Tuesday, October 18, 2016

SAKATA LA BILLCANAS YA MBOWE NA NHC,MAHAKAMA IMEAMUA HAYA LEO

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imetupilia mbali maombi ya Mfanyabiashara na Mwanasiasa, Freeman Mbowe, kutaka kurudishwa kwenye jengo la Bilicanas, baada ya kuondolewa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa kudaiwa kodi ya Shilingi bilioni 1.3.

Akitoa uamuzi huo leo asubuhi, Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Mahakama imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa mahusiano pekee yaliyosalia ni ya Mpangaji na Mpangishaji.

Pia Jaji Mwangesi amesema kuwa Mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.

Kuhusu kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa Mahakama wa kuendesha mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo alisema hiyo nayo haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.

NHC katika shauri hilo iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na Ipilinga Panya na mawakili wengine wa Shirika waliojikita katika kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na wateja wao

Mawakili wa Mbowe Hotels Mhe. John Mallya na Mhe. Peter Kibatala (pichani ) wakiongea na waandishi wa habari mara tu baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu kutoka, wakidai kwamba hawakuridhika na uamuzi wa kufutiliwa mbali kwa kesi ya mteja wao.

No comments: