Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chama, Dkt. Vincent Mashinji ni miongoni wa wageni mashuhuri walioalikwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Ghana, Nana Addo Dankwa Akufo-Addo na Makamu wake, Dkt. Alhaji Mahamudu Bawumia, itakayofanyika Jumamosi, Januari 7, mwaka huu jijini Accra.
Viongozi wakuu hao ambao wameondoka nchini usiku wa Januari 6, kuelekea Accra, pia watahudhuria kuapishwa kwa Spika wa Bunge la Ghana, pamoja na Wabunge 275, waliopatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Aidha, Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu Dkt. Mashinji wamepewa heshima ya kufanya mazungumzo na Rais Nana Akufo-Addo yatakayofanyika Jumapili ya Januari 8, baada ya kupata chakula cha mchana pamoja.
Kabla ya hapo, mapema asubuhi ya siku hiyo, viongozi wakuu wa CHADEMA watakuwa sehemu ya msafara utakaomsindikiza Rais Nana Akufo-Addo, kwenda kwenye ibada ya asubuhi, itakayofanyika eneo la Kyebi, kisha jioni msafara utarejea jijini Accra kuendelea na ratiba zingine.
Huu ni mwendelezo wa urafiki na uhusiano wa karibu kwa muda mrefu sasa, kati ya Chama cha Rais Nana Akufo-Addo cha New Patriotic Party (NPP) pamoja na CHADEMA, tangu vilipokutanishwa kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) na ule wa Afrika (DUA).
Viongozi wengine mashuhuri kutoka Afrika walioalikwa katika sherehe hizo ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Forum for Democtratic Change (FDC), Kizza Besigye, kutoka Uganda.
Imetolewa leo Ijumaa, Januari 6, 2017 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
No comments:
Post a Comment