Tuesday, January 24, 2017

BIASHARA 5 UNAZOWEZA KUZIFANYA JIJINI DAR ES SALAAM NA KUKUINGIZIA KIPATO

Na Jumia Travel Tanzania

Kuishi katika jiji kubwa kama vile Dar es Salaam kuna changamoto nyingi endapo hauna shughuli maalum ya kukuingizia kipato cha kila siku. Na ili kufanikiwa katika hilo basi huna budi kuwa mwerevu wa kugundua ni biashara ipi ukiifanya itakuwa inakuingizia kipato cha haraka.


Kama unaishi au ulikuwa na mpango wa kuja kutafuta maisha jijini Dar es Salaam, Jumia Travel inakushauri kujaribu kufanya shughuli zifuatazo ili kukuingizia kipato:


Kuuza vinywaji baridi (maji, soda, juisi, n.k.)

Kwa kipindi kirefu hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam huwa ni joto na jua kali, hivyo kupelekea uhitaji na utumiaji mkubwa wa vinywaji baridi. Hii ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara kwani watu hawawezi kuvumilia jua kali bila ya kutumia vinywaji kama vile maji, soda au juisi. Mtaji wa biashara hii sio mkubwa sana na haihitaji ofisi, kitu ambacho kinamuwezesha mtu yeyote kufanya biashara hii.  

Kuuza matunda
Wakazi wa jiji hili hupendelea matunda katika milo yao tofauti iwe ni asubuhi, mchana au usiku. Biashara hii ni nzuri kwa kigezo kikubwa kwamba watu hawana mashamba, matunda mengi huingizwa kutoka mikoa mingine. Mtaji wa biashara hii ni mdogo na sehemu nzuri za kupatia wateja ni kwenye vituo vya mabasi, pembezoni mwa barabara, karibu na migahawa au karibu na ofisi.

Kuuza magazeti

Magazeti ni nyenzo mojawapo ya kupatia habari ambayo wakazi wengi wa Dar es Salaam huitumia. Kutokana na kutingwa na shughuli nyingi, wengi wao huwa hawana muda wa kupitia kwenye sehemu maalum zinazouza magazeti. Njia pekee ya kuwafikia ni kwenye foleni za magari asubuhi wanapokwenda na jioni wanaporudi kwenye shughuli zao. 

Uchuuzi wa vyakula vya baharini (Pweza, ngisi, dagaa kamba, n.k.)
Kijiografia Dar es Salaam imepakana na bahari ya Hindi kwa sehemu kubwa na kupelekea upatikanaji wa vyakula vya baharini kuwa rahisi. Vyakula kama vile samaki wa aina tofauti, pweza, ngisi, dagaa kamba na kadhalika ni baadhi ya vinavyopendwa na wakazi wengi. Biashara hii ni rahisi kuifanya kwani haihitaji mtaji mkubwa wala ofisi na pia hivyo vyakula huuzwa kwa gharama ndogo ambayo kila mtu anaweza kuimudu. Hufanyika muda wa jioni kandokando ya barabara na kwenye vituo vya mabasi ambapo watembea kwa miguu na abiria wengi hupita wakirejea makwao.   

Kuuza vocha za muda wa maongezi wa kwenye simu

Faida ya kuishi kwenye jiji hili ni kwamba makampuni na taasisi zote kubwa ofisi zake zinapatikana hapa. Hali hiyo hutoa fursa kwa wafanyabiashara kuwa mawakala ili kuwafikia wateja wa kawaida. Mojawapo ya huduma muhimu inayotumika muda wote ni huduma za simu za mkononi kwa ajili ya mawasiliano ambapo si chini ya makampuni matano yanaendesha shughuli zake. Hii hupelekea wanaouza vocha za muda wa maongezi kuwa na uhakika na biashara zao.

Hizo ni baadhi tu ya biashara ndogondogo ambazo zitakufanya uishi vizuri katika jiji la Dar es Salaam ambalo bila ya shughuli maalum ya kufanya si rahisi kulistahimili. Jumia Travel inaamini dondoo hizi zitakuamsha wewe mkazi au mwenyeji ambaye ulikuwa unajiuliza nini cha kufanya ili ujiingizie kipato kwa urahisi.

No comments: