KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo asubuhi imeanza rasmi maandalizi ya kuikabili Majimaji katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, Ruvuma Jumamosi hii.
Azam FC iliweza kutoka suluhu dhidi ya African Lyon juzi kwenye mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi.
Wakati kikianza maandalizi hayo, taarifa iliyopo ni kuwa kikosi hicho kinatarajia kuanza safari ya kuelekea mkoani humo alfajiri ya kuamkia kesho Jumatano, ambapo kitamalizia maandalizi ya mwisho kikiwa mkoani humo.
Kikosi hicho kimeanza kujiandaa na mtanange huo kikiwa na nguvu mpya, ambapo ni wachezaji watatu tu waliokosekana, beki Abdallah Kheri, kiungo Mudathir, wote wakiwa wagonjwa na beki Gardiel Michael, anayeendelea na matibabu ya mkono wake wa kushoto ambao umeteguka.
Beki Ismail Gambo, naye leo ameendelea na programu ya ‘gym’ chini ya uangalizi wa mtaalamu wa viungo, Sergio Perez Soto, kutokana na majeraha ya goti yanayomsumbua aliyoyapata wakati Azam FC ikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Ruvu mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema kuwa ametumia programu ya leo kuwaunganisha wachezaji huku akidai kuwa maandalizi makubwa watayafanya wakifika Songea kutokana na muda kubana.
“Tunatarajia kufanyia kazi na kurekebisha udhaifu ulioonekana kwenye mchezo uliopita, kikubwa tutajitahidi kuweza kupata ushindi kwani ni moja ya malengo yetu kuelekea huko na kurejea na pointi tatu,” alisema.
Alisema kwenye mchezo uliopita walifanikiwa kucheza vizuri lakini hawakuwa na bahati ya kuweza kufunga bao, huku akidai kuwa anatarajia kulifanyia kazi suala hilo ili lisiweze kujitokeza katika mechi inayokuja.
“Kama uliona wachezaji waliweza kufanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wetu, wachezaji walijitahidi kupiga mashuti, safu yetu ya ulinzi haikupata shida sana na ilikuwa imara muda wote wa mchezo, jambo ambalo tulilikosa raundi ya kwanza,” alisema.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachoburudisha koo lako na kuchangamsha mwili na Benki ya NMB, kabla ya kuelekea Songea inatarajia kufanya mazoezi mengine leo saa 12.30 jioni.
Mabingwa hao wa Ngao Jamii mwaka huu, mpaka sasa wamefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 26 kwenye ligi baada ya kushinda mechi saba, sare tano na kupoteza michezo mine, ambapo inazidiwa pointi 12 na kinara Simba aliyekusanyia 38 huku Yanga iliyonafasi ya pili ikijizolea 36
No comments:
Post a Comment