Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba (katikati), Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio (kulia) na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga , wakionesha jarida la kupinga adhabu ya kifo wakati wa uzindi wake Dar es Salaam leo. |
Wakati leo ulimwengu
mzima ukiadhimisha siku ya kupinga Adhabu
ya kifo kituo cha sheria na haki za Binadamu nchini Tanzania LHRC
wameendelea kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa serikali kufuta adhabu hiyo ambayo ipo na kutafuta adhabu mbadala kwenye
makosa ya jinai na kwa wafungwa waliopo,vikiwemo vifungo vya muda mrefu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akisoma tamko la kupinga adhabu ya kifo. Kulia ni Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio na kushoto ni Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga.
|
Akizungumza na wanahabari
leo makao makuu ya shirika hilo Kijitonyama Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji
wa LHRC Bi Hellen Kijo Bisimba amesema kuwa adhabu ya kifo ni adhabu ambayo
inakwenda kinyume na haki za Binadamu,ambapo amesema kuwa adhabu hiyo imekua
ikiathiri kwa kiwango kikubwa haki ya msingi ya kuishi kwa kuwa ni adhabu
inayodhalilisha utu wa Binadamu.
Ameongeza kuwa Tanzania
imeridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo inaweka wajibu wa
kulinda haki hiyo pamoja na kuipa ulinzi ndani ya sheria za nchi ambapo ametaja
mikataba hiyo kuwa ni pamoja na Tamko la kimataifa la haki za Binadamu la mwaka
1948 ibara ya 3,Mkataba wa haki za kiraia na kisiasa wa mwaka 1966 (ICCPR)
ambao katika ibara ya 6 umeeleza bayana kwamba “Kila mtu anayo haki ya asili ya kuishi haki hii italindwa chini ya sheria
na mtu yeyote hatakuwa na mamlaka kuondoa uhai wa mtu kiholela” huku pia
mkataba wa Africa wa haki za binadamu na haki za watu wa mwaka 1981 nao katika
ibara ya 4 imeanisha “kila binadamu
anastahili heshima ya utu wake na haki hiyo haipaswi kuvunjwa”
Ameongeza kuwa kutokana
na mkikataba hiyo ambayo Tanzania ni mmoja kati ya mataifa yanayofwata ni
lazima tuondoe adhabu ya kifo nchini kwani inakwenda kinyume na mikataba hiyo
ya kimataifa na kikanda.
Aidha ameongeza kuwa
adhabu ya kifo nchini Tanzania haikuanzia nchini kwetu bali ni sheria ambayo
ililetwa na wakoloni ambapo adhabu hiyo imeainishwa kwenye sheria ya kanuni ya
adhabu sura ya 16 “Penal Code” ambayo nayo ililetwa na utawala wa kikoloni
mwaka 1945 na kuendelea kuwa moja ya sheria zetu hata baada ya uhuru wa
Tanzania licha ya marekebisho ya mwaka 2002.
Takwimu zinaonyesha
kuwa hadi kufikia mwaka 2015 jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa
ambao kati yapo 452 ni wanaume na 20 ni wanawake,na kati ya hao wanaosubiri kunyongwa
ni 228 na wengine 244 wanasubiri maamuzi ya Rufaa zao.ambapo licha ya adhabu
kutokutekelezwa nchini kwa Takribani miaka 22 na miaka 24 ya kwanza ya uhuru
Taarifa zinaonyesha kuwa ni watu 72 ambao walishawahi kunyongwa kutokana na
adhabu hiyo..
Akitaja sababu ambazo zinawafanya
wanaharakati hao kupinga adhabu hiyo ya kifo Bi Hellen Kijo Bisimba pamoja na
sababu nyingi ambazo wamezitaja amesema kuwa adhabu ya kifo ni adhabu ya
kinyama,na isiyo na staha,ni adhabu ya kibaguzi maana wanaopatikana na hatia na
kupewa adhabu hii mara nyingi huwa ni maskini wasioweza kuwa na mawakili,lakini
pia hakuna ushahidi wa moja kwa moja ambao unaonyesha kuwa adhabu hii inazuia
watu wengine kutokutenda makosa kama hayo.
Wanahabari wakichukua Taarifa Hiyo |
Wakati tukiadhimishwa
adhabu hii ya kifo nchini Tanzania Taarifa
zinaeleza kuwa duniani kote adhabu hii imeshafutwa katika mataifa
yapatayo 140 na kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Amnesty kati ya nchi hizo
140 nchi 17 ni nchi za Africa zikiwemo Rwanda,Burundi,Msumbiji,Visiwa vya
shelisheli,na Madagascar,Namibia,na Africa kusini pamoja na nchi nyingine,jambo
ambalo LHRC wanaeleza sasa ni wakati wa Tanzania kuiga mfano huo na kufuta sheria
hiyo Kandamizi na kutafuta mbadala wa adhabu nyingine kali kwa watuhumiwa wa
makosa makubwa.
No comments:
Post a Comment