Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari– MAELEZO Bw. Hassan Abbas amesema kuwa waandishi wa habari hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu muswada wa huduma za habari kwa vile hakuna mwandishi wa habari atakayefukuzwa au kuachishwa kazi kwa kigezo cha kutokuwa na elimu katika ngazi ya shahada ya kwanza.
Akizungumza katika kipindi cha mahojiano cha Clouds360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds, Bw. Abbas amesema hakuna haja ya waandishi wa habari kuuhofia muswada huu badala yake wausome na kuelewa na kisha watoe maoni yao ili kuuboresha zaidi.
“Sheria itatoa kipindi cha miaka 5 ili watu wajiendeleze katika taaluma hii ya habari, hivyo hakuna mwandishi wa habari atakayefukuzwa au kusimamishwa kazi kwasababu ya huu muswada kwa vile lengo ni kuwaandaa waandishi ili waweze kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia taaluma”alisema Bw. Abbas
Bw. Abbas aliongeza kuwa kigezo cha taaluma kwa wandishi wa habari hakitaainishwa katika sheria bali katika kanuni.
Aidha Bw.Abbas ameongeza kuwa katika historia ya masuala ya habari nchini huu ni muswada pekee unaolenga kulinda wanahabari kwani unazungumzia hali halisi ya mwandishi wa habari, ukilinganisha na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 inayozungumzia haki ya chombo cha habari pekee.
Muswada wa huduma za habari umetokana na maoni ya wadau baada ya kuona mapungufu katika sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo ilitungwa wakati ambapo hakukua na maendeleo makubwa katika sekta ya habarinchini.
Aidha,wadau na waandishi wa habari pamoja nchini wameombwa kuendelea kutoa maoni yao kwa kutuma barua pepe kupitia anuani yacna@bunge.go.tzilikutoa fursa ya kuboresha muswada huo kabla ya kuwa sheria.
No comments:
Post a Comment