TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU
UTEUZI WA WABUNGE WA KUTEULIWA NA NAFASI NYINGINE ZA UTEUZI UNAOFANYWA NA RAIS
19/01/2017
Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu kimetathmini mwenendo wa
masuala ya kijinsia katika teuzi mbali mbali zinazofanywa na Serikali katika
nafasi mbalimbali za uongozi nchini Tanzania.
Katika tathmini yetu
tumejikita zaidi kuangalia katika muktadha wa Haki za Binadamu na haki za Wanawake kwa kuzingatia mikataba mbalimbali ya
kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia kuhusu usawa wa kijinsia vile
vile kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano w Tanzania ya mwaka 1977 na pia sheria
nyinginezo.
Tukianza na kikanda,
Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa nchi za kusini mwa Afika na hivyo
imeridhia mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika yaani
SADC Gender Protocol ambapo mkataba huu katika Ibara ya 12 inazitaka nchi
wanachama kuhakikisha kuwa katika ngazi zote za maamuzi kuna usawa wa kijinsia
wa asilimia 50 kwa 50. Pia Mkataba wa Afrika wa Haki za Wanawake (Maputo
Protocol) unapinga ubaguzi dhidi ya wanawake katika ngazi za maamuzi.
Kimataifa, Mkataba wa
kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) Katika Ibara ya 7
inazitaka nchi wanachama wa mkataba huo kuhakikisha wanawake wanashirki
kikamilifu katika kutunga sera, sheria na kuwa katika ngazi za utekelezaji wa
sera na sheria hizo (ngazi za maamuzi).
Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Ibara ya 13 inaeleza jinsi ambavyo serikali itachukua
hatua za makusudi kurekebisha matatizo yaliyo katika jamii ili kuondoa ubaguzi.
Katika jamii kuna mfumo dume na mifumo mingine kandamizi ambayo imesababisha
wanawake wengi kukosa fursa ya kusoma, kuwa na kipato kidogo, kutopata nafasi
ya kuwa viongozi na kadhalika. Hii
imepelekea wanawake wengi kushindwa kugombea na kuwa wachache katika ngazi za
maamuzi. Ndio maana jitihada mbalimbali
za makusudi zinapaswa kufanyika ili kuweka nafasi maalum kwa ajili ya kurekebisha
tatizo hilo katika jamii.
Katika
muktadha huo Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetoa mwongozo katika teuzi
mbalimbali, kwa mfano Wabunge wateule wa Rais. Ibara ya 66 (1) (e) inasema na
tunanukuu:
‘… Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibara hii, kutakuwa
na aina zifuatazo za Wabunge, yaani:-…(e) Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa
na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na
(c) za ibara ya 67 na angalau wabunge
watano kati yao wakiwa wanawake...”
Ibara hiyo ya katiba
inamaanisha kuwa katika kuteua wabunge wa kuteuliwa na Rais anapaswa
kuhakikisha idadi ya wanawake haipungui watano; Neno angalau maana yake sio
chini ya.
Katika kufanya tathmini ya
wabunge walioteuliwa na Rais, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimebaini
kuwa mpaka sasa Rais ameshateua wabunge kama ifuatavyo:
1. Mhe.
Dr. Tulia Ackson (KE)
2. Mhe.
Prof. Joyce Ndalichako (KE)
3. Mhe.
Dr. Abdalla Possi (ME)
4. Mhe.
Dr. Augustine Philip Mahiga (ME)
5. Mhe.
Dr. Phillip Isdor Mpango (ME)
6. Mhe.Prof.
Makame Mnyaa Mbarawa (ME)
7. Mhe.Prof.
Abdallah B ulembo (ME)
8. Prof.
Palamagamba Kabudi (ME)
Katika hao
watajwa hapo juu idadi ya wanaume tayari wako sita, ambapo ukwelihuu unakinzana
na ibara ya 66(1) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Hata Rais akichagua wanawake tu katika nafasi
zilizobakia, bado haitakidhi haja ya kuwa na wanawake watano au zaidi kwa
mujibu wa Katiba.
Pia tumeangalia katika
nyadhifa zingine za uteuzi unaofanywa na Rais kama Mawaziri na Manaibu waziri,
Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri bado idadi ya wanawake
imekuwa chini sana na hivyo kutokuzingatia ulinganifu wa kijinsia. Kwa mfano
idadi ya mawaziri wanawake ni 4 tu kati ya 19, kati ya wakuu wa mikoa 26 wanne
tu ndio wanawake, kati ya wakuu wa Wilaya 134 wanawake ni 25 tu na kati ya
wakurugenzi wa halmashauri na Wilaya 185 wanawake ni 33 tu.
Kutokana na hali hiyo,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitaka
Serikali na mamlaka nyingine za uteuzi;
i)
Kuzingatia Sheria na Katiba katika teuzi
mbalimbali katika nafasi za uongozi.
ii)
Kufuata misingi ya Haki za Kijinsia kwa
mujibu wa mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Serikali imesaini na
kuridhia.
iii)
Kuzingatia usawa wa kijinsia na kuchukua
hatua za maksudi (affirmative action)
ili kuwa na jamii yenye haki na usawa katika suala la uongozi wa nchi.
iv)
Rais
aone uwezekano wakurekebisha hii hali iliojitokeza ya kukiuka maelekezo ya
katiba
Imetolewa leo tarehe 19
Januari 2017 na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu.
Dkt. Helen
Kijo-Bisimba
Mkurugenzi
Mtendaji
No comments:
Post a Comment