Katibu Mkuu Wizara ya Mambo
ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa wizara kuwa
tayari kutekeleza majukumu yao katika mazingira ya Makao Makuu ya Serikali mkoani
Dodoma na wale wanaobaki Dar es salaam katika kipindi hiki cha mpito kuzingatia,
hali itakavyokuwa kulingana na sheria, kanuni taratibu na miongozo na maelekezo
ya kiutumishi.
Prof Mchome ametoa rai hiyo
katika kikao cha pamoja na watumishi wa wizara kilichofanyika mjini Dar es
salaam ili kuwekana sawa kufuatia kuanza kuondoka kwa kundi la kwanza la
watumishi wa Wizara kuelekea makao makuu ya Serikali mjini Dodoma.
Prof Mchome amewataka
watumishi kujiweka tayari katika kila hali kwa kuwa Wizara imeanza kutekeleza
agizo la kuhamia makao makuu ya Serikali na kuchukua hatua stahiki katika
kukabiliana na changamoto zitakazo jitokeza katika utekelezaji wa zoezi la
kuhamia makao makuu.
“Nimewaita tuagane, mimi na
viongozi wenzangu na watumishi wengine tunaanza safari ya kuhamia Dodoma,
tumepeana wiki ijayo kuwa tumefika Dodoma kuanzia Januari 23 ili tuanze
kujipanga, muwe tayari, kipindi hiki ni cha mpito, kina changamoto zake kama
ilivyo katika maisha ya binadamu, hakuna kitu rahisi katika kuhama, kuanzia kwa
mtumishi binafsi hadi kwa ofisi, lakini mkijiweka sawa mkawa macho na makini
nina hakika sote kwa pamoja tutaweza kukabiliana na changamoto hizo,” alisema
Prof Mchome
Awamu ya Kwanza yenye
watumishi 25 wa wizara wakiongozwa na
Waziri Dkt Harrison Mwakyembe , Katibu Mkuu Prof Mchome na Naibu Katibu Mkuu Bw.
Amon Mpanju imeanza kuondoka mjini Dar es salaam kuanzia Januari 15, watakuwa
wanaendelea kuwasili mkoani Dodoma hadi wiki ijayo na Wizara inatarajia
kuzindua rasmi ofisi yake mkoani Dodoma Jumanne ya Januari 31, 2017.
No comments:
Post a Comment