilimali muhimu na ni kichocheo kikuu katika maendeleo ya uchumi inayochangia takribani 10% ya pato la Taifa kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya 75% ya watanzania na kati yao zaidi ya 50% ni wanawake. Licha ya Sera ya Taifa ya Ardhi 1995 pamoja na Sheria za Ardhi Na.4 na Na.5 za mwaka 1999 kuweka usawa kati ya wanawake na wanaume kumiliki ardhi, nafasi ya wanawake  katika kupata, kutumia, kudhibiti na kumiliki ardhi na rasilimali zingine bado hairidhishi.  Wakati huo huo, wanawake wanakadiriwa kuchangia asilimia 60 - 80% ya uzalishaji wa chakula, na ndio hasa wamekuwa wakilisha familia, taifa hususani kwa nchi nyingi za Afrika.

Mkurugenzi wa TGNP Bi Lilian Liund Akieleza machache kuhusu Safari hiyo

Kwa kutambua changamoto zinazoendelea kuwapata Wanawake wa Afrika katika suala zima la upatikanaji, umiliki na utumiaji wa ardhi na rasilimali, na kwa kuzingatia kufanana kwa kiasi kikubwa kwa changamoto hizo katika ukanda wote wa Afrika,  mashirika ya ActionAid Tanzania, TGNP Mtandao kwa kushirikiana na International Land Coalition, Wildaf,  na Institute for Poverty, land and Agrarian Studies (PLAAS) waliwezesha  Kongamano  la Ardhi kwa Wanawake wa Afrika, linalojulikana kama wazo la Kilimanjaro  (“Kilimanjaro Initiative”) lililofanyika huko Arusha kuanzia  13-16 oktoba  2016. Kongamano hili limefanikiwa kuleta sauti za wanawake wa Afrika pamoja ambapo tulikubaliana kwa pamoja  ili kuwasilisha maazimio yetu kikanda  katika kutetea na kulinda haki ya ardhi na kuleta mabadiliko yenye kuchochea maendeleo ya wanawake wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania. Tunaamini kwamba wanawake ni Zaidi ya 50% ya wananchi wote wa bara la AFRIKA, iwapo watashiriki kikamilifu katika maendeleo hakika Afrika itasonga mbele.

Takribani Wanawake 500 kutoka nchi 22 za       Afrika walihudhuria  kongamano hilo  ambapo kati yao  wanwake 30 kutoka nchi hizo  walipanda Mlima Kilimanjaro kwaajili ya kusimika madai ya Wanawake kuhusu umiliki wa ardhi.  Kati ya hao watanzania walikuwa saba, kati yao wanne  waliibuka kidedea wakafika kwenye kileleni  cha mwisho cha uhuru peak. Madai yetu haya pia yalipokelewa na viongozi wa nchi husika ambako kwa nchi yetu tunapenda kushukuru kipekee Wizara yetu ya Afya, Jinsia, Maendeleo na Jamii, Wazee na Watoto, Wizara ya Sheria na Mambo ya  Katiba, Wizara ya Ardhi na Makazi pamoja na Wizara ya Utalii na Maliasili ambao walishirikiana nasi tangu tulipokutana kama wanawake wa Tanzania kule mkoani Morogoro mwezi Septemba mwaka huu na katika kusanyiko la kitaifa hapa Dar es Salaam tarehe 12 Oktoba 2016 na hatimaye katika kongamano lililofanyika kule Arusha.

Aidha pamoja na viongozi wa serikali za Tanzania walioshiriki, madai haya pia yalikabidhiwa kwa viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU)  ambapo Mwakilishi wa Mwenyekiti wa AU Bi.Ouriatou Dinfaka alipokea. Mwenyekiti wa AU mama Zuma ameahidi kuhakikisha maazimio hayo yanaingizwa katika michakato ya maendeleo katika Ngazi ya AU.

Baada ya kutolewa kwa madai haya kwa serikali yetu pamoja na kwamba AU iyatafayia kazi, Tanzania tunategemea kwamba:

·        Mapitio ya sera ya ardhi ya mwaka 1995, sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, mchakato wa Katiba Mpya ni fursa muhimu ya masuala ya wamawake  kumilikishwa ardhi kuingizwa.
·        Muswada wa sharia wa  Jinsia na Maendeleo wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) unaojadiliwa kwa  sasa ukipita utakuwa nyenzo muhimu kwa nchi wanachama kuhakikisha suala la Jinsia linatekelezwa kikamilifu kwenye ardhi.
·        Nchi yetu ifanyie kazi maazimio mbalimbali  ya kimataifa yanayozitaka kuzingatia usawa wa Kijinsia katika mipango, sera na sheria zake.
·        Serikali ihakikishe badala ya Wanawake kuendelea kuwa watumiaji na wazalishaji kupitia ardhi, sasa wamilikishwe kikamilifu.
·        Serikali yetu inapotaka kuingia kwenye uchumi wa viwanda, itambue kwamba ardhi ndio rasilimali muhimu kwenye viwanda, na kama tunataka Wanawake wanufaike na uchumi huo ni lazima wamilikishwe ardhi

Imetolewa na wanawake waliopanda Mlima Kilimanjaro 
Kusimika madai ya wanawake wa Afrika juu ya  
haki ya umiliki wa ardhi. 
 
Imesainiwa na 
 
.................................
Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji  
TGNP Mtandao, 
Kwa niaba ya Wakurugenzi wa:
 
1.     AATZ                       ..........................................
 
2.     TAMWA                  ...........................................
 
3.     WILDAF                  ...........................................
 
4.     TAWLA                   ...........................................
 
5.     Oxfam                      ...........................................

No comments: