TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI-SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI- TAREHE 11/10/2016
Ndugu wanahabari,
Leo Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu kinaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike
Duniani, siku ambayo ilipitishwa na
Umoja wa mataifa mnamo Oktoba 11,
2011. Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka
huu ni ‘‘Mimba na ndoa za Utotoni zinaepukika, Chukua hatua kumlinda mtoto wa
kike’’.
Hivyo basi katika kuadhimisha siku hii Kituo kimeangazia mtoto
wa kike hapa Tanzania na changamoto anazokumbana nazo. Kwa mujibu wa takwimu za
sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa kike kati ya umri wa
miaka 0-17 hapa Tanzania ni 11,263,891
idadi ambayo ni sawa na asilimia 48.8 ya watoto wote chini ya miaka 17, ambapo
Tanzania bara kuna watoto wa kike elfu 10,943,846 na Tanzania visiwani
idadi yake ni laki 320,045.
Hivyo basi
nusu ya idadi hii ni wanawake na watoto
ikilinganishwa na idadi ya watanzania wote ambao ni milioni 44,928,923 ambapo kati yao wanawake ni milioni 23,058,933.
Inasikitisha kuona kuwa
mtoto wa kike hapa nchini bado amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi na cha
kusikitisha zaidi mtoto huyu anaanza kubaguliwa kuanzia katika ngazi ya
familia.
Katika familia nyingi za kitanzania mtoto wa kike amekuwa akikosa
fursa ya kupata Elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira
mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao wa kike kwa ajili ya
kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume. Ukiangalia pia katika suala zima la
Elimu ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa kumaliza
masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Shirika la watoto duniani UNICEF kumekuwa na ongezeko la mimba mashuleni kutoka
asilimia 23 hadi 26 yaani takribani watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kila
mwaka hukatisha masomo kwa ajili ya ujauzito. Vile vile idadi ya watoto wa kike
ambao wamekuwa wakimaliza Elimu ya msingi lakini kutokupewa nafasi ya
kujiendeleza kielimu hata pale wanapokuwa wamefaulu nayo pia imekuwa
ikiongezeka na badala yake mabinti hawa wamekuwa wakilazimika kuingia katika
ndoa katika umri mdogo.
Ndugu wanahabari,
Hali hii ya Watoto wakike
kutokupata fursa ya elimu husababisha ongezeko kubwa la watoto wa kike
wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuletwa mijini kwa minajili ya kuja
kuendelezwa kielimu na matokeo yake mabinti hawa wamejikuta katika wakati mgumu
kwa kufanyishwa kazi za ndani bila malipo stahiki na wakifanyiwa vitendo vingi
vya kikatili na vya kuwadhililisha.
Hali hii imepelekea mabinti wengine
kutoroka kutoka kwa waajiri wao na kuanza kuishi mtaani na hivyo kurubuniwa na
kujiingiza katika biashara za ngono na wengine hata madawa ya kulevya.
Tumeendelea pia kushuhudia
kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono kama ubakaji na ulawiti kwa
Watoto wa kike na cha kusikitisha zaidi vitendo hivi vimekuwa vikifanywa na
Ndugu wa karibu sana wa Watoto hawa wakiwemo wazazi, walezi, majirani na hata walimu
huko mashuleni. matukio haya yamekuwa hayafikishwi Katika vyombo vya Sheria
kwani mengi huzungumzwa kifamilia na kuwaacha watuhumiwa wakiendelea na maisha
yao.
Ndugu wanahabari,
Tanzania pia ni nchi moja
wapo yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa takribani ya asilimia 35 watoto wa kike hapa nchini
huozeshwa nchini ya umri wa miaka 18 na hivyo kukatishwa ndoto zao za
kujiendeleza kielemu na hata ustawi mzima wa maisha yao.
Inasikitisha zaidi kuona
pia pamoja na juhudi mbalimbali za utetezi na ushawishi wa wanaharakati katika
kupinga vitendo hivi viovu na mila kandamizi bado Ukeketaji umekuwa ni tatizo
kubwa sana hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu za Viashiria vya Idadi ya watu na
afya 2010, asilimia 14.6% ya wanawake Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni
watoto wa kike. Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mbinu mpya zimekuwa
zikibuniwa ikiwemo kukeketa watoto mara
wanapozaliwa. Vilevile, kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu ya mwaka 2015
inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kila mwaka ongezeko la
matukio ya Ukatili kwa watoto ikiwemo watoto wa kike kupewa adhabu kali ambazo
hazilingani na makosa waliyoyafanya, mfano unakuta mtoto anachomwa mikono moto
kwa kosa la kuunguza mboga.
kwa kifupi watoto wa kike
wanapata athari mbalimbali ikiwemo;
1. Kuendelea
kudidimiza nafasi ya mwanamke katika Jamii na taifa zima kwa ujumla na
kuendeleza mfumo dume kwani ukatili mwingi huanzia katika ngazi ya familia
2. Kutokuendelezwa
kielimu kwa mtoto wa kike na hii hupelekea kuendelea kuwa na idadi kubwa ya
Wanawake ambao hawana Elimu na hivyo kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume na pia
kushindwa kujikwamua kiuchumi.
3. Idadi
kubwa ya athari za kiafya zinazowapata watoto wa kike kwa ajili ya kujifungua
katika umri mdogo ambayo husababisha wengine kupoteza maisha, kupatwa na
fistula na maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na magonjwa mengine ya zinaa.
4. Malezi
duni ya watoto kwa kuwa watoto hawa wanakuwa bado ni wadogo kuweza kukabiliana
na jukumu kubwa la malezi na matunzo ya familia.
5. Kuendelea
kuongezeka kwa Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwani watoto hawa mara nyingi
huolewa na watu waliowazidi umri sana na hivyo kutokuwa na maamuzi yoyote
katika nyumba.
Hivyo basi tunapendekeza yafuatayo:
1. Katika
ngazi ya familia wazazi na walezi kuthamini na kuwajali watoto bila ubaguzi wa
jinsi zao. Watoto wote wapewe fursa sawa kielimu na kujiendeleza kimaisha.
Wazazi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili hasa Ukatili
unaoanzia majumbani,sambamba na hilo kutoa taarifa za matukio ya Ukatili
wanayofanyiwa watoto na sio kutatua matatizo haya katika ngazi ya familia
ilihali haki ya mtoto inapotezwa.
2. Wito
kwa Jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya
Ukatili. Kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona mtoto wa mwenzako ni wa kwako;
pia kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili katika maeneo wanayoishi na sio
kufumbia macho na kuwaficha waovu.
3. Serikali
kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinasimamiwa na zinatekelezwa pale
zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyowazi na rahisi ya kupata na kufuatilia
haki. Vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa ni kandamizi kwa mtoto
wa kike ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki mtoto wa kike kuolewa
katika umri wa miaka 15. Serikali itekeleze agizo lilitolewa na Mahakama Kuu
Julai 8 2016 la kubadili kifungu na 13 cha sheria ya ndoa 1971 juu ya ndoa za
utotoni
4. Serikali
kwa kupitia taasisi zake kama polisi na mahakama kuhakikisha kuwa Mashauri
yanapolekwa Mahakamani yanasikilizwa bila vikwazo na kutolewa maamuzi kwa wakati
stahiki maana ‘justice delayed is justice denied’ - ‘kuchelewesha haki ni kunyima
haki’.
5. Wito
kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili
wanayofanyiwa watoto ili wale wanaofanya vitendo hivi waaibishwe na waadhibiwe
kwa mujibu wa sheria; tunavitaka vyombo vya Habari visiishie tu kuripoti
matukio haya pindi yanapofanyika bali hata kuendelea kufuatilia mashauri
yaliyopo mahakamani ili kusaidia mashauri haya yafanyiwe kazi kwa wakati.
6. Pamoja
na hilo tunaviomba vyombo vya habari kuwa makini jinsi wanavyoripotia matukio
haya ya Ukatili kwa watoto kwani utoaji wa taarifa hizi wakati mwingine umekuwa
pia ukiendelea kuwavunjia haki watoto hawa kwa kutozingatia sheria inayotaka
utoaji wa taarifa za watoto kutunza majina halisi ya watoto na hata sura zao.
7. Na
mwisho kabisa tunaomba viongozi wetu katika ngazi zote za kijamii na hata
kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususani haki za watoto wa kike
kama ajenda ya kitaifa ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo viovu na
wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na mustakabali mzuri wa maisha
yao ya sasa na ya baadae.
Tunawashukuru
sana.
Wasalaam,
Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu
………………………………
Dr.
Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi
Mtendaji
No comments:
Post a Comment