BAADA ya kupona majeraha ya nyonga, beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amesema kuwa hivi sasa anapambana vilivyo kurejesha makali yake yaliyomfanya akubalike na mashabiki wa timu hiyo.
Beki huyo kipenzi wa mashabiki wengi wa soka nchini, amerejea mazoezini hivi sasa kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), alishindwa kuitumikia vema timu hiyo baada ya kukosa mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza wa ligi kufuatia majeraha hayo.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kapombe alisema kuwa kwa sasa anazidi kujiandaa vema kupitia mazoezi wanayopewa na benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na mengine binafsi anayoyafanya peke yake.
“Mimi binafsi nimejiandaa vizuri na naendelea kujiandaa vizuri kwa mazoezi ambayo tunapewa na mengine ya kwangu binafsi, yote hayo nafanya ili kupambana na kurejesha makali yangu ili kuisaidia Azam FC,” alisema.
Kapombe alisema kwa sasa anaendelea vizuri na afya yake ipo vizuri kabisa kuweza kupambana kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mzunguko wa pili wa ligi unaoanza Jumamosi ya wikiendi hii.
Sura mpya dirisha dogo
Kapombe pia alifurahishwa na namna wachezaji wapya waliosajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili, ambapo amedai kuwa ni wachezaji wazuri na anaamini ya kuwa wataisadia sana Azam FC kuelekea mechi za mzunguko wa pili.
“Mpaka sasa kuna sura mpya ambazo zimeongezwa, ni wachezaji wazuri wanaokuja kuziba mapungufu ambayo tumayaona mzunguko wa kwanza, kila mchezaji aliyekuja hapa anasifa yake na uzuri wake kuweza kuisaidia timu yetu katika kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.
Hajawaacha mashabiki
Beki huyo mwenye sifa ya kupandisha mashambulizi kwa kasi na uwezo kufunga mabao, aliyeweka nyavuni mabao 11 msimu uliopita, kuelekea raundi ya pili ya ligi amewaachia ujumbe mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa waunganishe nguvu kuwasapoti uwanjani katika mechi zao.
“Mimi ninachowaomba mashabiki wa Azam FC ni waendelee kuwa nasi katika vipindi vyote vya shida na raha, waunganishe nguvu na waendelee kutusapoti katika mechi za raundi ya pili ili na sisi tuweze kufika pale Azam FC inapohitajika kufika,” alimalizia.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola, kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili pamoja na Benki bora kwa usalama wa fedha zako ya NMB, inatarajia kufungua ng’we ya mzunguko wa pili kwa kukipiga na African Lyon Jumapili hii Desemba 18 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam saa 10.00 jioni.
No comments:
Post a Comment