Friday, December 30, 2016

PHIRI:FITI DHIDI YA MBAO,NGASSA KUANZIA BENCHI

img_0983

ZIKIWA zimesalia  saa kadhaa kabla ya kuchezwa kwa mchezo wa ligi  kuu ya Vodacom Tanzania  bara  kati  Mbeya City fc na Mbao Fc kutoka jijini Mwanza uliopangwa  kuchezwa  kesho  jumamosi kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine  jijini hapa, kocha Kinnah Phiri amesema  maandalizi  kwa timu yake kuelekea mchezo huo yamekamilika  kinachosubiriwa ni dakika 90 huru za ndani ya uwanja.

Muda mfupi uliopita kocha Phiri ameidokeza mbeyacityfc.com kuwa amekamilisha maandalizi kwa kufanya marekebisho makubwa kwenye mapungufu kadhaa yaliyoonekana kwenye michezo miwili iliyopita yaliyoiacha City ikiambulia pointi mbili za suluhu mbele ya Kagera Sugar na Toto Africans ya Mwanza.Mchezo wa kesho ni muhimu, tumejitahidi kurekebisha mapungufu yote yaliyokuwepo kikosini kwenye michezo miwili iliyopita,vijana wangu wako ‘fiti’ na wameniahidi watafanya  vizuri, ni jambo jema kusikia hivyo kutoka kwao  hii ni kwa sababu  kila mmoja anataka  tushinde, wapo  wachezaji kadhaa tutawakosa kwa sababu ni wagonjwa, Danny Joram na Omary Ramadhani hawakuwepo kabisa kikosini.
Kuhusu kiungo Mrisho Ngassa na  mshambuliaji  Zahor Pazzi, kocha Phiri amesema wanaweza kuwa sehemu ya kikosi cha kesho lakini watalazimika kuanzia kwenye bechi  na kuingia baadae hii ni kwa sababu  wamefanya mazoezi kwa siku chache hivyo hawako sawa asilimia 100.
Hawako fiti asilimia 100, watakuwepo kikosi lakini tunaweza kuwatumia kipindi cha pili, siku mbili nyuma Ngassa  alikuwa  anasumbuliwa na tumbo, leo amefanya mazoezi  mapesi, kwa mujibu wa daktari ni wazi hatuwezi kumtumia muda wote  wa mchezo, hivyo hivyo kwa Pazzy ambaye amefanya mazoezi kwa siku tatu sasa.

No comments: