KITUO cha kukuza vipaji cha Green Sports Academy kutoka jijini Nairobi, Kenya kinatarajia kufanya ziara maalumu kwenye makao makuu ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC.
Ziara hiyo ya siku sita itakayoambatana na mechi za kirafiki, itaaanza rasmi Desemba 20 jioni watakapowasili nchini hadi Desemba 25 mwaka huu watakaporejea nchini kwao.
Green Sports itakuja nchini ikiwa na timu zake nne za umri tofauti chini ya miaka 13, 15, 18 na 21, ambapo itacheza mechi tatu za kirafiki kuanzia Desemba 22, 23 na 24 dhidi ya timu za vijana za Azam FC.
Uongozi wa kituo hicho kupitia kwa Mkurugenzi wa Ufundi, Stephen Ochiel Otieno, umetoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Azam FC kwa kuwakubalia ziara hiyo ya kuja hapa nchini.
Otieno amesema kuwa hiyo itawahamasisha sana vijana wadogo wenye vipaji kuelekea kuwa nyota wa kimataifa katika siku za usoni, huku pia kwa upande wao wakiangalia mbele kuendeleza ushirikiano wa kudumu na Azam FC, ambayo kwa sasa ndio klabu bora iliyowekeza kwa vijana katika ukanda huu.
Huu ni ugeni mkubwa wa pili kwa mwaka huu kwa Azam FC ikihusisha kituo cha kukuza vipaji, wa mara ya kwanza ulikuwa ni mwezi Juni ilipozialika timu mbili za Afrika Mashariki, Football For Good Academy ya Uganda na Ligi Ndogo Academy ya Kenya kwenye michuano ya Azam Youth Cup 2016, ambayo pia iliishirikisha Future Stars Academy ya Arusha na kushuhudiwa wenyeji Azam FC Academy ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo
No comments:
Post a Comment